Ushindi mnono wa mabao 3-1 waliopata Simba Sc kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Premiero De Agosto uliopigwa Uwanja wa Novemba 11 nchini Angola umewafanya kuingiza mguu mmoja katika hatua ya makundi.
Katika mchezo huo, Clatous Chama aliipatia Simba bao la kwanza dakika ya nane baada ya kumpiga chenga mlinzi mmoja wa De Agosto na kupiga shuti kali la chini chini akimalizia krosi iliyopigwa na Augustine Okrah.
Baada ya bao hilo Simba iliendelea kulishambulia kwa zamu ambapo dakika ya 42 alimanusura Chama atupie bao la pili kufuatia krosi iliyopigwa na Israel Patrick kumgonga mguuni.
Kipindi cha pili wenyeji De Agosto walirudi kwa kasi ambapo dakika 10 za mwanzo waliliandama lango la Simba ingawa walinzi walisimama imara kuhakikisha tunakuwa salama.
Mlinzi wa kulia Israel Patrick alifunga bao la pili dakika ya 62 kwa shuti kali ndani ya 18 akimalizia pasi ya Sadio Kanoute kufuatia shambulizi lililoanzishwa na Mzamiru Yassin.
Moses Phiri hakubaki nyuma aliifungia Simba bao la tatu dakika ya 75 baada ya kumalizia pasi safi ya Chama ambalo halikudumu kufuatia De Agosto kufunga muda huo huo kwa mkwaju wa penati lililofungwa Tshibamba Dago.Kocha Juma Mgunda alifanya mabadiliko ya kuwatoa Okrah, Kibu Denis na Phiri na kuwaingiza Kennedy Juma, John Bocco na Pape Sakho.
Ushindi huu umeiweka Simba kwenye mazingira mazuri ambapo katika mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo jijini Dar es Salaam watahitaji ushindi wowote au sare ili kutinga hatua ya makundi.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.