Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 23
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 23 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA....!!! “Sawa. Hakikisheni mnawatesa sana mpaka wawaambie ukwel...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 23
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 23
ILIPOISHIA....!!!“Sawa. Hakikisheni mnawatesa sana mpaka wawaambie ukweli. Umenielewa?” aliuliza upande wa pili.
“Ndiyo mkuu!”
“Basi sawa. Nataka nipewe taarifa nzuri baada ya saa moja.”
“Hilo ondoa shaka, nitafanya hivyo,” alisema jamaa huyo na kukata simu. Kazi iliyobaki ilikuwa ni kuwateka watu hao tu. Vijana wakaandaliwa na kuanza kwenda huko.

ENDELEA NAYO SASA.......
Ilikuwa ni lazima watu hao watekwe na kupelekwa katika mapango ya Djara yaliyokuwa Qesm Al Wahat Ad Dakhlah, pembeni kidogo mwa Jiji la Cairo. 

Walichokifanya wanaume hao ni kwenda huko hospitali na kufanya kile walichoambiwa wafanye kwani ilikuwa ni lazima ndani ya saa chache watu hao watekwe na kupelekwa katika mapango hayo.

Wakaondoka, walipofika huko wakaelekea mpaka katika korido ya chumba alichokuwa Saida na kusubiri kwa nje. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu nao, walionekana kuwa watu wa kawaida kwani hata mavazi yao tu yalionyesha kwamba walikuwa watu wazuri.

Madaktari hawakuwauliza kitu chochote kile, waliendelea na shughuli zao huku wakiwaona watu hao wakiwa mahali hapo. Mbali na wao, pia kulikuwa na watu mbalimbali waliokuwa wakiwatembelea wagonjwa zao, na hiyo ndiyo iliwapa uhakika madaktari kwamba watu hao nao walikuwa wamefika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwaona wagonjwa wao.

Baada ya kukaa kwa saa kadhaa, Kareem akarudi hospitalini hapo, yeye mwenyewe hakuonekana kuwahofia watu hao, ndiyo kwanza akakaa karibu naye huku wote wakitaka kuingia ndani ya chumba hicho.

Kareem hakuonekana kuwa na furaha, moyo wake ulikuwa na huzuni kubwa, hakuamini kama kweli yeye na mpenzi wake ndiyo walikuwa wakipitia maisha hayo. Kila kitu kilibadilika, hakujua ni kitu gani kiliendelea nyumbani kwao, hakujua kwamba baba yake alikufa baada ya ndege kupotea.

Kitu pekee alichokuwa akikiangalia kwa wakati huo ni maisha yake na mpenzi wake. Alibaki hapo kwenye kiti mpaka pale daktari alipomwambia kwamba alitakiwa kumuona mgonjwa wake, akasimama na kuingia ndani.

Bado Saida alikuwa kitandani, alikuwa hoi na mashine ya kupumulia ndiyo iliyokuwa ikimsaidia kupumua, alisikitisha mno na muda wote alipokuwa akimwangalia, Kareem alikuwa akibubujikwa na machozi tu.

Alikaa humo kwa dakika thelathini, akatoka na kuondoka kwani tayari muda wa kuona wagonjwa ulikuwa umepita. Alikwenda mpaka hotelini, hakutaka kusikia kitu chochote kile kilichokuwa kikiendelea, huko, alikuwa mtu wa kulala tu.

Wakati yeye akiwa hotelini, tayari wanaume wale wakajiandaa kufanya kazi yao, muda ule waliokuwa wamekwenda huko ilikuwa ni kwa ajili ya kuangalia mazingira, baada ya kuona hakukuwa na tatizo lolote lile, wakaondoka, waliporudi wakawa na makoti makubwa ya kidaktari.

Walifanana na madaktari, hata watu wengine walipowaangalia, waliamini kwamba jamaa hao walikuwa madaktari. Wote kwa pamoja wakaingia ndani, humo, hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya Saida ambaye bado alionekana kuwa kwenye hali mbaya.

“Tumchukueni...” alisema jamaa mmoja.
“Hatutoweza kutoka naye salama!”
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Ni lazima tumteke dokta mkuu! Yeye ndiye atakayetufanya tutoke ndani ya chumba hiki tukiwa salama,” alisema jamaa mwingine.
“Tuondoke na huyu tu? Vipi kuhusu yule mwanaume?”
“Hatakiwi kuachwa, kazi itaanza mpaka atakapokuja,” alisema jamaa huyo.

Hilo ndilo lililotakiwa kufanywa, ilikuwa ni lazima kuondoka mahali hapo wakiwa na watu wote wawili. Hakukuwa na tatizo lolote lile, kusubiri kwao kilikuwa kitu cha kawaida sana na kitu muhimu walichokuwa wakikitaka ni kuona wakifanikiwa katika lile walilokuwa wamelipanga.

Ilipofika saa kumi jioni, Kareem akarudi hospitalini hapo. Bado hakuonekana kuwa na furaha hata kidogo, kichwa chake kilikuwa na mawazo mno, hakujua kama mpenzi wake alikuwa amerudiwa na fahamu au la.

Alipofika sehemu aliyotakiwa kusubiri, akatulia kwenye kiti huku kukiwa na daktari mmoja ambaye hakuwa akimuelewa kabisa, mara atembee kwenda kule, mara atembee kwenda huku, alimtia hofu lakini aliamua kupuuzia kwa kuhisi kwamba kweli alikuwa daktari.

Majamaa wawili wakaondoka na kwenda katika ofisi ya daktari mkuu! Walipofika huko, wakazungumza naye kidogo, kiamani lakini baada ya dakika kadhaa wakamuweka chini ya ulinzi kwa kumwambia kwamba hakutakiwa kufanya kitu chochote kile.

“Tulia kwanza,” alisema jamaa mmoja huku akiwa amemnyooshea bastola.
“Jamani! Nimefanya nini?”
“Nimesema tulia. Tunataka utusaidie jambo moja.”
“Jambo gani? Nipo tayari kufanya lolote lile ila msiniue. Nina familia na watoto wawili wananitegemea,” alisema daktari huyo huku akitetemeka, alionekana kuwa na hofu kubwa, kijasho chembamba kikaanza kuumtoka.

Wakamwambia kile alichotakiwa kuwafanyia kuwa walitaka kwenda kwenye chumba kile na kumtoa Saida na kuondoka naye kuelekea nje pasipo kugundulika. Hilo halikuwa tatizo, wakakubaliana naye kwani kwake, maisha yake yalikuwa muhimu kuliko mtu yeyote yule.

Wakamchukua na kuondoka naye. Walimwambia kwamba hakutakiwa kufanya jambo lolote lile kwani vinginevyo wangemuua, akatulia tuli. Wakamchukua na kuondoka naye mpaka katika chumba kile, walipofika katika chumba kile, wakaingia ndani.

Kareem aliyekuwa hafahamu chochote alibaki pale nje, alichojua ni kwamba wote walikuwa madaktari. Baada ya dakika mbili, wakatoka huku wakisukuma kitanda alichokuwa amelala Saida.

“Kuna nini?” aliuliza Kareem.
“Na wewe twende huku!” alisema jamaa mmoja.
“Hali yake imekuwa mbaya?”
“Ndiyo! Tunamuhamisha hospitali na kumpeleka Hindu Mandal,” alijibu jamaa mwingine.

Wakaondoka na Kareem ambaye hakuwa akijua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea. Manesi na madaktari wengine hawakuonekana kuwa na hofu yoyote ile, waliamini kwamba wale walikuwa madaktari wa kweli kwani mbali na mavazi walikuwa na daktari wao mkuu.

Walipofika nje, Saida akapakizwa ndani ya gari, Kareem naye akaingia, hawakumuacha daktari, walihitaji kuwa salama zaidi hivyo wakaondoka naye. Mpaka wanafika karibu na Soko la Al Khalif Kareem hakujua lengo la watu hao lilikuwa nini, hakujua kama watu hao hawakuwa madaktari kama walivyokuwa wakionekana.

Baada ya dakika thelathini, Kareem alionekana kuhisi jambo, haikuwa kawaida kwa gari kutembea umbali mrefu tena kwa muda huo pasipo kufika kule walipokuwa wakielekea. 

Alishangaa, akaanza kuhisi jambo kwamba kulikuwa na kitu.
Alipouliza, hakujibiwa zaidi ya kuambiwa abaki kimya, alipotaka kuuliza zaidi, mwanaume mmoja akatoa bastola na kumuweka chini ya ulinzi. Alishangaa, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea mahali hapo, alitamani kuuliza lakini alishindwa kufanya hivyo kwa sababu tu alikuwa amechanganyikiwa.

Baadaye, daktari wakamshusha huku wakimchukulia simu yake na wao kuondoka kwa mwendo mkali. Hakujua mahali walipoelekea. Njiani, Kareem akahisi kwamba watu hao walikuwa hatari sana, alijua kwamba kila kitu kilikuwa kimekwisha kumbe ndiyo kwanza kilikuwa kimeanza.

Saida hakuwa ameamka, alikuwa kimya kitandani pale, hakujua kitu kilichokuwa kikiendelea. Kareem alikuwa akilia, hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kutoka katika mikono ya watu hao walioonekana kuwa hatari ambao hawakutaka kusikia kitu chochote kile zaidi ya kuitoa roho yake na mpenzi wake.

Wakafika katika mapango ya Djara ikiwa ni saa kumi na mbili jioni. Ilikuwa ni sehemu iliyotisha mno ambapo kulikuwa na wadudu wengi wakiwemo ng’e. Kareem aliogopa, aliwahi kusikia kuhusu mapango hayo, hayakuwa sehemu salama, watu waliuawa huko na kama kulikuwa na watu walionusurika, basi hali zao zilikuwa mbaya.

“Huku ndipo kutakuwa kwenu,” alisema mwanaume mmoja huku akiwashusha kutoka garini. Hapohapo Saida akarudiwa na fahamu.

Hakujua alikuwa wapi, aliyafumbua macho yake, kulikuwa na mwanga hafifu, hakujua alikuwa mahali gani, aliwaona watu wakiwa wamvalia makoti makubwa ya kidaktari. Wakati akiangalia huku na kule, akamuona Kareem.

“Kareeem,” aliita kwa sauti ndogo. Kareem alipoisikia, harakaharaka akakimbia kuelekea kule alipokuwa Saida.
“Saida mpenzi...Saida mpenzi...” aliita Kareem huku akiwa amemfikia, palepale akaanza kumwagia mabusu mfululizo mashavuni mwake.
“Tupo wapi? Mbona giza? Nini kinaendelea?” aliuliza Saida huku akimwangalia mpenzi wake.
“Saida...ni matatizo!” alijibu Kareem.
“Matatizo? Matatizo gani?” aliuliza Saida lakini hata kabla Kareem hajajibu, mwanaume mmoja akatokea na kumtaka anyamaze vinginevyo angempiga risasi kadhaa kifuani. Saida akanyamaza. Mbele yake akakiona kifo na hakujua humo alifikaje.

Je, nini kitaendelea? Usikose Sehemu ijayo.


++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top