Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 19
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 19 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA....!!!! “Wazo zuri sana, ileteni China,” alisema kiongozi wa ...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 19
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 19
ILIPOISHIA....!!!!
“Wazo zuri sana, ileteni China,” alisema kiongozi wa China baada ya kukubaliana na Urusi vifaa vya ndege hiyo kuelekea China. Ilitakiwa kutumwa na wataalamu kumi na mbili ambao walifika Oman kwa ajili ya kuipekua ndege hiyo.

ENDELEA NAYO SASA...
Jeshi la Marekani lilichanganyikiwa, kilichokuwa kimetokea nchini Oman hakikutakiwa kuachwa, walijua kwamba walikuwa kwenye ugomvi mkubwa na Urusi na China hivyo kama kweli mawasiliano yalifanyika na wataalamu wa kijeshi wa China na Urusi walitakiwa kufika nchini Oman, walitakiwa kufanya jambo.

Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kufuatilia kwa ukaribu juu ya wataalamu hao ambao walitaka kusafiri na kuelekea China, ilikuwa ni lazima wapande ndege, hawakutaka kukubali, walitaka kufanya kila liwezekanalo mpaka kujua ndege ambayo wangepanda kuelekea nchini humo.

Ufuatiliaji wao ulikuwa mkubwa, walitaka kufuatilia pasipo shirika lolote la ndege kufahamu, haikuwa kazi ngumu kwao, maofisa wa CIA walikuwa kila kona duniani hivyo walifuatilia na kugundua kwamba watu hao walitakiwa kupanda ndege ya Shirika la Ndege la Qatar kuelekea huko China.

“Namba ya ndege?” alisema mkuu wa majeshi kutoka Pentagon.
“A590-750 A7-EDR,” alisikika mwanaume kwenye simu.
“Sawa.”

Kilichofanyika ni kuwasiliana na watu wa kampuni ya kutengeneza injini za ndege ambacho kilikuwa nchini Marekani. Kwa kipindi hicho mpaka sasa, injini za ndege zote kubwa duniani (Boeing), injini zake zilikuwa zikitengenezwa nchini Marekani katika Jiji la Dallas.

Huko ndipo ambapo mataifa mengi duniani yalipokuwa yakinunua injini na kuziweka katika ndege zao kubwa. 

Alichokuwa akikifanya Marekani ni kuweka vitu vyake katika injini hiyo na kama kulikuwa na kitu wanataka kufanya kisiri, ilikuwa ni kuziongoza ndege hizo walivyotaka wao.

Namba ya ndege ikapelekwa kiwandani, baada ya dakika mbili, majibu yakatoka aina ya injini iliyokuwa ikitumika katika ndege hiyo. Walipopewa jina la injini, wakaingia kwenye mitambo yao kwa ajili ya kuiongoza ndege hiyo walivyotaka. 

Ndani, marubani wasingekuwa na uwezo wowote ule, wao ndiyo wangeamua kuipeleka ndege sehemu yoyote ile duniani.
“Nimeipata hapa...”
“Ndiyo yenyewe?”
“Ndiyo! Inatarajiwa kuondoka saa sita mchana kutoka Oman, itapitia Syria, China, Dubai na kisha kutua Misri,” alisema jamaa wa kitengo cha IT.
“Fanyeni kama mlivyofanya ndege ya Malaysia, ndege ipotee, isionekane katika rada yoyote duniani....” alisema mkuu wa majeshi.
“Hakuna shida mkuu!”

Wanajeshi walikuwa nchini Marekani lakini wao ndiyo waliokuwa wakiiongoza ndege hiyo mara baada ya kupaa. 

Marubani hawakuwa na kazi, walitulia huku wakishangaa tu, walitamani kuishusha ndege hiyo lakini hawakuweza hata kidogo.

Ndege ilikuwa angani, wakati hayo yote yakitokea, Wamarekani haohao wakaanza kuziingilia rada za nchi nyingine, hawakutaka kuona ndege hiyo ikijulikana ilipokuwa, ilikuwa ikisafirishwa kuelekea katika Bara la Antaktika ambalo hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akiishi huko.

Wakati ndege hiyo ikielekea huko, wanajeshi wa Kimarekani walikuwa wamekwishaondoka kuelekea huko. Ilikuwa ni lazima ndege hiyo itue huko ambapo kulikuwa na kambi yao ya siri ya kijeshi ambayo ilihusika katika mambo mbalimbali ya kinyemera na hawakutaka dunia itambue kama walikuwa na kambi huko.

Ndege hiyohiyo ambayo ilianza kuongozwa huko ndiyo waliyokuwepo wale wataalamu wa kijeshi wa Kichina na Urusi, ndiyo ndege hiyohiyo ambayo ilibeba vifaa vya ndege ile iliyotunguliwa na ISIS, mbali na hao, ndiyo ndege hiyohiyo ambayo ilimbeba Bwana Abdulaziz na wale vijana wa Mzee Faraq.

Abiria wote walikuwa wakishangaa, hawakujua ni kitu gani kilitokea mpaka ndege hiyo kusafiri umbali mrefu pasipo kutua. Baada ya saa thelathini, kila mmoja akaanza kumuuliza mwenzake, hakukuwa na aliyejua kitu chochote kile, walishangaa kwani haikuwa kawaida hata kidogo.

Ndege ilitua katika uwanja mmoja huko Antaktika, abiria wakachungulia madirishani, hawakuelewa walipokuwa, walichokiona kilikuwa ni barafu tu sehemu yote, hakukuwa na jengo lolote zaidi ya mahema kadhaa magumu yaliyokuwa huko pamoja na ndege za kijeshi.

Mara baada ya ndege hiyo kusimama, harakaharaka mlango ukafunguliwa na wanajeshi kuingia humo. Hawakutaka mtu yeyote atoke, walikuwa wakiangalia huku na kule, waliwaangalia abiria waliokuwa ndani ya ndege hiyo huku wenzao wengine wakifungua sehemu ya mizigo na kuanza kuchukua vifaa vya ndege yao.

“Mkuu! Tumekamilisha. Tufanye nini na hawa abiria?” aliuliza mwanajeshi mmoja.
“Waueni wote. Hii ni siri, haitakiwi mtu yeyote kujua chochote kile. Tukiwaacha, jua dunia itajua, ili kuficha siri, ua wote halafu chukueni mabawa ya ndege hiyo, pelekeni katika Visiwa vya Tasmania na Comoro kwa ajili ya kuichanganya dunia, yaani kama tulivyofanya kwenye ndege ya Malaysia. Nimeeleweka?” alisema kamanda mkuu wa jeshi la Marekani.
“Ndiyo mkuu!”
“Sawa.”

Kilichofanyika ni kufanya kama walivyoambiwa. Abiria wote wakauawa na wanajeshi kuvunja barafu lililogandisha bahari moja huko na kisha kuizamisha ndege hiyo huku wakiwa wametoa mabawa yake.

**********************************
Dunia ilishangaa, kila mtu alipigwa na butwaa mara baada ya kusambaa taarifa zilizosema kwamba Ndege ya Shirika la Ndege la Qatar lenye namba A590-750 A7-EDR ilikuwa imepotea.

Hakukuwa na aliyeamini, mbali na ndege ya Malaysia ambayo ilipotea miezi kadhaa iliyopita, leo kulikuwa na ndege nyingine iliyopotea huku ikiwa na abiria zaidi ya mia sita. 

Hawakujua ni kitu gani kilitokea, hakukuwa na mtu aliyejua ukweli wowote ule. Watu waliokuwa na ndugu zao ambao walikuwa wanasafiri ndani ya ndege hiyo wakaanza kujaa uwanja wa ndege, walitaka kujua ni kitu gani kilitokea, kwa nini ndege ipotee, tena ikiwa ni nyingine baada ya ile ya Malaysia.

Hilo ndilo lilikuwa gumzo kubwa duniani, kila kona, stori zilikuwa ni za kuhusu ndege hiyo. Hakukuwa na mtu ambaye alijua kile kilichokuwa kimetokea, hawakujua kama Marekani ndiyo iliyokuwa imehusika katika upotevu wa ndege ile.

Ili kuipiga upofu dunia, Marekani ikatuma wachunguzi wake kwa ajili ya kuchunguza mahali ndege hiyo ilipopotelea, kitu cha kwanza wakatembelea katika rada zote za viwanja vya ndege, kitu cha kushangaza, hakukuwa na mtu aliyejua mahali ndege hiyo ilipokuwa.

“Hata tukipata kiboksi cheusi, itatusaidia,” alisema mchunguzi mmoja.

Msiba ulitawala, hakukuwa na aliyejua mahali ndege hiyo ilipokuwa. Wiki ya kwanza ikapita, ya pili na ya tatu lakini hakukuwa na mtu yeyote aliyeufahamu ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

“Yaani hata Marekani ameshindwa kujua mahali ndege ilipo, kweli si mchezo,” alisikika jamaa mmoja.

Wakati dunia ikiendelea kushikwa na taharuki, China na Urusi walikuwa wakiendelea kuchunguza, hawakujua ni kitu gani kilitokea, ndege hiyo ilikuwa muhimu mno kwa kipindi hicho kuliko ndege yoyote ile lakini kitu cha ajabu, haikuonekana kabisa.

Wiki ikakatika, hawakupata mawasiliano yoyote na watu wao kujua mahali walipokuwa. Wakati wakijiuliza sana, wakahisi kwamba Marekani alikuwa amehusika kwani kupatikana kwa ndege hiyo na kupata vile vifaa vya ndege yao ilimaanisha kwamba nchi hiyo ingedhoofika kivita hivyo walipambana mpaka kuipoteza.

Baada ya hapo, Marekani hiyohiyo ikaanza kuichanganya dunia kwa kusema kwamba bawa moja limeonekana katika Kisiwa cha Tasmania, walikuwa na uhakika kwamba inawezekana ndege hiyo ilipotelea huko.

Dunia nzima masikio yao yakawa Tasmania, walitaka kufahamu kama wangeweza kusikia chochote kile kwani kutokana na bawa hilo kutangazwa kila siku, watu wakahisi kweli ndege hiyo ilikuwa imepotelea huko.

Baada ya mwezi mmoja, tetesi zikaibuka tena na kusema kwamba bawa jingine lilionekana katika Visiwa vya Comoro, taarifa hizo zilimchanganya kila mmoja, watu wakabaki wakiwa hawajui mahali ambapo ndege hiyo ilipokuwa.

Mmarekani hakuchoka, alichokifanya ni kutengeneza ramani ya uongo kwa kutumia satelaiti na kuiambia dunia mahali ndege hiyo ilipopitia mpaka kupotea. Kila mmoja aliwaamini, hawakujua kwamba ndege hiyo haikupotea bali ilichukuliwa na kupelekwa sehemu nyingine huku rada zao zote zikitolewa uwezo wa kuiona ndege hiyo.

******************************
Vijana wa mzee Faraq walikwishafika uwanja wa ndege kwa ajili ya kuwapokea ndugu zao ambao wangefika mahali hapo na mzee Abdulaziz. Walisimama mbele kabisa ya bango lililokuwa alikionyesha ratiba za ndege ambazo zilitarajiwa kuingia siku hiyo.

Ndege ya Qatar ambayo ilikuwa ikitoka Oman, kupitia China na kufika Misri, ilionekana kuwa kwenye ratiba kwamba ingefika saa nne asubuhi lakini kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele, ratiba ilikuwa ikibadilikabadilika, ikabadilika na kuwa saa tano, baadaye saa saba, saa tisa na mwisho wa siku kuonyesha kwamba watu wangepewa taarifa kuhusu ndege hiyo.

Hawakujua nini kiliendelea, watu wa uwanja wa ndege walikuwa wakihangaika kupata mawasiliano na ndege hiyo lakini hawakuambulia kitu chochote kile. 

Walichanganyikiwa, hawakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea huko.

Watu wengi waliokuwa wakiwasubiri ndugu zao kutoka katika ndege hiyo wakajazana uwanja wa ndege, ndege ambayo ilitakiwa kuingia saa nne asubuhi, mpaka saa kumi jioni haikuwa imeingia. 

“Nini kinaendelea?” aliuliza mwanamke mmoja, alionekana kuchanganyikiwa kwani ndani ya ndege hiyo kulikuwa na watoto wake wawili.
“Hata mimi sijui! Labda kuna tatizo!”
“Lakini si wangetuambia kuliko kukaa kimya jamani!”
“Hilo ndilo kosa. Nadhani tunatakiwa kuwa wavumilivu,” alisema jamaa mwingine.

Waliendelea kusubiri, hakukuwa na ndege hiyo, kila mmoja alichanganyikiwa, watu hao hawakutaka kutulia, walichokifanya ni kwenda kwenye ofisi za shirika la ndege hiyo, walitaka kujua ukweli juu ya kilichokuwa kimetokea.

Watu hao wakawasiliana na idara ya mawasiliano ambapo nao hawakujua ni kitu gani kilitokea mpaka ndege hiyo kutokuonekana.

“Kwa hiyo?”
“Ngoja, tutawapa majibu!”

Hakukuwa na kilichoendelea, rada zilijaribu kuitafuta ndege hiyo, kwa msaada mkubwa wa satelaiti lakini hawakufanikiwa kuiona kwani katika kipindi ambacho ndege hiyo ilipokuwa ikipelekwa Antaktiki, satalaiti zote zilifichwa na kutokugundua chochote kile.

Ndege ikapotea, hakukuwa na aliyejua mahali ilipokwenda. Vijana hao wakawasiliana na mzee Faraq na kumwambia kile kilichotokea kwamba ndege hiyo iliyotarajiwa kumleta mzee huyo, vijana wake na fedha ilipotea, mzee huyo akachanganyikiwa mno, hakuamini kilichotokea.

Je, nini kitaendelea?, Je, Saida atakufa?


++++++++++++++++++++++++++++++++++++++

++++++++++++++++++++++++++++++++++++++
KUWA KARIBU NASI LINDIYETU.COM
Usipitwe!! Ungana na Familia hii kupitia FacebookTwitter na Instagram ili kupata Infortainment zote!! Usikose kujiunga na Youtube channel yetu ili kupata Exclusive mbalimbali kali kutoka LindiYetu TV

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top