DK MWAKYEMBE AWATANGAZIA VITA WATUMISHI WASIO WAADILIFU

Waziri wa Katiba na Sheria Dr.Harrison Mwakyembe ametangaza vita dhidi ya watumishi wasiokuwa na maadili wa idara ya mahakama, wakiwemo mahakimu ambao wamekuwa wakituhumiwa kwa rushwa kuwa wajiandae kuondoka wenyewe kabla hatua dhidi yao hazijachukuliwa.
Dr.Mwakyembe
Dr.Mwakyembe ametoa onyo hilo wakati alipofanya ziara za ghafla katika mahakama za mwanzo ya Ukonga, Buguruni na Ilala kufuatia malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu ucheleweshwaji wa mashauri, rushwa na upotevu wa majalada ya kesi.

Amesema Serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kupambana na rushwa na watumishi wa Umma wasiokuwa waadilifu katika nyanja zote ikiwemo ya mahakama na kuwataka wananchi kutoa Ushirikiano katika kuwafichua huku pia akifungua milango kwa wananchi hao kwenda ofisini kwake kuwasilisha malalamiko ili aweze kuchukua hatua stahiki.

Aidha Dr.Mwakyembe amesikitishwa na hali ya miundombinu ya mahakama hizo ikiwemo ubovu wa majengo ya mahakama hizo, ukosefu wa vyoo safi na salama, maeneo ya kuhifadhia majalada ya kesi na kuahidi kuyashughulikia mara moja.

Baadhi ya mahakimu waliokutwa katika mahakama hizo wameelezea changamoto mbali mbali ikiwemo uwepo wa kesi nyingi huku mahakama hizo zikikabiliwa na uchahe wa mahakimu.

Baadhi ya wananchi walitoa malalamiko mbele ya waziri ikiwemo mazingira ya rushwa na ucheleweshwaji wa kesi zao.
Previous Post Next Post