MSHALE WA MLIMA ILULU::.IKULU HAKUNA BIASHARA..

Na.Ahmad Mmow.
Salam wapendwa wananchi wenzangu. Poleni wote ambao mpo hospitali na sasa mnashindwa kufuatilia kikamilifu mchakato wa maandalizi ya uchaguzi mkuu. Mimi naungana na wote wanaokuombeeni mpone haraka. Poleni wengine msiyo na amani kutokana na matatizo mbalimbali ya maisha. Jipeni moyo kuweni watulivu na imani kuu. Bila shaka yatakwisha, wala msikate tamaa. Kwani hakuna marefu yasiyo na ncha. Mnao amini uwepo wa MUNGU kupitia imani zenu, mtangulizeni yeye. Kwani yeye ni kila kitu. Na wale wasioamini uwepo wake basi tangulizeni mbele kile mnacho amini ni msaada kwenu. Bali kwa njia zilizosalama na halali.
Ikulu
Tupo pamoja na tutaendelea kuwa pamoja. Kwenu mliowazima na wenye afya njema basi natuendelee kuzungumza na kujadiliana kwa maslahi mapana ya taifa. Huu ndio wakati wenyewe, tusiogope kuzungumza. Lakini mazungumzo na mijadala yetu ilenge katika kujenga na siyo kubomoa mshikamano wetu. Nchi yetu ipo katika kipindi cha kuwatafuta madereva watakao endesha vyombo vyetu. Urais, ubunge na udiwani. Nimuhimu tutambue kuwa kazi iliyopo ni ngumu, Na sisi ndio wenye jukumu la kuwachagua madereva watakao endesha vyombo hivyo kwa umakini na ufanisi mkubwa ili watufikishe kule tunakohitaji kufika. Kazi hii ni yetu wote, tusaidiane kuwapima na kuwachambua waliojitokeza na watakao jitokeza kutaka kuomba kazi hiyo.
Tukiwa wavivu wa kuchagua, itakula kwetu. Leo ninatumia muda wangu kuwakumbusha umuhimu wa kushiriki kikamilifu mchakato huu. Hasa katika kuwapata aina ya madereva wanaofaa kuendesha vyombo hivyo. Kwani miongoni mwa makosa makubwa tunayofanya kila kipindi cha uchaguzi ni kujitega katika hatua za hizi muhimu. Hasa katika kuwatambua hao wanaotaka watuongoze. Hatuwafuatilii na kujishugulisha kutafuta rekodi zao. Badala yake tumekuwa tukiwaacha watu wachache watuoneshe nani" mnaulizana makabila, mnataka kutambika? Karne ya ishirini na moja mnatuingiza kwenye basi la ukabila! Hayo ni baadhi ya maneno yaliyo kwenye hotuba moja, hata tunaojaribu kufuatilia mchakato tunaendeshwa na watu wachache na kuwa mashabiki wa wanaotangaza nia. Tunawashabikia bila kuzijua rekodi zao na mambo yao kwa undani. 
Uvivu! Ukiwauliza wanaoshabikia nikwanini wanawashabikia wanaowashabikia huwezi kupata sababu za msingi. Wengi wao wanawashabikia wanaonesha matumizi makubwa ya fedha kwakufanya mbwembwe na manjonjo wakati wakutangazania. Wale wachache ambao wapo kwenye timu za watangazania wanapita huku na kule kuongeza idadi ya mashabiki kutokana na kile walichokipata au wanachotarajia kupata kwa watangaza nia wanaowaunga mkono. Tunaingia kichwa kichwa. Hivi inaingia akilini mtu akushawishi muunge mkono mtangazania fulani kwakuwa nitajiri? Na kwamba kwakuwa nitajiri akiingia ikulu hataiba. Ebo! nani aliyewaambia mafukara ndio wezi na matajiri ni wasafi! Kimsingi tabia ya mtu haitokani na hali. Mtu anaweza kuwatajiri asiwe mwizi, kadhalika mtu anaweza kuwafukara asiwe mwizi. Tajiri anaweza kuiba, nafukara anaweza kuiba. Hali za wote hao (utajiri na umaskini) hasababishi mtu awe msafi au mchafu.
Ndipo tunapotakiwa kuwafuatilia ili kupata taarifa zao kwakina. Ili tuweze kufahamu huo utajiri aliupataje. Njia zilizotumika ni halali au haramu? Je njia iliyotumika haikuwa na haitakuwa na madhara kwetu. Na yule anayejiita fukara ni fukara kweli, naufukara wake umetokana na nini, utakuwa na madhara gani kwetu tukimpa anachokitaka? Hayati baba wa taifa, mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutueleza kuwa Ikulu hakuna biashara.
Yeye alifanyakazi katika ofisi hiyo kwa miaka 23, hakuwahi kuiona biashara. Lakini utadhani tumerogwa, tunayasahau maelezo hayo. Tumeanza kuwapima watangazania kwa vigezo na sifa za ufukara na utajiri. Niwaombe basi tutumie sifa hizo kama kichocheo cha kuzitafuta sababu za sifa hizo kwa wahusika. Tujue tajiri huyo atakuwa na uzalendo kiasi gani pindi akienda ikulu. Tujue fukara huyo hakuwa na uzalendo gani akienda Ikulu. Lakini baada ya kuzipata na kuzijua taarifa zao za kina zilizosababisha hali walizonazo. Ebu tuwekane sawa hapa Ingawa mwalimu aliishi na kufanyia kazi Ikulu ya Magogoni, lakini maana pana zaidi nikwamba ikulu ni ofisi za umma hususani serikali katika ngazi zote za utawala. Kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa. Kwahiyo katika makala haya sijawalenga watangazania wa nafasi ya urais pekee. Bali watu wote wanaotaka kuomba nafasi zitakazo kugombewa katika uchaguzi mkuu ujao.
Tuache uvivu katika kuwafuatilia, ili tuepuke kununua mbuzi walio ndani ya magunia. Tutafakari na tuchue hatua. 
MUNGU IBARIKI TANZANIA. 0757-115973/ 0717-924695.
Previous Post Next Post