Na.Abdulaziz Ahmeid. Kilwa.
Wakuu wa idara katika halmashauri ya wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, wametakiwa kuiga utendaji wa idara ya elimu ya halmashauri hiyo ili kuwa na matokeo mazuri katika idara zao. Hayo yalielezwa jana katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo kilichofanyika Kilwa masoko.
Madiwani hao ambao pamoja na mambo mengine walikosoa utendaji wa baadhi ya idara za halmashauri hiyo. Walisema baadhi watendaji hasa wakuu wa idara nyingine za halmashauri hiyo hawana budi kujifunza na kuiga juhudi za mkuu wa idara ya elimu ya msingi ambaye ameonesha juhudi kubwa katika usimamizi na utendaji katika idara yake, huku wakiwa na matumaini juhudi za mkuu wa idara hiyo zinaweza kutoa matokeo mazuri ya ufaulu kwa wanafunzi. Haji Mulike, diwani wakata ya Kikole(CCM) aliyeungwa mkono na madiwani wenzake ndani ya ukumbi huo. Alisema ingawa katika baadhi ya idara kuna utendaji usioridhisha na kusababisha malalamiko. Lakini wanatambua juhudi zinazofanywa na mkuu wa idara ya elimu, ambaye matokeo ya juhudi zake yataanza kuonekana.
Hivyo wakuu wa idara wengine ambao idara zao zinalalamikiwa mara kwa mara waige na kujifunza kutoka kwa mwenzao. "Lazima tuwe wa kweli kabisa, kwamba tukiwa na wakuu wa idara kama huyu wa elimu ya msingi tunauhakika halmashauri yetu itasonga mbele na kuwa na madiliko makubwa" mkuu huyu wa idara anajituma kiasi cha kushika chaki mwenyewe na kuingia darasani kufundisha, mkiwa na wakuu wa idara kama huyu mtashindwaje kupata mafanikio", alihoji Mulike.
Jafari Arobaini, diwani wa kata ya Kivinje (CUF) pamoja na kupongeza utendaji wa idara hiyo alitoa rai kwa madiwani wenzake kuangalia uwezekano wa kutoa zawadi kwa wakuu wa idara ambao idara zao zinafanya vizuri. Alisema halitakuwa jambo baya kwa wakuu wa idara ambao jitihada zao zinaonekana kama watapewa zawadi au tuzo ili kutambua mchango wao na kuwahamasisha wengine wafanye kazi kwa bidii. Katika hatua nyingine, idara ya afya katika halmashauri hiyo imeyafunga maduka saba ya madawa ya binadamu kutokana na kukiuka masharti mbalimbali ya kisheria.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, Dkt Peter Msanya. Alilieleza baraza la hilo kwamba kufungwa kwa maduka hayo ni matokeo ya ukaguzi ulioanza wiki iliyopita na ambao unaendelea. Masanya alisema katika msako na ukaguzi huo wamebaini ukiukwaji mkubwa wa sheria katika uendeshaji wa maduka hayo. Ikiwamo kuuzwa madawa yalikwisha muda wa matumizi yake, baadhi ya wauzaji kutokuwa na taaluma na madawa yasiyositahili kuuzwa kwenye maduka hayo. Ikiwamo kuwalaza wagonjwa na kuwaongezea maji mwilini, kuwachoma sindano.
Maelezo ya daktari huyo yalikuwa nimajibu ya swali la diwani wa kata ya Lihimalyao, Mahadhi Nangona (CUF) aliyetaka kujua sababu za kufungwa maduka hayo.