Na Ahmad Mmow.
"Mnaulizana makabila, mnataka kutambika? Karne ya ishirini na moja mnatuingiza kwenye basi la ukabila!" Hayo nibaadhi ya maneno yaliyo kwenye hotuba moja wapo za baba wa taifa, hayati mwalimu Julius Nyerere. Nimiongoni mwa hotuba za nguli huyo wa siasa za Tanzania, Afrika na duniani. Baba wa uhuru wa mataifa mengi ya Afrika. Aliyechukia ubaguzi, rushwa, uonevu na ukabila kwa vitendo. Hakika hotuba za baba wataifa zinaendelea kuwa lulu kwa watu makini.
"Mnaulizana makabila, mnataka kutambika? Karne ya ishirini na moja mnatuingiza kwenye basi la ukabila!" Hayo nibaadhi ya maneno yaliyo kwenye hotuba moja wapo za baba wa taifa, hayati mwalimu Julius Nyerere. Nimiongoni mwa hotuba za nguli huyo wa siasa za Tanzania, Afrika na duniani. Baba wa uhuru wa mataifa mengi ya Afrika. Aliyechukia ubaguzi, rushwa, uonevu na ukabila kwa vitendo. Hakika hotuba za baba wataifa zinaendelea kuwa lulu kwa watu makini.

Maneno niliyo yanukuu hapo juu, ni kipimo tosha kinachoonesha alivyokuwa anayachukia mambo hayo kwa nguvu zote. Maneno hayo yananikumbusha wimbo mmoja wa taarabu, unaosema ubaya hauna kwao tena hauna kabila.Wimbo ambao mwimbaji wala jina la kundi silikumbuki. Labda wasomaji mtanisaidia na msisite kunieleza ni nani aliimba na wakundi gani.
Nimeanza kunukuu maneno ya baba wataifa na ya wimbo wa taarabu baada ya kubaini tumeanza kuyashabikia mambo hayo kuelekea uchaguzi mkuu. Kama kuna mtu anabisha kwamba hayo hayaanza kuchomoza, namshauri ajichanganye huku vijiweni ambako wengine tumekulia na tunataka kuzeekea.
Yameanza kuzungumzwa. Kadri siku zinavyochanja mbuga kuelekea uchaguzi mkuu ndivyo hayo yanavyoshika kasi. Tumeanza kuwapima watangazania kwa kuangalia wanatoka mikoa, kanda, kabila na dini gani.

Nihatari, ni hatari kwasababu tumeanza kuingia kwenye vyombo vya usafiri ambavyo havitatufikisha salama tunakokusudia kufika. Kupitia hayo baadhi wameanza kuzimilikisha kabila baadhi ya tabia kuwa ni mali yake. Hasa tabia chafu. Kupitia hayo baadhi wameanza kuzihukumu kanda na mikoa kwamba urais wa mwaka huu ni zamu yao. Tena wengine wanasema urais wa mwaka huu ni zamu ya dini yao. Jamani mambo hayo yanatoka wapi! Kuacha kumchagua mtu eti kwa sababu anatoka kwenye kabila lililomilikishwa tabia ya udokozi na wizi ni hatari. Wenye mawazo hayo yawapasa kufikiri mara mbilimbili wakati wakijiuliza yafuatayo.
Wezi na vidokozi wanaosumbua katika eneo na mahali wanapoishi ni watu wanaotoka kwenye kabila hiyo waliyoimilikisha tabia ya udokozi na wizi? Mafisadi waliopo serikalini wanaopigiwa kelele kila uchao wanatoka kabila hiyo? wamechanganyika tu. Wanaosema makabila fulani hayafai kupewa wadhifa huo kwasababu ni makubwa au madogo. Nao wajiulize kama ni kosa kuwa wengi au wachache?.
Wale wanaosema hii ni zamu yao nao pia wajiulize kama tunautaratibu wa kuongoza kwa zamu ili kumpata anayefaa kwa nafasi hiyo kupitia vigezo na sifa za kipuuzi, za dini, ukabila, ukanda na mikoa. Mimi sidhani kama tunautaratibu huo. Bali ujuha tu. Kutoka kabila dogo au kubwa sio sifa na vigezo vya msingi vya rais tunayemtaka. Awe anatoka kabila kubwa, dogo, na hata akitoka kwenye kabila linalokula mbwa, panya, samaki, senene na hata wavaa ndonya, wacheza likomanga, msolopa hata litungu apewe. Alimoradi akidhi vigezo vya msingi kwa maslahi mapana ya taifa.

Iwapo aina ya rais tunayemtaka anapatikana kutoka kanda, mkoa, au kabila ambayo imewahi kumtoa rais na apewe. Kwani hatuna utaratibu wa zamu, nikwasababu tukiwa na utaratibu wa zamu kuna hatari siku moja tunaweza kuwa na rais chizi alimoradi wakati huo ni wa zamu ya kabila, kanda, dini na mkoa anaotoka.
Tusithubutu mchezo huo. Inasikitisha kusikia hata baadhi ya wanaotangaza nia wameanza kucheza ngoma hiyo ya kipumbavu kwa kujinadi chini chini kwa kutumia sifa na vigezo vya kijinga vinavyoweza kulipasua na kuligawa taifa letu na kusababisha kusambaratisha umoja na mshikamano wetu. Haiwezekani fisadi alazimishe kupewa nchi kwa sababu anatoka kanda fulani ambayo haijawahi kutoa rais, haiwezekani mtu safi aogope kuomba eti kwa sababu anatoka kanda au mkoa ambao umewahi kutoa rais. Haiwezeni mwizi alazimishe kupewa urais eti kwavile anatoka kabila kubwa au dogo.
Lazima tuyakatae mawazo hayo ya kijinga na kuwakataa wanaotaka kutupandisha kwenye mabasi ya ukabila, udini. ukanda, mikoa na hata rangi ya mtu. Nilazima tuyapige vita hayo kwa nguvu zote. Nakila mwenye kufanya hivyo atakuwa amedhihirisha kwa vitendo kwamba analitakia mema taifa letu.
Lazima tuyakatae mawazo hayo ya kijinga na kuwakataa wanaotaka kutupandisha kwenye mabasi ya ukabila, udini. ukanda, mikoa na hata rangi ya mtu. Nilazima tuyapige vita hayo kwa nguvu zote. Nakila mwenye kufanya hivyo atakuwa amedhihirisha kwa vitendo kwamba analitakia mema taifa letu.
Nakila mwenye kulitakia mema taifa anakuwa ni miongoni mwa wazalendo. Je,wewe hupendi na hutaki kuwa miongoni mwa wazalendo? Kumbuka kuwa WEMA NA UBAYA HAVINA KWAO WALA KABILA.
Ahmad Mmow
0757-115973/ 0717924695.
Tags
MAKALA