MSHALE WA MLIMA ILULU :: MAWAZIRI MNAOTAKA RIDHAA YA CCM KUGOMBEA URAIS,ACHENI"USANII" TUTENDEENI HAKI.

Na.Ahmad Mmow, Lindi
Nishiiida! wanachuana, wanarushiana vijembe wanakataana kama hawajuani na hawafanyi kazi kwenye serikali moja. Kaaazi kwelikweli! Kuanzia makamo wa rais, waziri mkuu, mawaziri wakubwa na wadogo wote wanakitaka kiti.
Tobaa! hakuna kujuana wala kuheshimiana sasa. Kila mtu anatangaza kivyake na mtindo wake.
Barabarani, uani, sebuleni, kwenyekumbi, barazani na viwanjani. Twende kazi mwaka huu! Nianze kuwauliza swali dogo tu mliopo kwenye baraza la mawaziri kwa nyazifa zenu au hata mliopo serikalini ikiwamo mawaziri wadogo ingawa wengine hawapendi kuitwa hivyo, wanataka waitwe manaibu waziri tu. Kwangu mimi naona yote sawa.
Kama buku(1000) kuichenji na kupata jelojelo(500) mbili, yaleyale tu. Kwani demokrasia wakati wa uchaguzi, hasa mwaka ambao rais anaetokana na CCM anatimiza vipindi viwili inageuka nakuwafujo? Kuanzia makamo hadi mawaziri wadogo kutaka urais maana yake nini kama siyofujo? Hata kama mtajitetea lakini hakuna maana nyingine zaidi ya fujo zinazosababishwa na tamaa tu.
Januari makamba
Januari Makamba, Mtangaza nia ya Urais kupitia CCM 2015

Ebu tutulize akili zetu kidogo tu, nakufikiri. Hivi hao wote hawamjui mwenzao mwenye uwezo na anayesitahili kuvaa kiatu hicho? Jamani hata kama mkisikia darasa lina wanafunzi wenye uwezo mkubwa kiakili, na hata darasa lenye sifa ya wanafunzi mbumbumbu lakini madarasa hayo lazima yatakuwa na wa kwanza na wa mwisho. Nashindwa kabisa kuelewa kwa jamaa hawa ambao wote wamo ndani ya serikali wakimsaidia Rais, lakini hawajuani na hawamjui mwenye uwezo kuwazidi, nidarasa la ajabu kweli.
Tuache hayo nisije nikawachosha na kusababisha mshindwe kuvielewa vipaumbele vya marais wetu watarajiwa. Wengine mmeanza kuwapokea wanao tafuta wadhamini. Hoja yangu ya leo ninamna baadhi watangazania wanavyojaribu kwa nguvu zote kujitoa serikalini wakiwa wangali ndani ya serikali hiyo hiyo. Tunatambua kwamba maamuzi mengi kama siyo yote ya serikali yanafanywa na baraza la mawaziri. Ndicho kikao cha siri kikubwa kabisa. Ndiyo sababu wanapoapishwa kuwa mawaziri, wana apa kwamba watakuwa waaminifu na hawatatoa siri za baraza hilo. Hata hivyo haohao wanapo tangazania wanalalamikia na kulalamika yaleyale ambayo yanalalamikiwa na watu walio nje ya serikali, ikiwamo vyama vya siasa vya upinzani.
Mimi naona kama kitendo hicho nisawa na kumkimbia Rais kiaina na kumuachia lawama hizo azibebe peke yake. Bora basi wangenyamaza badala ya wao nao kulalamika na kuhaidi wakipewa nafasi hiyo watakomesha, watashugulikia na watayaondoa. Wanaosema wataendeleza mema na juhudi zilizofanyika ni wachache sana. Hata wengine ambao sasa wapo nje ya serikali lakini walikuwepo, nao wanasema tatizo la serikali iliyopo haifanyi maamuzi magumu.
Serikali iliyopo inaongozwa na rais, kwanamna yoyote ile
kama serikali inashindwa kufanya maamuzi maana yake anaye iongoza ndiye anayeshindwa. Wanaungana na walioserikalini kumshambulia! Mlikuwepo katika serikali hiyo hiyo mbona hayo maamuzi magumu hamkuyafanya! Au rais aliwazuia msiyafanye namkaamua kujiuzulu? Mbona hamkusema kama mnajiuzulu kwasababu rais hashauriki? Mnamuonea, kumbe ndivyo mlivyo! Ninyi mliondani ya baraza la mawaziri hayo mnayolaumu na mnayohaidi kuyafanya mkichaguliwa mnakataliwa na kuzuiwa na Rais msiyafanye? nakama nikweli aliwazuia na labda anaendelea kuwazuia na hataki kupokea ushauri wenu mbona hamjiuzulu? Uzalendo wenu upowapi na tunawezaje kuwa amini nyinyi! Inawezekana hamkumshauri mlitegea mwaka huu mfanye mtaji wa kuingilia ikulu.
Razalo Nyalandu
Razalo Nyalandu, Mtangaza nia ya Urais kupitia CCM 2015

Kama ndiyo hivyo basi hamkumkomoa rais bali sisi wananchi ndio mliotutesa kutokana na matatizo mliyoyaweka kama akiba ya kuingilia ikulu. Watanzania wenzangu tuwatazame kwa jicho la ziada watu hawa. Tena tukiwatazama tusigeuke haraka. Haipendezi hata kidogo ionekane kila jambo halikufanyika vizuri. Nanyinyi ndio mnamadawa ya kutibu yote hayo. Aliyesababisha ninani hasa! leo tunataka tumjue adui yetu. Mnalalamika na kuja na mikakati lakini hamtuambii aliyetufikisha hapa tulipofika. 
Hapana jamani! ebu tuambieni adui yetu. Kama hamtuambii basi nanyinyi mmeshiriki kutufikisha hapa. Mwanzo nilidhani tabia ya kulaumu serikali ingeishia kwa mzee Kinana na mtani wangu Nape, msishangae kumuita Nape mtani wangu. Mimi ni mngindo na Nape ni mmakonde. Na kwakuwa ni mtani wangu ninatangaza nia ya kumsaidia apate ubunge kama atagombea popote maana akipata nitafaidika kwani mtani ana haki ya kumnyang'anya mtani wake kitu alichoshika mkononi. Wao wana sababu na wanalazimika kufanya hivyo. Na kwakweli walau juhudi zao kupitia propaganda, wamefanikiwa walau kuwarejesha na kuwazuia baadhi ya waliotaka kujitoa ndani ya chama hicho.Hongera Kinana na wasaidizi wako. Kuvuka ni kuvuka tu siyo sawa na kushindwa. Mimi wanao nichanganya hawa waliokuwepo na ambao wapo serikalini kufanya usanii. Kwa faida ya nani? Wale wanafanya ili chama kisife, wakiwa na matarajio wanaweza kukirejesha kwenye mstari na kuwapa matumaini wanachama wake na kuwerejeshea imani wale ambao wamekikatia tamaa kama baba yangu Dkt Lwaitama ambaye alishatangaza ni mwanachama mfuu wa chama hicho. Sasa hawa wanaotangazania wanafanya usanii kwa faida ya nani! Ndiyo sababu natoa wito kwenu tuwatazame kwa jicho la tatu.
Kumtwisha lawama aliyewapa ulaji, kuahidi wana madawa ya kutibu yale wanayo laumu wakati wamo, na wengine walikuwemo ndani ya serikali hiyo hiyo siyo jambo dogo. Sisemi kama ni dhambi kugombea bali fujo na ulaghai ndivyo vinanifanya niwa seme na kuwahoji ninayowahoji. Kutaka urais kwa kumtupia lawama mtu ambaye aliwaamini mtamsaidia, ni kukosa shukrani.
Sina nia wala lengo la kuwagombanisha na mheshimiwa rais. Kwani hawezi kuwachukia kwasababu mimi nimesema hayo, kwani naye amebaki kuwangalia kama ninavyowashangaa mimi. Na labda alikuwa anawaonea basi sisi tunamsaidia kuwaeleza. Ingawa tunajua baadhi yenu mlianza mikakati ya kumuangushia jumba bovu. Kwa sababu hata baadhi ya mambo ambayo baadhi yenu mlikuwa na uwezo wa kuyashugulikia kutokana na mamlaka mliyonayo, ambayo mumepewa kisheria. Lakini mlishindwa, badala yake mkawa mnatuambia mngekuwa marais mngechukua na kufanya uamuzi. 
Tumepata kusikia mtu anasema angekuwa Rais angewatimua siku ilele waliovurunda kazi. Maana yake nini! na rais asipowatimua inakuwaje? Nakama hukuwa na uwezo na mamlaka ya kuwafukuza kazi alitutangazia sisi iliiweje! Kumbe akijaandaa amkatae kama Petro alivyomkana bwana YESU mara tatu kabla jogoo kuwika.
Tumewakamata, sasa mtujibu maswali yetu kwanza ndipo tuwape urais mnaoutaka. 
MUNGU IBARIRIKI TANZANIA.
0757-115973/0717-924695.
Previous Post Next Post