MSHALE WA MLIMA ILULU:: HUJUMA YA MAWAZO YENYE MASLAHI MAPANA YA TAIFA NI UFISADI PIA

Na.Ahmad Mmow, LINDI
Wapendwa wasomaji wa maandiko yangu, awali ya yote niwape pole kwa kutonisoma kwa takribani siku nne sasa. Msiwe na hofu, mimi ni mzima wa afya. Kwa wale ambao mpo katika funga nawatakia saumu njema. Mungu awajalie nguvu na imani ili ibada yenu hiyo iwe yenye kutakabariwa. Ebu tuendelee kujadiliana kama kawaida yetu. 
Wagombea Urais CCM
Mnajua tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu. Pilikapilika zimeanza kila mahali, vyama vipo katika hekaheka za kuwapata makada wataopeperusha bendera za vyama vyao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huo. Watangazania ya wanaotaka ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi wanapishana angani na ardhini kutafuta wadhamini. Idadi ni kubwa haijapata kutokea. Ukiuliza kulikoni unaambiwa ni kukua na kupanuka kwa demokrasia ndani ya chama hicho kikongwe miongoni mwa vyama vikongwe barani Afrika.

Uongo mtupu. Hatutaondoka kwenye mjadala wa uchaguzi mkuu. Maana ndiyo habari ya mijini na vijijini kwa sasa. Bila shaka mnawasikia watangazania wanavyoparurana na kukataana. Wengine wanalalamika kuwa wanapakwa matope, ili wasikubalike. Na mwisho wa siku waondolewe kwenye uteuzi katika chama hicho ambacho balozi Augustine Mahiga akikituhumu kwa kukumbatia na kuwapitisha kwenye uteuzi watoa rushwa. Chambilecho kaka yangu Makongoro Nyerere akisema chama hicho kimetekwa na wafanyabiashara na vibaka.
Makongoro Nyerere
Ebu tuwekane sawa hapa kwanini nasema Makongoro ni kaka yangu wakati mimi ni mngindo wa Liwale, na yeye ni mzanaki wa Butiama. Makongoro kwa umri ni kaka yangu. Lakini baba yake ni baba wa taifa, kwa hiyo ni baba yetu wote. Ni kama wa kristo safi wanavyojiona kuwa ni waisraeli kwa kuunganishwa na mwanakondoo Yesu mpakwa mafuta (kristo, masiha na mfalme wa wafalme). Ukiwasikiliza watangaza nia karibu wote wanazungumzia ufisadi. Na wanaoitwa mafisadi kati ya waliotangaza nia ni wachache sana. Hawazidi wawili kama siyo mmoja. Hao wamefanywa kuwa ndiyo nembo ya ufisadi kana kwamba matatizo ya uchumi wa nchi hii yamesababishwa na wao peke yao. Mbaya zaidi ufisadi unaozungumzwa na ulioganda vichwani mwa watu ni ufisadi wa mali ya umma.

Hata wananchi wakawaida wameingia kichwa kichwa kuamini hivyo. Hali ambayo inasababisha idadi ya mafisadi wanaotangaza nia kuwa ni ndogo kama nilivyotangulia kueleza. Nimewasikia watangazania wengi wakisema watawashugulikia mafisadi pindi wakichaguliwa kuwa marais. Wakiamini na kutuaminisha ni wachache. Kwangu mimi ukweli haupo hivyo. Mimi naamini mafisadi ni wengi sana, wasiotangazania na waliotangazania. Bali kosa ni hilo la kuamini kuwa ufisadi nikupora mali za umma ikiwamo fedha za umma kwa njia tofauti. 
Ima kwa kuingia mikataba isiyo natija kwa umma, kuingiza bidhaa kwa njia za magendo. kupeana zabuni bila kufuata taratibu, kanuni na sheria. Kwangu mimi hata wanaohujumu mawazo na mapendekezo yenye maslahi ya taifa ni mafisadi pia. Wanaopambana kuminya demokrasia kwa njia za wazi na kificho ni mafisadi pia. Iwapo tutawaingiza na watu wa aina hiyo hatuwezi kuwa na idadi ndogo ya mafisadi kati ya waliotangazania kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Ebu chukulia kwa mfano Mzee Samuel Sitta ambaye amekuwa akijinadi kuwa ni msafi na kwahiyo anasitahili kupokea kijiti kutoka kwa rais Kikwete. Mzee Sitta nimiongoni mwa vinara wanaowashambulia wenzao kwa kuwaita mafisadi, amesahau kuwa yeye alikuwa ni kinara pia wa waliofisidi mawazo ya wananchi waliowengi katika mchakato wa kupata katiba mpya. Tikitaka alizofanya mzee Sitta akiwa spika wa bunge maalum la katiba ni ufisadi tosha kwa mawazo ya wananchi waliowengi. Kwa kuzingatia ukweli huo mchungu hata yeye nifisadi. Mzee Sitta alifisidi matarajio ya wengi kwakuuzima mjadala wa kampuni tata
ya kufua umeme ya Richmond. Leo anageuka nakuimba wimbo wa ufisadi uliotokana na sakata hilo. Kwakuzima mjadala ule na kupuuza mapendekezo ya tume ya Mwakyembe ni ufisadi wa hali ya juu.
Hivyo hata yeye alishiriki kuwalinda anaowashambulia sasa. Tuite nini hiki kama sio unafiki (uongo) uzalendo wake anaotambia sasa upowapi iwapo alitupa mapendekezo ambayo yangeweka ukweli hadharani kwa watuhumiwa wa sakata hilo ambao leo wanashambuliwa na kugombewa mithili ya mpira wa kona wangefikishwa mahakamani. 

Kama sio ufisadi wa demokrasia tuite nini na kama siyo unafiki mchungu kwetu iwapo jaji ambaye kwa mujibu wa sheria hakutakiwa kuwa mwanachama wa chama cha siasa anapoibuka na kutangazania ya kutaka kupitishwa na chama cha siasa kugombea urais katika kipindi kifupi tu tangu astahafu na bado akiendelea kushika uongozi katika taaluma ya sheria katika medani za kimataifa?

Niukweli usio na shaka jaji huyu alikuwa kada na mwanachama mtiifu akiwa jaji ambaye kwa mujibu wa sheria hakutakiwa kuwa mwanachama chama chochote cha siasa. Kujificha na kutudanganya kuwa hakuwa mwanachama wa chama cha siasa ilihali nimwanachama wa chama cha siasa ni ufisadi wa demokrasia. Mafisadi niwengi sana lililokubwa ni utulivu tu katika kufikiri. Tukitulia tutawa gundua na kuwapata mafisadi wengi wengi sana. Lilokukubwa ni kujua ufisadi sio wa pesa na mali tu. Mie namuona jaji huyo ni fisadi pia katika ukuaji wa demokrasia katika nchi yetu. Wote hao ni mafisadi sawa na hao wengine wanoitwa wachafu. 
Nape Mnauye
Viongozi wa CCM hasa katibu wa idara ya itikadi na uenezi, Nape Mnauye anasema chama hicho hakitakuwa tayari kumteua mtu ambaye kitahangaika kumsafisha kwa dodoki mbele ya wapiga kura. Najua hata yeye hakujua kuwa hata hao niliowataja nimafisadi pia. Ambao sisi ambao bongo zetu hazijachanganyika na uji tunawaona nimafisadi ambao hawafai kusafishwa hata kwa brashi ya chuma.

Huenda mtani wangu Nape alikuwa anadhani mafisadi ni wachache. Basi atambue sasa kuna mafisadi wengi. Mimi nimemuongeza wawili basi nijuu yake sasa kuwatafuta mafisadi wengine ambao kama atadhamiria atawapata tu. Maana hao wa sasa hata wakisafisafishwa kwa brashi ya chuma hawatatakata. Nasi kama wananchi tunawajibu wakuwatafuta na kuwatambua mafisadi wengine ili mwisho wa siku tuwakatae.
Tukutane siku nyingine.Ramadhan karim. 0757115973
Previous Post Next Post