MADIWANI WILAYA YA KILWA WAMKALIA KOONI MKURUGENZI WAO, MADAI YA POSHO NA MAKATO YAKE, KIKAO CHAVURUGIKA KWA AJILI YA VURUGU

Na. Abdulaziz, Lindi
Kikao cha baraza la madiwani katika halmashauri ya wilaya Kilwa mkoani Lindi kimeshindwa kuendelea baada ya madiwani kugomea kufanya kikao hicho kwa madai mbalimbali ikiwemo kushinikiza kulipwa posho zao zaidi ya miezi mitano.
Madiwani Kilwa
Hali hiyo ilijitokeza baada ya diwani wa kata ya Kilanjelanje Saidi Mtotela kuomba mwongozo kwa makamu mwenyekiti ambaye alikuwa anaongoza kikao hicho, juu ya posho, maslai na stahiki za madiwani.
Baada ya hoja hiyo kujibiwa na Mwanasheria wa halmashauri hiyo Godfray Jafari kwa kuainisha aina za posho madiwani waliomtaka kaimu mkurugenzi Peter Mwelekela kutoa maelezo juu ya madai ya fedha zao za posho za miezi mitano wanayodai pamoja na kiiunua mgongo chao kabla ya baraza kuvunjwa.
Abdala Mkumbaru diwani wa kata ya Chumo alisema kuwa hakuna haja ya kuendelea na baraza kama ofisi ya mkurugenzi haina majibu yakutosha juu ya malipo ya madeni ya madiwani hao.
Mkumbaru alisema kipindi cha madiwani kuwa madarakani kimebaki kifupi sana hivyo kama halmashauri hataweza kuwalipa katika kipindi hiki cha dakika za lala salama hawawezi kuzipata tena fedha.
Diwani Haji Mulike alisema madiwani hawako tayari kuendelea na kikao hicho mpaka mkurugenzi alipe madai yao katika kikao hicho ndipo waendelee.
Mulike alisema kuwa watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa na dharau kwa madiwani na kuwasababishia madeni katika taasisi za fedha baada ya kushindwa kulipa madeni ya mikopo ambapo kila mwezi ukatwa lakini hazifikishi benki kwa ajili ya kulipa madeni yao.
Alisema kuwa kwa kipindi cha miezi zaidi ya mitano madiwani wamekuwa wakikatwa fedha za posho zao kwa ajili ya kulipia madeni ya mikopo ya zaidi ya shs milioni 43 hazijalipwa hadi sasa.
Kwa upande kaimu mkurugenzi mtendaji Peter Mwelekela aliwataka madiwani hao kuendelea na kikao hicho wakati zoezi la kuwalipa madeni yao linashughulikiwa kiutekelezaji.
Kauli hiyo iliongeza vurugu hadi kumlazimu makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bakari Nalinnga kufunga kikao hicho kwa kubadilisha tarehe ya kufanyika tena huku akiwaangiza watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanatafuta majibu na fedha za kumaliza tatizo.
Previous Post Next Post