Unknown Unknown Author
Title: MATOKEO VPL: MTIBWA SUGAR YAREJEA KILELENI, YATOKA 1-1 NA JKT RUVU, COASTAL UNION YABANWA MKWAKWANI
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MABINGWA mara mbili wa Tanzania, 1999 na 2000, Mtibwa Sugar wamewatoa kileleni mwa msimamo mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara, ...
Mtibwa Sugar
MABINGWA mara mbili wa Tanzania, 1999 na 2000, Mtibwa Sugar wamewatoa kileleni mwa msimamo mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara, Azam fc baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na wenyeji JKT Ruvu katika mchezo uliochezwa hapo jana katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam.

Azam walirejea kileleni juzi baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga, ambapo walifikisha pointi 17 na magoli 11 ya kufunga kufuatia kushuka dimbani mara 9.

Kutokana na Mtibwa Sugar kuvuna pointi moja, wamefikisha pointi 17 sawa na Azam, lakini wamewazidi wakali hao wa Chamazi kwa magoli ya kufunga kwani sasa wametikisa nyavu mara 12 katika mechi 9 walizokipiga.

JKT Ruvu nao wamefikisha pointi 17 katika nafasi ya tatu kutokana na kuwa na magoli 11 katika mechi 11 walizocheza.

Katika mechi ya jana, JKT Ruvu waliandika bao la kuongoza katika dakika ya 7’ kupitia kwa mshambuliaji mwenye uchu wa magoli, Samuel Kamuntu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Said Mohammed.
Mtibwa walishindwa kutumia nafasi nzuri waliyopata katika dakika ya 13’ ambapo Musa Hassan Mgosi alipata pasi kutoka kwa Ame Ally katika eneo la hatari na kuingiza krosi nzuri, lakini Ally Shomari alipaisha mpira juu ya lango..

Coastal UnionCoastal Union wametoka suluhu dhidi ya Polisi Morogoro uwanja wa CCM Mkwakwani.

JKT Ruvu waliendelea kufika langoni kwa Mtibwa kutokana na nidhamu ndogo ya walinzi wa Wakata Miwa na katika dakika ya 25’ iliingizwa kona maridadi na ikatokea piga nikupige langoni mwa vijana wa Manungu na Ally Bilal akazamisha mpira nyavuni, lakini mwamuzi alipuliza kipyenga kuashiri ameotea.

Mpaka dakika hiyo tayari JKT Ruvu walikuwa wamepata kona tatu wakati Mtibwa hawakupata kona yoyote, kitendo kilichodhihirisha kuwa wenyeji walifika zaidi langoni kwa mpinzani wao.

Bilal alipata nafasi nzuri katika dakika ya 32’ kufuatia mabeki wa Mtibvwa kudhani ameotea, akapiga shuti lililopanguliwa na kipa Mohammed.
Mtibwa waliendelea kucheza chini ya kiwango hususani safu ya ulinzi na dakika ya 33’, kocha Mecky Mexime akalazimika kumtoa Dickson Daudi na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhani Kichuya.

Dakika ya 37’ David Charles Luhende aliingiza kona kutoka winga ya kushoto, Ame Ally alipiga kichwa baada ya kuwachekecha mabeki wa JKT Ruvu na kuzamisha mpira nyavuni akiisawazishia Mtibwa.

Mbali ya goli hilo, mashuti ambayo yalilenga lango mpaka dakika 40’ yalikuwa matatu kwa JKT Ruvu na mawili kwa Mtibwa Sugar.

Dakika ya 44’ iliingizwa kona na Luhende, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ alitumbukiza gozi kimiani kwa mkono na mwamuzi Aman Paul kutoka Musoma Mara akamuonesha kadi ya njano.
Mpaka dakika 45’ zinakamilika, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

JKT Ruvu walimiliki mpira kwa 52% dhidi ya 48% za Mtibwa Sugar.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kucheza mpira wa taratibu na kushambuliana kwa zamu, lakini Mtibwa Sugar walipata nafasi nyingi za kufunga, ingawa washambuliaji wake Mudathiri Yasini, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ na Ame Ally hawakuwa makini.

Dakika ya 72’ kama kawaida, Mgosi alikwenda benchi na nafasi yake kuchukuliwa na Vicent Barnabas. Katika mechi nyingi wachezaji hawa wawili wamekuwa wakibadilishana nafasi.
Katika dakika ya 78’ Abdallah Juma aliingia kuchukua nafasi ya Ame Ally ‘Baba Amina’
Mpaka dakika 90’ zinamalizika timu hizo mbili zimetoka sare ya bao 1-1.

Mechi nyingine ya ligi kuu ilichezwa uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga ambapo Wagosi wa Kaya, Coastal Union wametoka suluhu (0-0) dhidi ya Polisi Morogoro.
Kikosi hicho cha Mkenya James Nangwa kilicheza soka kali na la kushambulia muda mwingi, lakini vijana wa Adolf Rishard walikuwa imara kuzuia mashambulizi hayo.

Coastal Union wameonesha makali kiuchezaji, lakini bado wamekuwa na tatizo katika nafasi ya ushambuliaji, hivyo kocha anatakiwa kurekebisha tatizo.
Kwa matokeo hayo Coastal Union wamefikisha pointi 12 wakati Polisi Moro wamefikisha pointi 15.

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top