WAKUU WA USALAMA WATIMULIWA KAZI

Joseph Ole Lenku
Aliyekuwa waziri wa usalama Joseph Ole Lenku

Rais Uhuru Kenyatta amemwachisha kazi waziri wa usalama Joseph Ole Lenku na kumpendekeza waziri mpya wa usalama Joseph Nkaiseri kuchukua nafasi hio.

Wakati huohuo mkuu wa polisi nchini Kenya inspekta generali David Kimaiyo amejiuzulu kutokana na shinikizo dhidi yake afanye hivyo kwa kushindwa kukabiliana na utovu wa usalama nchini.

Rais Kenyatta alisema kuwa baada ya mazungumzo na Bwana Kimaiyo alikubali 'kustaafu' mapema kutoka kwa majukumu yake kwa sababu za kibinafsi.

Rais alitoa tangazo hilo wakati akihutubia taifa kufuatia shambulizi la hapo jana dhidi ya wachimba migodi 36 waliouawa na Al Shabaab mjini Mandera Kaskazini ya Kenya.

Rais pia alitangaza kuwa amekubali ombi la Generali wa polisi David Kimaiyo kuachia wadhifa wake.

Kimaiyo na Ole Lenku wamekuwa wakikabiliwa na shinikizo za kuachia ngazi kufuatia kukithiri kwa utovu wa usalama nchini.

David Kimaiyo
Aliyekuwa mkuu wa polisi David Kimaiyo

Hatua ya kuwatimua kutoka katika nyadhifa zao wawili hao bila shaka litakuwa jambo la kuridhisha kwa wakenya wengi ambao wamekuwa wakilalamikia utovu wa usalama na kuwataka waondoshwe ofisini.

Uteuzi wa Joseph Nkaisery kama waziri mpya wa usalama ni jambo jipya kwani atakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka kwa upinzani kuwa ndani ya serikali.

Alipokuwa anahutubia nchi,Rais Kenyatta aliwasihi wabunge kuongeza mda wa vikao vyao vya leo ili kumhoji na kumkagua Nkaisery aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya waziri mpya wa usalama na maswala ya ndani ili wamuidhinishe.
>>BBCSWAHILI

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post