Unknown Unknown Author
Title: MAKALA TAMASHA LA RAMBIRAMBI YA SIDE BOY
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MAREHEMU SIDE BOY ENZI ZA UHAI WAKE NA SALUM MKANDEMBA KIGWEMA, BEST NASO, SAM WA UKWELI, 20% WAFANYA ONYESHO NYANGAO HAPO JANA...
MAREHEMU SIDE BOY ENZI ZA UHAI WAKE

NA SALUM MKANDEMBA

KIGWEMA, BEST NASO, SAM WA UKWELI, 20% WAFANYA ONYESHO NYANGAO HAPO JANA

Ø     Ni katika Onesho Maalum kumuenzi Side Boy
Ø     Mama wa marehemu afunguka, aomba sapoti
 
SIKU 40 zimepita tangu tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini ilipopata pigo baada ya kumpoteza mmoja wa wasanii mahiri, Said Salum Hemed maarufu kwa majina ya kisanii kama Side Boy, Side Mnyamwenga na lile ambalo mwenyewe alikuwa akipenda kujiita la Rais wa Kusini. 

Hakika alikuwa na sifa zote za kujiita Rais wa Kusini, ambapo akiwa hai aliweza kuiwakilisha vema Kanda ya Kusini kupitia muziki wa Bongo Fleva, ambako alitamba na vibao kadhaa vilivyobeba ujumbe mzito uliokonga nyoyo za mashabiki, lakini ukitoa elimu ya kina kwa kila waliosikiliza mistari yake. 

Taarifa za kifo chake ziliibua simanzi kuu kwa kila mdau wa Bongo Flava, ambapo nyimbo zake kama Hujafa Hujaumbika, Usimdharau Usiyemjua na nyingine, zilirejea kupigwa tena na tena katika kumkumbuka mkali huyo, ambaye alifanya makubwa kupitia nyimbo hizo alizowashirikisha Best Naso na Ney wa Mitego. 

Siku Hazigandi, ndivyo navyoweza kusema, kwani licha ya ukweli kuwa maumivu ya kumpoteza Side Boy yakiwa hayajanipungua moyoni, tayari familia ya marehemu, leo inafanya ibada maalum ya arobaini, kumuombea mkali huyu ambaye kwangu mimi I zaidi ya rafiki.
Ni ndugu, niliyejuana naye kabla hajakuwa msanii, wala mimi sijawa mwandishi wa habari…tulitoka kumoja mkoani Lindi, ambako yeye alitoka Kijiji cha Ujamaa Mtama yaliko Makao Makuu ya Jimbo letu, huku mimi nikitoka Kijiji cha Ujamaa Mtumbya..kisha tukaja kukutana Dar es Salaam. 

Tukaja kukutana Dar es Salaam, ambako tulikuwa pamoja katika harakati za kibiashara, ambazo alishiriki kabla ya na baada ya kujipatia umaarufu kwenye Bongo Flava, biashara ambazo mimi nilizifanya/nazifanya sambamba na uandishi wa habari, ambao ulinifanya nimtangaze vya kutosha…wadau wakamjua na kujua anachofanya.

Tamasha la kumuenzi kuunguruma Nyangao leo
Sambamba na shughuli ya 40 ya marehemu Side Boy, wadau wa sanaa wameandaa shoo kali iliyolenga kukusanya pesa kwa ajili ya kuichangia familia yake kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali baada ya kuondokewa na mtegemezi wao Rais wa Kusini, ambaye alijipambanua kwa utunzi wa nyimbo za ujumbe. 

Kutokanana kupata taarifa za uwapo wa shoo maalum ya kukusanya rambirambi za msiba wa Side Boy, nilifanya jitihada za kuwapata na kuongea kwa simu na familia ya marehemu, lakini pia waratibu wa shoo hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa miongoni mwa mashabiki wa mikoa ya Kusini.

Mama mzazi wa Side Boy anavyoizungumzia shoo
“Hakika siku zinakimbia mwanangu, na hatimaye arobaini ya mwanangu Side Boy ni Ijumaa Novemba 7. Kama familia tutakuwa na mkesha wa Arobaini itakayoingia Ijumaa kuamkia Jumamosi, ambayo ni utaratibu wa kawaida tu kidini kulingana na imani yangu ya Uislamu, ambayo pia ilikuwa dini ya mwanangu. 

“Lakini ukiondoa shughuli yetu hiyo, rafiki zake wamebuni wazo moja la kumuenzi mwenzao na watafanya onesho maalum la kukusanya rambirambi, ambalo sisi kama familia tumeruhusu, kwani ingawa liko kinyume na imani ya dini, lakini halikwepeki katika tasnia ambayo yeye alikuwa akijihusisha. 

Tumefurahishwa na wazo hilo na naamini litatusaidia kwani Side Boy ameacha majukumu mbalimbali ambayo kupitia kitakachokusanywa katika onesho hilo, tutaweza kupunguziwa mzigo. Wito wangu mashabiki wajitokeze kwa wingi, lakini umoja huo usiishie siku ya onesho, kama familia tunahitaji kufarijiwa na kila mmoja.” 

Hiyo ilikuwa ni kauli ya Sharifa Ali Kawanga, ambaye ni mama mzazi wa Side Boy, ambaye aliwaomba wadau wa muziki kutoisahau familia ya Side Boy, wakiwamo watoto watatu aliowaacha na mjane, ambao wanahitaji sana sapoti kama inayotarajia kuoneshwa leo kijijini Nyangao.

Kauli ya Mratibu Mkuu wa Shoo hiyo – Hamadi Khamisi
Kwa upande wake, Mratibu kinara wa shoo hiyo, Hamadi Khamisi, alikiri kutambua mazingira aliyoyaacha Side Boy kwa familia, inayohusisha wazazi, watoto wa marehemu huyo na mjane wake. 

“Wazo hili lilitokana na fikra yakinifu za namna gani tutaungana na familia kuomboleza msiba wa Side Boy. Tunashukuru kuona wadau wa muziki wajitokeza kutuunga mkono, wito wetu ni kuwaomba wafike kwa wingi siku ya onesho, ili kupitia kiingilio kidogo tulichopanga waweze kuichangia familia. 

“Ameacha mjane na watoto, ambao tunatakiwa kuwasapoti kupitia kiingilio tulichopanga ambacho ni shilingi 3,000, mauzo na manunuzi ya fulana maalum zenye picha yake lakini pia harambee maalum ambayo kila atakayeingia atachangia kwa uwezo wake bila kujali kiingilio alicholipa ama fulana (t-shirt) atakayonunua.

Kigwema – Msanii/Mratibu mwenza anavyoizungumzia

Hakuna asiyemfahamu Kigwema, ni mkali mwingine mwenye jina kubwa tu katika muziki wa kizazi kipya nchini, ambaye amefunguka kuizungumzia shoo hiyo, aliyoiita ‘fursa muhimu na adhimu’ ya mashabiki kuonesha upendo na moyo wa kujali kwa familia ya marehemu Side Boy. 

“Wazo la kuja kufanya shoo hii lilizaliwa siku ya kumzika Side Boy, baada ya kuona mazingira aliyoiacha familia yake na kilio alichotoa mke wa marehemu, ambaye alikuwa akilalamikia jukumu zito la malezi aliloachiwa na marehemu huyo la kuwalea na kuwasomesha watoto watatu aliowaacha. 

Tukazalisha wazo la kufanya shoo maalum ambayo itakuwa kwa ajili ya kukusanya rambirambi, nia ni kupata kuanzia angalau shilingi mil. 1 ambayo kwa kuanzia itasaidia katika kumsomesha mtoto wake mkubwa, na kuwalea vijana wake wawili wadogo katika kipindi hiki ambacho mama yao anakusanya nguvu. 

“Familia ya marehemu (wadogo zake) watakaa mlango kuangalia kila senti inayoingia, lakini itasimamia pia mauzo ya fulana maalum (t-shirt) na kusanyo la harambee ya pesa taslimu nje ya viingilio. Tunaamini tutakuwa tumesaidia kwa kiasi Fulani,” alisema Kigwema ambaye aliwataka amashabiki kujitokeza kwa wingi. 

Kigwema alisema kila kitakachopatikana kupitia mchakato huo, kitakabidhiwa kwa familia kabla ya kumalizika kwa shughuli ya arobaini Jumamosi, ndio maana wamepanga kuifanya shoo mapema, ili kufanikisha makusanyo na kuyawasilisha kwa familia, ambayo itagawa sambamba na mali zingine za marehemu mchana wa Jumamosi.

Wakali watakaopamba shoo Nihamo Garden Nyangao
Shoo hii maalum itafanyika katika Ukumbi wa Nihamo Garden uliopo kijijini Nyangao, ambako Side Boy alifariki akiwa anauguzwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lindi iliyopo kijijini hapo iitwayo St. Walburg’s Hospital. Nyangao ni kijiji jirani na Mtama, ambako ni nyumbani kwa marehemu. 

Wakali kadhaa wametajwa kuwamo katika shoo ya leo, huku wengi zaidi wakitarajiwa kuwa sehemu ya onesho hilo, ambalo lengo so kutoa burudani, bali ni kukusanya rambirambi za kuisaidia familia ya marehemu. Wapo wasanii gumzo kwa mikoa ya Kanda ya Kusini, lakini pia wamo wakali gumzo Tanzania kama Kigwema. 

Wakali wanaotarajia kuwamo ukiondoa Kigwema ni pamoja na Best Naso, Nyasi, Twenty Percent (20%), Sam wa Ukweli, Kundambanda (Mapembe), Msaga Sumu, Jongo Sudy na wengineo ambao walikuwa wakiendelea kuthibitisha ushiriki wao. 

Side Boy alifariki akiwa St. Walburg’s Hospital, alikokuwa amelazwa akitibiwa ugonjwa wa TB ya Mifupa, ambayo ilichukua uhai wake, atakumbukwa kazi mbalimbali alizotoa na kumtangaza vilivyo Rais huyo wa Kusini aliyekataa katakata kuimba nyimbo za mapenzi ili kutanua pato lake. 

Alianza kuiteka tasnia ya muziki wa kizazi kipya kwa kibao cha Kua Uyaone alichoimba na Ali Kiba, akaja na wimbo wa Jifungue Salama, kabla ya kutikisa katika Hujafa Hujaumbika aliomshirikisha Best Naso na Usimdharau Usiyemjua aliofanya na Ney wa Mitego. Kuna nyimbo nyingine nyingi alizotikisa nazo, zikiwamo Tafuta Utapata, Nitakupenda Tu, Sina Mtoto aliofanya na Ney wa Mitego, Sababu ni Wivu aliomshirikisha Q-Jay na nyinginezo.
Nyimbo ambazo alisisitiza kutokuwa na mpango wa kuimba mapenzi ili kupata pesa, kwani ametosheka na kushukuru kwa anachopata kupitia ‘nyimbo za meseji’ ambazo ukweli uko wazi tu kwamba zilimtangaza na kumpa heshima kubwa, zikigusa hasa hisia za waliomsikiliza akiimba. Mungu amlaze mahali pema PEPONI. Aamin.
 
Makala hii imetayarishwa na Salum Mkandemba
Kwa maoni, maswali ama ushauri kwa mwandishi
Barua pepe; mkandemba@yahoo.com
Simu namba: 0789 94 77 44 0656 11 47 57

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top