Mzazi aliyeoza mtoto wake kwa mzee wa miaka 54, juzi alikamatwa na polisi na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda, na kufunguliwa kesi ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuozesha mtoto mdogo kinyume cha sheria. Aliyefikishwa katika Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Ahmed Kasonso, ametambuliwa kwa jina la Kakwaya Monge au Luguya (53) mkazi wa Kijiji cha Nyaburundu wilayani hapa.
Aidha, mzee anayetuhumiwa kuoa mtoto huyo ambaye awali ilidaiwa kuwa anao umri wa miaka minane, lakini juzi mahakamani ikaelezwa kuwa umri wake ni miaka 12, Changwe Changigi (54), naye amefikishwa katika Mahakama hiyo na kushitakiwa kwa makosa yote matatu, likiwemo la kubaka.
Akiwasomea mashitaka yao Mwendesha Mashitaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Masoud Mohammed, alisema kuwa washitakiwa wote kwa pamoja wanashitakiwa kwa kosa la kula njama kwa nia ya kutenda kosa.
Mohammed alisema kuwa mzee anayetuhumiwa kuoa mtoto huyo anashitakiwa kwa makosa yote matatu, yakiwemo ya kubaka na kuoa mtoto mdogo kinyume cha sheria.
Alisema kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo siku ya mwaka mpya 2014 majira ya saa 10.00 jioni katika Kijiji cha Nyaburundu, wilayani hapa.
Aidha, awali alipohojiwa na Dawati la Jinsia katika Kituo Kikuu cha Polisi Bunda,
likiongozwa na Rita Charles, mzazi wa mtoto huyo, alisema kuwa aliamua kumuoza mtoto wake kwa sababu alikuwa anaumwa ugonjwa wa moyo na kwamba fedha za kishika uchumba Sh 55,000 alizopewa zilimsaidia kununua dawa za ugonjwa huo.
Pia akizungumza na mwandishi kabla ya Mahakama kuanza mzazi wa mtoto huyo alisema kuwa mwanawe huyo hakuwa mwanafunzi kwani alimuachisha shule miaka miwili iliyopita, baada ya kuugua ugonjwa wa moyo, ili amsaidie kazi za nyumbani kwani mke wake walikwishaachana na kuolewa sehemu nyingine.
Alisema kuwa mke wake ambaye ndiye mama wa mtoto huyo waliachana mwaka 2010 na akaolewa na mwanamume mwingine katika Kijiji cha Hitubiga-Lamadi Wilaya ya Busega mkoani Simiyu na kwamba mwaka 2012 alizaa mtoto mmoja kwa mwanamume aliyemuoa.
Aliongeza kuwa mke wake huyo waliachana wakiwa na watoto 11, ambapo tisa ni wa kiume na wawili ni wa kike na kwamba hapo nyumbani alikuwa akiishi na watoto wanne tu, akiwemo huyo aliyemuoza.
Naye mzee huyo alipozungumza na mwandishi alisema kuwa alimchukua mtoto huyo na kuamua kuishi naye kama msaidizi wa ndani, kwani aling’atwa na kiboko mguu wa kushoto na kujeruhiwa vibaya na kwamba alikuwa hafanyi naye tendo la ndoa. Hata hivyo baadhi ya watetezi wa haki za watoto walisema kuwa huo ni uongo na kwamba atachukuaje mtoto mdogo kumfanyia kazi za ndani hali anao watoto wengine wanne wakiwemo wa kike wawili hapo nyumbani kwake.
“Huyo mzee ni mwongo kabisa atachukuaje mtoto wa mtu na kumtoa shule eti amsaidie kazi za ndani…ni kwanini watoto wake anaoishi nao wasimsaidie kazi hizo za ndani,” alisema mwanaharakati mmoja.
Kwa mujibu wa Polisi mwanamume huyo alikamatwa juzi akiwa anaishi na mtoto huyo (jina limehifadhiwa) kama mke wake nyumbani kwake na kukamatwa kwake kunatokana na taarifa ya siri kutoka kwa raia wema.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.