Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro pichani.
Wadau, waandishi wengi wa habari wananipigia nithibitishe ikiwa CUF iliandaa makundi ya wanachama wakamshabikie ZZK mahakamani leo hii. Taarifa ya namna hii pia imeenea mitandaoni.
Pia viongozi kadhaa wa CHADEMA wamenipigia kunijulisha kuwa Intelijensia yao imegundua kuwa vijana wa CUF wamepenyezwa na kwamba wamevishwa T-SHIRT za M4C na mapanga.
Napenda kuwajulisha wadau wote kuwa CUF haijapanga wala kutuma makundi ya vijana kwenda kumshabikia ZZK. Ikiwa pana wanachama wa CUF wameonekana mahakamani itakuwa wamekwenda kwa Utashi na Matakwa yao.
Sisi chama Taifa hatujawahi kukutana, kupanga wala kutuma vijana wa CUF wakasimamie upande wowote katika mgogoro huu. Wakati wa fukuto la HAMAD RASHID na CUF watu wengi tu raia walifika mahakamani, sie hatukuwa kuhoji na kutafuta vyama vyao, tuliamini ni watanzania tu.
Ni ushauri wangu kuwa, panapokuwa na kesi inayovuta hisia za watu haitajalisha watu hao wanatoka makundi gani, mwenye kutaka kwenda atakwenda tu.
Ni vigumu kwa chama chetu kukataza wanachama wake wasihudhurie kesi ya Babu Seya, ya Sheikh Ponda, ya Zitto Kabwe, ya Samaki wa magufuli n.k., Unapokuwa na chama chenye mamia elfu ya wafuasi si rahisi kujua mfuasi yupi yuko wapi kwa wakati gani anafanya nini na ametumwa na nani.
Lakini kwa ajili ya kujenga mshikamano wa vyama vyetu, tunachunguza taarifa hizo ili kubaini kama ni kweli palikuwa na wanachama wetu mahakamani na tukiwabaini tutawahoji na kujua nani aliyewatuma na tutaona hatua za kuchukua.
Ikumbukwe kuwa mwenyekiti wa chama chetu taifa Prof. Lipumba wakati akisoma maazimio ya kikao Cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa mwezi Desemba mwaka jana alieleza kuwa Baraza Kuu la CUF linawaomba CHADEMA wamalize mgogoro wao haraka ili tuwekeze nguvu za upinzani katika kuunganisha umma kutafuta katiba ya watanzania katika bunge la katiba, Msimamo wa CUF ni kutokuwa na upande katika mgogoro huu.
Tunatoa wito kwa viongozi wa CHADEMA kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama iwapo wataona au kuhisi kuna mwananchi au mfuasi wa chama chetu amejiingiza katika mgogoro wao na kwamba amehatarisha amani ili sheria ichukue mkondo wake.
CUF itaendelea kuiheshimu CHADEMA kama taasisi inayojitegemea. Hatukuwahi kuingilia, kushabikia wala kupinga masuala na maamuzi ya ndani ya CHADEMA, tukiona pana jambo linatugusa mara zote huwa tunatoa ushauri wetu tu na sio kuingilia masuala ya ndani ya vyama vingine.
Julius Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu,
Chama Cha Wananchi CUF,
Tanzania Bara.
06 Jan 2014.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.