Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
KWA: MHE. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, JAKAYA MRISHO KIKWETE
Ndugu,
YAH: UNYANYASAJI ULIOPITILIZA WA BODI YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WASOMAO CHINA
Tafadhali rejea mada iliyotajwa hapo juu.
Mheshimiwa Rais, awali ya yote, tunapenda kuchukua fursa hii kukupa pole na majukumu yako ya kila siku na kukutakia heri ya Mwaka Mpya.
Mheshimiwa, tunaandika barua hii ya wazi kwako tukiomba kutatuliwa matatizo yetu makuu mawili. Tumefikia hatua hii baada ya kushindwa kupata suluhisho la matatizo haya kwa watendaji walio chini yako ambao ni Bodi ya Mikopo (HESLB) na Ubalozi wa Tanzania nchini China (kupitia mwambata wa wanafunzi).
1. Ucheleweshwaji uliopitiliza wa pesa za kujikimu.
2. Kiwango kidogo cha pesa ya kusafirishia na kutolea mizigo.
UCHELEWESHWAJI ULIOPITILIZA WA PESA ZA KUJIKIMU:
Kwa masikitiko makubwa tunapenda kuwasilisha tatizo la ucheleweshwaji uliopitiliza wa pesa za kujikimu kwa wanafunzi tunaoendelea na masomo yetu nchini China. Kwa mujibu wa utaratibu wa Bodi ya Mikopo ni kwamba pesa hii ya kujikimu inayozungumziwa ilipaswa iwe imemfikia kila mwanafunzi kwa mwaka wa masomo kila uanzapo mwezi wa tisa (Septemba). Lakini katika hali ya kusikitisha, pesa hii bado haijatufikia hadi sasa mwezi Januari.
Tumejaribu kuchukua hatua nyingi za awali ikiwemo kuwasiliana na ubalozi wtu kwa kupitia mwambata wa wanafunzi wasomao China (ushahidi upo ) pia tumefanya mawasiliano na Bodi ya Mikopo moja kwa moja bila mafanikio yoyote (ushahidi upo ushahidi ) zaidi ya kuambulia majibu yasiyo na kichwa wala miguu (ushahidi upo ).
Licha ya sisi kuwa wavumilivu kwa miezi zaidi ya mitano sasa, bado tunaendelea kupewa majibu mepesi ya kwamba tuendelee kuwa na amani na wavumilivu kwamba pesa zitakuja tu lakini haijulikani ni lini, mwezi gani na nini hasa chanzo cha kucheleweshwa mikopo hiyo?
Ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wanatarajia kuhitimu mwezi wa saba (Julai) licha ya kwamba wanahitaji pesa ya kujikimu ila pia watahitaji pesa kwa ajili ya kusafirishia mizigo yao pindi watakapomaliza muda wao wa masomo nchini China.
KIWANGO KIDOGO CHA PESA YA KUSAFIRISHA MIZIGO:
Moja ya changamoto kubwa ambayo imekuwa ikitukabili wanafunzi tusomao China na hasa wakati wa kuhitimu masomo yetu ni usafirishaji wa mizigo (vitu mbalimbali vikiwemo vifaa vya utafiti, vitabu na vitu binafsi).
Kwa wanafunzi waliohitimu kabla ya mwaka 2013 walikuwa wanapewa pesa ya kusafirishia mizigo kuanzia Dola za Kimarekani 3,000 hadi 3,500 lakini baadaye Bodi ya Mikopo iliamua kupunguza pesa hiyo kufikia Dola za Kimarekani 1,200.
Ukweli ni kwamba gharama za usafirishaji wa mizigo kutoka China kwenda Tanzania zimeongezeka kwa kasi sana na pesa hii kwa uhalisia haitoshi hata kidogo.
Kwa mshangao mkubwa na bila kushirikishwa kwa wanafunzi tusomao China ambao ndiyo wanufaikaji, Bodi ya Mikopo iliamua kupunguza pesa hiyo kwa zaidi ya asilimia 100 hadi kufikia Dola za Kimarekani 1,200, pamoja na kwamba kiasi kilichoombwa baada ya utafiti wa kina juu ya gharama za usafirishaji na utoaji mizigo viliambatanishwa.
Kiasi hicho kusema ukweli hakikidhi gharama za usafirishaji wa mizigo ya wahitimu kutoka sehemu mbalimbali za China kwenda nyumbani Tanzania.
Mfano mwaka jana wanafunzi walishindwa kusafirisha baadhi ya vitu vyao kutokana na gharama kuwa kubwa sana na ambao waliweza kuongeza pesa kutoka mfukoni mwao na kusafirisha walishindwa kuvitoa pale bandarini Dar es Salaam.
HITIMISHO:
Kutokana na matatizo haya na mengine mengi ambayo tunashindwa kuyaeleza hapa, suala hili limesababisha usumbufu mkubwa kwa wanafunzi katika shughuli zao za kimasomo. Hii ni pamoja na baadhi ya tafiti zao kushindwa kufanyika ipasavyo.
Ombi letu kwa Mh. Rais ni kwamba tunaomba tupatiwe ufumbuzi wa matatizo yetu haraka kwa sababu tumeshavumilia vya kutosha. Tunaomba pesa ya kujikimu iwe inatumwa kwa wakati na pia pesa ya kusafirishia mizigo ipatiwe ufumbuzi.
Aidha irejeshwe kama ilivyokuwa awali au ikiwezekana iongezwe ili kukidhi gharama za usafirishaji na utoaji mizigo Tanzania.
Mheshimiwa Rais, ni wazi kuwa tumehuzunishwa na kusikitishwa sana na udhalilishaji, uonevu na unyanyaswaji tunaofanyiwa kutokana na kutowajibika kwa baadhi ya watendaji wa Bodi ya Mikopo na ubalozi wetu ama kwa kutambua au kutotambua wajibu wao.
Tunaamini suala letu utalipa uzito unaostahili.
Tunatanguliza shukrani zetu za dhati na pia tunakutakia mafanikio mema katika shughuli zako za ujenzi wa taifa.
Wako wanafunzi wa Tanzania walio China.
SOURCE: GPL
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.