Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali kwa upande wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA kinachonisukuma kusema kuwa tunachoona hivi sasa ni historia. Bila kupoteza muda mrefu kujaribu kuzungumzia matukio naona kuwa watanzania tungefaidika zaidi kuelewa vyema zaidi nini hasa tunachokiona.
Lazima tukubali kuwa lengo moja kuu (kama si lengo kuu pekee) ya chama chochote cha kisiasa ni kuingia madarakani. Vyama hivi vinaweza kutushawishi kuwa wanataka madaraka haya kwa sababu wanataka kutusaidia na ni haki na wajibu wetu kutathmini na kuamua ni chama kipi kitatusaidia kama jamii kufikia malengo tutakayokubaliana nayo. Lakini kwa kifupi wanataka madaraka. Tukishakubali hali hii, basi tunaweza kuangalia tukio lolote la kisiasa kama ushindani wa kutwaa madaraka. Na ni muhimu tutambue hili bila kujaribu kudai kuwa eti mwanasiasa au chama fulani kinatupenda na kutujali zaidi na kadhalika. Hilo ni suala la mtazamo na kwa sasa tuliweke pembeni.
Ninachotaka tujaribu kuangalia ni kuwa ushindani huu wa kutwaa madaraka pia yapo ndani ya chama chochote cha kisiasa. Na ni kitu kizuri sana. Naamini ndani ya CCM, CHADEMA, CUF, NCCR tutaendelea kuona malumbano kwa sababu ya uchaguzi mkuu 2015. Ni uchaguzi wa kihistoria kwa sababu rais aliyopo madarakani hatagombea tena (hakuna incumbent) hivyo hata mgombea wa CCM atakuwa ‘mgeni’ kwa wapiga kura. Hivyo vyama vya upinzani vina nafasi kubwa sana wakicheza karata zao vizuri. Lakini pia ndani ya CCM, hakuna mteule mpaka sasa – kwa hiyo yoyote anaweza kuibuka kuwa mgombea. Tukishaweza kuangalia hali ya kisiasa kwa jicho hili tutaona kuwa ndani ya vyama kuna makambi ambayo yanaona kuwa wao wakiendesha chama sasa wanaweza kukihakikishia ushindi chama chao. Hivyo uongozi wa chama nao unawaniwa. Na ninarudia hakuna ubaya wowote tena ni kitu kizuri. Kwani asiyekubali kushindana si mshindani – na ukweli ni kuwa mgombea ambaye atateuliwa tu na chama chake bila kupitia ushindani mkubwa ndani ya chama chake, mara nyingi hawi mgombea mwenye ushwawishi mkubwa.
Ninakiri kuwa mi ni muumini wa ushindani katika nyanja zote kwani ninaamini ushindani hatimaye huleta matokeo mazuri kwani maoni mbalimbali yakigonganishwa basi tunaweza kupata kitu bora. Kwa bahati mbaya, ushindani katika historia ya nchi yetu haikuwa neno zuri au dhana iliyokubalika – katika sekta ya uchumi na hata siasa. Tunaweza kukaa na kuongea na kuleta nukuu za Baba wa Taifa kuwa alipenda ushindani lakini ukweli halisia ni kuwa kulikuwa hakuna uhuru wa kusimama na kum-challenge yeye kama kiongozi, au chama (mfumo wa chama kimoja), ushindani wa kibiashara nk. Na ili kuweza kukamilisha maoni yangu nitaomba tukiweke hiki kiporo, na mvumilie mawazo yangu kwa sasa.
Sasa basi ni katika historia hii ndo tunaona vyama vya upinzani hapa nchini vilizaliwa na kwa kweli historia itakuja kutambua mchango mkubwa wa wale wachache waliokuwa na uthubutu wa ku-challenge system wa wakati huo. Lakini sasa kipindi kile cha awali cha kuunda umekamilika, kwani hivi leo kuanzisha chama cha siasa, NGO au kampuni si kitu cha ajabu. Kinachofuata sasa ni UIMARISHAJI wa vyama hivi.
Vyama hivi vinahitaji kuimarishwa kwa sababu ni lazima vitoe taswira mpya na tofauti na chama kilichopo madarakani tangia uhuru – ya kuwa demokrasia ya kweli ni mfumo yaani taasisi na si ya kikundi fulani. Na hapo ndipo ninapoona tatizo. Vyama vya upinzani vimejaa kutokuaminiana. Hii inatokana na kuwa wakati wa kuundwa kwao – juhudi za wazi na za siri zilifanyika kuwahujumu na hadi leo hii juhudi hizi zipo kwani narudia kwenye kile nilichokizungumzia hapo juu kuwa vyama vya siasa vinataka madaraka. Yule aliyopo madarakani hatakubali kuondoka kwa hiari, hivyo ndiyo maana demokrasia inahitajika kuhakikisha kuwa kwa njia ya wazi, anayekuwa madarakani anakubalika na walio wengi, na hatimaye awapishe wengine. Sasa hapo ndipo tunapokuja na kuleta dhana hii hii ndani ya chama chochote cha siasa. Ushindani huu ni muhimu, ili kujenga imani. Na ningependa nitoe mfano wa nchi ya Marekani ambayo kwa karne nyingi kumekuwa na ushindani wa kisiasa tena mkali sana.
Mwaka 1968 chama cha Democratic ilikuwa na mkutano wake mkuu jijini Chicago yaani National convention. Wajumbe na wanachama walikuwa wametofautiana mawazo kutokana na kuwa mgombea mmoja Hubert Humphrey (makamu rais) alionekana kubebwa na kupendelewa na viongozi wa chama na rais wa wakati huo Johnson (ambaye alitangaza kutogombea tena). Wanachama na wafuasi wa mgombea Eugene McCarthy walikataa matokeo na maandamano makubwa yalifanyika katika eneo lililozunguka mkutano mkuu. Ni vyema kujua pia kwamba McCarthy alikuwa mgombea pekee ambaye mapema kabisa alikuwa tayari kum-challenge rais Johnson ambaye mwanzoni alikuwa tayari kugombea. Katika kura za awali katika mkoa (state) ya New Hampshire, McCarthy alipata 42% na Johnson 49%. Hii ilimshtua rais Johnson ambaye hatimaye alijitoa na kumpendekeza makamu wake. Uthubutu wa McCarthy ya kum-challenge rais aliyopo madarakani na kupata sapoti kubwa pia iliwahamsisha wagombea wengine kuingia ulingoni kama Robert Kennedy ambaye aliuwawa wakati mchakato wa uchaguzi wa ndani ukiendelea. Hivyo basi kwenye mkutano mkuu, ushindani huu uligeuka kuwa ugomvi na mapigano kati ya wafuasi wa McCarthy na kile kilichoonekana ni uongozi wa kimabavu wa chama. Polisi waliitwa kutuliza ghasia na badala yake ghasia ilizidi, na wanachama wengi walipigwa na kuumizwa napolisi. Humphrey alitangazwa mshindi ingawa ushindi wake ulikuwa wa mashaka kwa wanachama wengi. Na Humphrey alienda kugombea urais na hatimaye kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.
Je chama cha Democratic ilifanya nini? Ilimtimua Eugene McCarthy? Iliwatimua wafuasi wake? Hapana. Mara baada ya uchaguzi mkuu, uongozi wa Democratic party ulikaa na kuunda kamati iliyoongozwa na Senator George McGovern na baadaye Donald M Fraser. Na mabadiliko makubwa yalifanyika NDANI ya chama – ikiwa ni pamoja na kuwa na UWAZI mkubwa zaidi hususan katika chaguzi mbalimbali. Matokeo yake ni kuwa katika mikoa au states mbalimbali walianzisha mfumo wa primaries – yaani ngazi ya chini kabisa wanachama waliweza kupiga kura ya mgombea wanayemtaka. Si tu wagombea wa serikali za mitaa, bunge yaani Senate na House of Representatives, lakini hata za rais – presidential primaries. Kupitia njia hii ya wazi, chama cha Democratic ilijikuta kuwa hata kufikia 1984, mmarekani mweusi wa kwanza alitaka kuwa rais wa Marekani – Jesse Jackson – na alithubutu na kujaribu kutwaa ugombea rais wa chama ingawa hakufanikiwa. Hatimaye 2008, mmarekani mweusi Barack Obama alifanikiwa kuutwaa ugombea rais wa chama chake kama mwanasiasa mgeni asiye na uzoefu mkubwa – akimbwaga Hillary Clinton ambaye alikuwa ameshachukuliwa na viongozi wa chama kuwa ndo mgombea mteule. Kupitia mfumo huu wa uwazi, Obama na Hillary walichuana vikali sana kiasi kwamba wataalam wa masuala ya siasa wanasema Obama alipata mikikimikiki mingi zaidi katika uchaguzi wa ndani ya chama kuliko wakati wa uchaguzi mkuu. Mfano mzuri ni kashfa ya mchungaji wake Rev Wright ambayo iliibuliwa na kambi ya Hillary Clinton. Kambi ya Hillary pia iliandaa matangazo ya TV na radio ya kumbeza Obama kuwa akiamshwa usiku wa manane kuwa kuna janga limetokea atashindwa kutoa suluhu kwa sababu si mzoefu. Matangazo kama haya yalikuwa mengi kwa kambi zote mbili, ila Hillary Clinton alianza na pesa nyingi na sapoti ya viongozi wa chama. Lakini kama tunavyojua Obama alitumia mbinu ya kutafuta sapoti ya wanachama wapya – hususan vijana na wafanyakazi. Swali je Obama na timu yake wangekuwa Tanzania wangeruhusiwa kugombea?
Mfano huu wa Marekani utatusaidia vipi kuelewa hali ya sasa hivi? Chama chochote nchini si tu CHADEMA ni lazima iwe tayari kufanya yafuatayo ili iendelee kuimarika:
- Uwazi mkubwa katika uongozi wake – katika matumizi ya fedha na kadhalika
- Ushindani wa wazi katika kuwania uongozi na kuhakikisha kuwa uongozi uliopo madarakani inaweza kuwa challenged kwa uwazi
- Mfumo au utaratibu wa wazi wa kugombea nafasi za uongozi – primaries kwa ngazi zote
Lakini mi si mtaalam wa masuala ya siasa na ninaamini katika vyama vyote wataalam wapo wengi na wasomi wanaoweza kuja na reform ya chama chao ili kurudisha imani miongoni mwao.
Hivyo basi tunachokiona leo hii ndani ya CHADEMA ni changamoto kubwa lakini pia ni nafasi ya kipekee kwa chama hiki kikubwa cha upinzani kuandika historia. Kwani suluhu si kutimuana, “kuvuana nguo”, kuitana majina – hii itafanyika wakati wa mchakato rasmi – ila kwa sasa ni muda wa kujitafakari. Ni nafasi ya kipekee kwa chama hiki kukaa na kutafakari na kupokea ukosoaji wote wa pande zote na kisha kuzifanyia kazi. Huu si wakati wa kurudi kwenye dhana ya zamani ya kusema eti ushindani ni kitu kibaya. Wananchi wengi nilioongea nao na kuwasiliana nao wanaonyesha hofu na wamekata tamaa wakisema chama hiki kikubwa cha upinzani kikipasuka hakuta kuwa na ushindani wa vyama. Mi binafsi nasema mpaka sasa tamko la Zitto na la Kitila kuwa hawaondoki ndani ya chama na watabaki ni habari njema. Kwani mikwaruzano, na malumbano haya ndani ya chama kinaweza kuimarisha chama kama pande ZOTE zitaweza kutambua kuwa lengo lao kuu hatimaye ni kushika madaraka ya nchi. Na sisi wananchi tutambue kuwa katika ushindani huu hakuna malaika wala shetani, ni mgongano wa mawazo.
Hivyo basi katika ushindani huu ndani au nje ya chama – tujue kuwa ile principle ‘All is fair in love and war” – yaani kila kitu ruksa katika vita na mapenzi – hata hapa hutumika. Ninamaanisha kuwa ili kutwaa madaraka, pande zote zitapanga mikakati, zitajadili njia za kumdhoofisha mpinzani wake, zitatumia njia hata za kutuma ‘majasusi’ wa kisiasa kupata taarifa kuhusu pande wa pili, zitatoa taarifa za uongo za kuchafuana, zitatumia uzushi. Hii pia ni sawa kabisa na si kitu cha ajabu. Tusijidanganye, huu ni ushindani tena mkali. Upande utakaokataa kuwa haifanyi au haitumii mbinu hii utakuwa hausemi ukweli au utapotea bila kujielewa. Siasa ya vyama vingi ni ya ushindani na ushindani si lelemama. Kama kuna mtu anadhani Obama aliingia Ikulu ya Marekani kwa huruma, na kambi yake haikutumia mbinu na hila basi anajidanganya. Kama mtu anafikiri kuwa Magreth Thatcher aliongoza Uingereza kama waziri mkuu kwa sababu waingereza walimwonea huruma, wajue wamepotoka. Kama mtu anafikiri Tony Blair au David Cameron waliingia madarakani kutokana na ujana wao tu, wanahitaji kusoma zaidi historia. Viongozi wote hawa wameshika madaraka kutokana na kuwa walijiandaa mapema tena kwa SIRI, walikuwa na timu kali iliyowapangia mikakati yao ya ndani ya siri. Kuna wataalam wa mikakati yaani political strategists ambao wanafanya hii kazi kitaalam na huajiriwa na kambi za wagombea ili kuwaandikia mikakati. Hii si kitu cha ajabu na muda umefika hata sisi Tanzania tuwe tayari kuona ukweli kuwa pande zote husika katika siasa zetu, ndani na nje ya vyama vya siasa hutumia mbinu na hila. Kusema eti kambi fulani haiitumii mbinu na hila ni uongo, wako katika ushindani mkali wa kudhoofishana machoni mwa wanachama wao. Hivyo utasikia kambi moja inamwita mgombea mtarajiwa wa kambi nyingine “msaliti”, kambi nyingine inamwita mgombea mtarajiwa wa pande wa pili “mbadirifu”. Lakini lazima wakiri hatimaye kuwa wanachogombania ni madaraka. Angalau katika mkutano wao na waandishi wa habari, Zitto na Kitila wamekuwa wa kweli na kukiri hilo. Pande wa pili pia ifanye hivyo ili sasa ushindani wa wazi uanze. Lakini pia ikumbukwe kuwa katika harakati hizi chama kitakachokinzana na CHADEMA yaani CCM inatumia fursa hii kuwadhoofisha – na itaendeleza ushindani huu wa kutwaa uongozi wa ndani ya chama na kuukuza. Na hii pia ni sehemu ya ushindani wa kisiasa. Hatutakiwi kukataa au kujidanganya katika hili.
Kitu ambacho sikubali kabisa ni pale watu wanapojaribu kusema eti “hii ni Tanzania, hatuendi hivyo”. Mi naomba nijibu hiyo hoja – demokrasia na mfumo wa vyama vingi havikutungwa Tanzania. Kama tumekubali kutumia huo mfumo tufuate kama ilivyolengwa. Vinginevyo turudi kwenye uchifu. Tanzania tunaweza kujenga jamii ya kidemokrasia na itajengwa na SISI wananchi na si wanasiasa. Kwa sababu wanasiasa wako bize kutwaa madaraka - mwanasiasa yoyote yule – tusidanganyike! Hivyo basi sisi wananchi tukiwa kama wanachama wa vyama, kama wapiga kura, tuhakikishe tunakuwa mashabiki wa demokrasia na uwazi kwanza na si mashabiki wa vyama na wanasiasa. #ChangeTanzania
Posted by Maria Sarungi-Tsehai at 8:26 PM
Makala hii inapatikana katika blogu ya Dada Maria inayoitwa IN MY HUMBLE OPINION
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.