Na Walter Mguluchuma, Mpanda Katavi.
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Mkoa wa Katavi imemfikisha mahakamani mwenyekiti wa Baraza la Kata ya Kapalala Tarafa ya Nsimbo Wilaya ya Mlele Mkoani hapa Salvatory Mwanakatwe (63) kwa tuhuma za kuomba Rushwa ya ngono
Kwa mijibu wa mkuu wa Takukuru Mkoa wa Katavi John Minyenya mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo mnamo Agosti 11 mwaka juzi katika nyumba ya kulala wageni inayoitwa Mawenzi iliyoko katika mtaa wa mji mwema
Mtuhumiwa anadaiwa akiwa mwenyekiti wa Baraza la Kata alitumia wadhifa wake kutenda kosa la kumshawishi na kumwomba Rushwa ya ngono mwanamke mmoja ambae jina limehifadhiwa ili amsaidie katika shauri lake dhidi ya mumewe ambae alikuwa amemshitaki kwenye Baraza hilo kwa kumtelekeza na kisha kuuza mali walizochuma pamoja
Minyenya alieleza mbele ya waandishi wa habari kuwa mwanamke huyo baada ya kuombwa Rushwa hiyo ya ngono akuridhika na kitendo hicho cha kutoa rushwa ya ngono kwa mwenyekiti wa Baraza la Kata
Alisema ndipo alipofikisha taarifa kwenye Taasisi ya kupambana na Rushwa Mkoani Katavi kuhusiana na tuhuma za Salvatory Mwanakatwe kudai apewe Rushwa ya ngono na mwanamke huyo
TAKUKURU baada ya kupokea taarifa hizo ilianza kufanya uchunguzi juu ya rushwa hiyo ya ngono na iliweza kubaini kuwa tuhuma hizo zilizotolewa na mwanamke huyo ni za kweli
Alisema ndipo Maafisa wa TAKUKURU walipoandaa mtego wa Rushwa dhidi ya mshitakiwa Salvatory hapo mnamo Agosti 11 2011 na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Mawenzi Katika mtaa wa Mji Mwema akiwa na mwanamke huyo
Mshitakiwa amefikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la kuomba rushwa ya ngono ikiwa ni kinyume na kifungu cha sheria cha 25 cha sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11ya mwaka 2007
Mshitakiwa baada ya kusomewa mashitaka yanayomkabili dhidi yake alikana kutenda kosa hilo hata hivyo mtuhumiwa alikwenda rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana
Mkuu wa Takukuru wa Mkoa wa Katavi alieleza kuwa kesi hiyo imechelewa kufunguliwa kutokana na taratibu zilizopo sasa ambapo kesi zote zinazofunguliwa na Takukuru mahakamani lazima kibali kitoke kwa mwanasheria mkuu wa Serikali
Aidha TAKUKURU imetowa wito kwa wananchi wote kuzingatia maadili na kutojihusisha na vitendo vya Rushwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku wakati wanapodai haki zao kwani Rushwa ni adui wa haki hivyo Rushwa haikubaliki
HABARI NA KATAVI YETU
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.