RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali haitawabeba wawekezaji wa ndani katika ugawaji wa vitalu vya mafuta na gesi. Aidha, amesema mwekezaji wa ndani mwenye uwezo wa kufanya kazi hiyo ashindane pamoja na wawekezaji wa nje.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika uzinduzi wa awamu ya nne ya ugawaji wa vitalu katika kina kirefu kaskazini mwa ziwa Tanganyika iliyofanyika jijini Dar es Saam.
Hata hivyo, Kikwete alisema wawekezaji wa ndani wanaweza kununua hisa kupitia (TPDC) ambayo ni Serikali na sio kupitia sekta binafsi au mtu mmoja mmoja.
“Wazo la kuwatengea maeneo wazawa halipo, kwa sababu hakuna mwenye uhakika wa wapi hasa gesi inapatikana..... tunaweza kutenga eneo tukawapa wakachimba wakakosa wakalalamika tumepelekwa ambako hakuna kitu,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete alisema anatambua kuhusishwa kwa sekta binafsi katika suala hilo, lakini haipaswi kulaumiana au kuzungumza kwa ugomvi.
Akifafanua kwa watanzania, alisema kumekuwa na maneno na mabishano ambayo yanaonesha kuwa watanzania tutapata hasara wawekezaji wa nje kuingia katika uchimbaji wa mafuta na gesi na kwamba watakaonufaika ni wawekezaji wageni.
“Mkataba uliopo unafafanua utaratibu utakaotumika, wawekezaji watakaopata vitalu watapewa leseni, watagharamia uwekezaji wenyewe wataseti matetemeko kwenye maeneo wanayohisi yanafaa ili kuona hasa wapi pana matumaini .... wakishaona, wakichimba tu kisima kimoja gharama yake ni dola (Marekani) milioni 100,” alisema Kikwete.
Hata hivyo Kikwete alisema ni zaidi ya miaka mitano ndipo gesi itaanza kupatikana na watakapoanza kuuza ndipo watarudisha gharama zao na kwamba watanzania hatuwezi kuingia katika biashara ambayo ni hasara ukikosa.
Alisema hata watakapopata mgawanyo kati ya Serikali ikiwakilishwa na TPDC na wawekezaji hao ni aidha wao wachukue asilimia 25 na Serikali asilimia 75 au Serikali ichukue asilimia 35 na Serikali ichukue asilimia 65 ndipo hisa zitaanza kuuzwa kutoka TPDC.
Rais Kikwete aliwahakikishia watanzania kuwa hakuna hasara yoyote ambayo wataipata katika mchakato huo kulingana na utaratibu uliowekwa na Serikali na kwamba kama kuna mtu anasema kuna hasara ni aidha hajui au anapotosha watu.
Mwenyekiti wa Taasi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dk Reginald Mengi, juzi katika maonesho na mkutano wa sekta ya mafuta na gesi alihoji kuwa, serikali itawezaje kutoa vitalu vya gesi na mafuta, bila kuwa na sera.
Dk Mengi, alisema: Tanzania ni tajiri, gesi tuliyonayo ndiyo mtaji wenyewe tulionao na hivyo wazawa wawezeshwe na kwamba wageni kuja kuwekeza sio sahihi kwa sababu fedha zipo kwenye masoko ya fedha watanzania wanaweza kukopa.
Kwa hisani ya Habari leo.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.