Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA KUMI NA SABA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
RIWAYA: SITAISAHAU facebook MTUNZI: EMMY JOHN PEARSON SEHEMU YA KUMI NA SABA “Kwani mtu akifa anakuwaje?” aliniuliza, sikujibu. Akaendelea, ...

FACERIWAYA: SITAISAHAU facebook
MTUNZI: EMMY JOHN PEARSON
SEHEMU YA KUMI NA SABA
“Kwani mtu akifa anakuwaje?” aliniuliza, sikujibu.
Akaendelea, “hebu tuachane na hayo..msichana mdogo kama wewe ukifa sio vizuri ujue.”
“Kama ukiwa makini hautakufa. Tena wewe hautakufa, nitakusaidia usife sawa!!”
“Sawa!!” nilijibu kwa nidhamu kubwa.
“Njoo huku…”
Nikamfuata hadi mahali patulivu kabisa. Sasa hii ilikuwa ofisi kweli. R.I.P akanipokea. Akaniacha ofisini kwa muda, kisha akaingia tena baada ya dakika kadhaa.
Hakuwa yule tahira, hakuwa mchafum,chafu kama nilivyokueleza mwanzoni. Huyu alikuwa na hadhi ya yule mvulana ninayemuhitaji. Alikuwa mtanashati.
Hakuwa akicheka hovyo! Alikuwa makini na mtaratibu.
Roho Iliyo Potea (R.I.P). Alianza kwa kujitambulisha jina lake halisi. Kisha akaniupongeza sana kwa ujasiri wangu hadi kufika hapo.
Akajieleza kwa ufupi maisha yake ya utafutaji huku na kule hadi alipojikuta akitafuta kwa njia za mashetani. Ni katika maelezo haya alinieleza juu ya namba 666. Nilishangazwa sana na maelezo yake lakini nilipiga moyo konde nikiamini tiba ipo.
Baadaye akanieleza jinsi alivyojitoa katika harakati hizo za kumtumikia shetani. Haikuwa njia rahisi. Aliwapoteza ndugu zake kadhaa lakini mwisho akawa amejikomboa.
Hiyo chapa uliyopigwa lazima ifutwe! Ni njia hiyo tu ya kukukomboa kutoka ufalme huo.
Nilikuwa makini nikimsikiliza.!
USIKU MNENE
Safari ya kuelekea kuitoa ile alama ilikuwa imewadia. Pesa taslimu milioni moja ilikuwa imenitoka tayari ili kufanikisha jambo hili.
Tulitumia usafiri wa gari binafsi. Tulikuwa watatu. Mimi, RIP na mwenzake ambaye sikuwa namjua jina. Yeye alikuwa anaendesha gari.
Sasa gari ilisimama. Tukashuka garini. Nilikuwa nimevaa upande wa kanga kama RIP alivyoniagiza. Tulitembea kwa muda hadi tukakifikia kichaka. Hapakuwa na vibuyu wala dawa za kienyeji lakini tulikuwa mbele ta kaburi, hilo kaburi lilikuwa likimsubiri mtu limmeze. Yaani lilikuwa wazi.
Mara akachomoa kisu, akachomoa na kisahani.
Nikaamuriwa kuvua nguo!! Nikavua. Nikawa uchi mbele ya wanaume hawa wawili. Sikuwa na aibu!!
R.I.P akatoa sindano akavuta dawa. Akanigeuza, nikageuka.
Akanidunga sindano. Hii ya sasa ilipenya. Nikaisikilizia maumivu yake kisha taratibu nikasikia mguu wangu wa kulia unakufa ganzi.
Kisu kikatwaliwa upesi. Ilikuwa saa sita kasoro dakika sita. Hii ni kwa mujibu wa RIP.
Sikujua kinachoendelea lakini nilipotazama chini niliona kitu kama maji vile. Ghafla ikasikika sauti. Sauti ya kike ikiniita kwa mbali. Sauti ile ilikuwa inanisihi sana nikimbie.
Nikimbie kwenda wapi sasa.
RIP na mwenzake walikuwa wameshikilia kile kisahani. Sasa niliweza kuona kipande cha nyama. 666 zilionekana zikiwa katika mng’aro wa dhahabu.
Nikiwa sijajua lolote linaloendelea. Mara ghafla ile sauti sasa iliweza kusogea zaidi na zaidi.
Hatimaye aliyekuwa anaita kwa juhudi zile nikamuona. Alikuwa ni Maria, yule rafiki yangu tunayeishi naye. Alikuwa yu uchi wa mnyama. Alikuwa akikimbia kwa juhudi zote lakini hakuwa akikimbia bure kuna kitu ama mtu alikuwa anamfukuza.
Nikajaribu kupiga kelele. RIP na mwenzake hawakunisikia.
Maria alikuwa anakimbizwa na nyoka. Nyoka mkubwa alikuwa anang’ara sana. Nashangaa wenzangu hakumuona.
Nikajikuta natimua mbio uchi. Na nilikuwa kitendo cha sekunde chache yule nyoka akavamia eneo lile. Sikushuhudia sana kilichowatokea wenzangu. Sasa nikaanza kuhangaika huku na huko katika pori hilo ambalo sikuwa nalifahamu.
Mguu mmoja ukiwa umekufa ganzi. Ningeweza vipi kukimbia mbio ndefu. Isabela mimi nikaanguka chini. Sasa nikawa najivuta kama nyoka. Nalia kama mtoto. Sikuwa na uelewa bado kwa nini mguu wangu ulikufa ganzi. Lakini kumbukumbu za kuchomwa sindano ile kali zilikuwa kichwani mwangu.
Nikiwa bado sijapata jibu sahihi. Lile joka la maajabu sasa likatokeza mbele yangu. Mdomoni likiwa na kipande cha nyama. Nyama ile yenye namba 666.
Nikajiinamia kwa uchungu. Nikafanya dua fupi. Nikajilaani kwa kila hatua ya maisha yangu niliyopitia. Nikatamani ningekuwa na nguvu niweze kutimua mbio. Lakini tayari nilikuwa nimelegea. Macho yakazidi kuhesabu hatua za yule nyoka kunifikia. Sijawahi kuona nyoka mkubwa kama huyu!!! Nakufa kwa kumezwa na nyoka. Inauma sana!!
Joka likazidi kusogea!! Joka kuu likawa linatambaa!!!
Kabla joka halijanifikia. Lilibadilisha uelekeo. Ni kama kuna kitu lilikuwa limehisi. Likaanza kutambaa kuelekea upande mwingine.
Joka linatoka mara sasa namuona John. John yule mpenzi wangu ambaye alipotea katika mazingira ya kutatanisha pale chuoni.
“John…John!!” nilianza kumuita. Sauti ilikuwa imekauka. Haikutoka.
Joooooh!!! Nikajaribu tena, nikawa kama ninafanya mnong’ono. John akawa anaenda zake. Nikalia sana kuikosa nafasi hii hadimu ya kusikiwa na John!! Huenda angeweza kuwa msaada mkubwa kwangu.
Ubaridi ulipenya katika mwili wangu. Mwanzoni niliuhisi kuwa wa kawaida lakini baadaye nikahisi kama maumivu hivi. Nikajipapasa. Nilipoutazama mkono wangu ulikuwa na damu. Nikageuka kujitazama sehemu zangu za nyuma.
Maajabu!! Nilikuwa na kovu kubwa sana takoni!! Na palikuwa pamechimbika. He! Ina maana nilikatwa nyama yangu ya…..!! niliduwaa.
Maumivu yakazidi. Na sasa giza likazidi kuchukua nafasi yake baada ya mbalamwezi kutoweka. Giza nene!! Hapo bado nilikuwa sijaweza kunyanyuka imara. Nikajaribu kujikunjua nisimame. Maumivu makali katika makalio. Nikaanguka kama mzigo. Nilipoanguka palikuwa na kisu kipya, kikiwa na damu.
Nikaendelea kulia. Sauti haitoki.!! Nilikuwa katika jaribio kuu maishani.
Ikiwa bado sijaweza kusimama. Lile joka lililopotea njia sasa lilionekana tena. Safari hii lilikuwa linakuja kwangu tena.
Bora nife!! Nilijiapiza. Sasa nikaanza kutambaa kumfuata huyo nyoka. Mkononi nikiwa na kisu ambacho nilikiokota, bila shaka ni kile kilichotumika kunikata nyama.
Nikawa natambaa kama joka lile linavyotambaa. Sikuwa naijua nia yangu. Lakini nilihisi ni vyema kufa kuliko mateso haya.
Lile joka likazidi kunisogelea, macho yake makali yakiangaza huku na huko. Urefu wa joka lile la dhahabu likiwa na kipande cha nyama mdomoni ulinitia kwenye hofu. Nikajiuliza iwapo kisu changu kinaweza kupenya katika ngozi yake, nikajipuuza maana kisu changu kilikuwa kidogo sana. Nikasita kutambaa. Nikatulia tuli, huku nikiamini kuwa ni heri linimeze kistaarabu kuliko kunimeza likiwa na hasira baada ya mimi kujaribu kupambana nalo. Nikafumba macho nikakitupa kisu changu chini, nikajinyoosha tayari kwa kumezwa.
Haikuwa ndoto kwamba nikifumbua macho nikutane na mashuka yangu masafi ya kuvutia yakinibembeleza kulala badala yake nilipofumbua macho. Joka kuu hili hapa!!
Ubaridi wake ukapenyeza sasa, lilikuwa juu ya mwili wangu, pumzi zikawa zinaniishia. Ndio ninamezwa au? Nilijiuliza.
Nikaanza kugalagazwa kadri lilivyokuwa linajivuta. Sasa ile hamu ya kufa ikatoweka baada ya lile kovu langu makalioni kupatwa maumivu makali. Maumivu yaliyosimamisha misuli yangu. Nilipogeuka kujitazama nikakuta kuna mwiba umezama nikajivika ujasiri nikauchomoa. Sikuwa navutwa tena. Nilitazama mbele nikalishuhudia lile joka likienda zake.
Inamaana huyu nyoka hakuniona ama!! Nilitafakari. Nikashangaa.
Damu zilikuwa zikinitoka tena, sasa haikuwa katika kovu tu, bali na sehemu nyingine. Lile joka lilikuwa limenivuta hadi katika mti wa miiba na ni hapo nilipojitonesha.
Pori likatulia kimya, kimya kikawa kirefu sana. Nikawa nahisi kiu kikali. Lakini hapakuwa na maji. Usingizi ukanisaidia kuikwepa karaha hii. Nikasinzia.
Mwanga wa jua ndio ulionishtua. Nikakurupuka. Ni uchi!! Nikajishangaa kisha nikawahi kujiziba lakini bahati mbaya hakuwepo ambaye alikuwa ananichungulia. Nilikuwa peke yangu katika pori lile.
Hakuna mnyama, hakuna mmea ninaoufahamu, hakuna hata mdudu!! Lilikuwa pori la maajabu, pori la mateso makali kwa kiumbe hai.
Nilisimama wima, nikajisikia dhaifu sana lakini sikutakiwa kuendelea kuwa lelemama, nikiwa nachechemea nilianza kuzunguka huku na kule niangalie uwezekano wa kupata msaada. Harakati zangu sasa zikazaa matunda, kwa mbali nilimuona mtu akiwa analima. Alhamdulilah!!
Lilikuwa jambo maalumu kwa wakati maalumu. Nikajongea kwa kujikaza hadi nikalifikia lile shamba. Hakika mtu huyu alikuwa mchapakazi. Alikuwa peke yake na shamba lilikuwa kubwa sana.
“Kaka!!....Kaka…” Sauti ilitoka kwa taabu, nadhani hakuweza kunisikia.
Nikataka nimsogelee. Lakini ghafla akageuka. Ni kama aliuhisi uwepo wangu pale.
Japo alikuwa amechakaa sana. Nguo zikiwa zimeraruka, lakini niliweza kumtambua. Huyu mtu alikuwa ni marehemu. Zaidi ya kuwa marehemu, kifo chake niliwahi kukiota. Basu!!
Hakusema neno alipogeuka na wala hakunitazama, ni mimi niliyeiona alama ya 666 kifuani pake. He! Anamilikiwa!! Nilitafakari. Nikatimua mbio. Mbio za kuchecheme ziliniumiza lakini nitafanyaje??
Akili yangu ilikuwa sawa kabisa. Nilikuwa namkumbuka vyema Davis. Nilijuta kukutana na bwana huyu katika mtandao na kumuamini sana. Nilijutia na pesa alizokuwa akinipatia.
Mara nikaanguka!! Nilikuwa nimegongana na kitu kigumu. Ajabu na kweli haukuwa mti bali mtu. Jesca! Jesca na urembo wake alikuwa amebeba ndoo kubwa ya maji, alikuwa peku na alikuwa amepauka sana. Hata Jesca naye hakunitazama, badala yake aliendelea na safari zake huku akinipa nafasi ya kuitazama alama ya 666 katika mkono wake.
“Jesca!! Jesca!!” hakunijibu na dhani hakunisikia. Akatoweka.
Sasa sikukimbia tena, ina maana hawa watu hawanioni. Na kama
hawanioni hata lile joka halinioni. Nilijiuliza.
Kwani kuna kitu gani sifanani nao? Nilipojiuliza hivyo. Nikaikumbuka alama ya ‘666’ iliyokuwa imetolewa katika upande mmoja wa makalio yangu.
Alama hii ni ile ninayoijua ama kuna utofauti? Nilitafakari. Jesca huyo akawa ametoweka. Nilipoendelea mbele kidogo nikakutana na kile kisu nilichokitupa. Nikakitwaa. Nikazunguka huku na huko nikiwa uchi nikaipata ile kanga yangu, nikaivaa, wakati naivaa ndipo nilikumbuka juu ya watu wawili niliokuja nao huku katika kujisafisha na alama hiyo mbaya.
Nilipowakumbuka nikalikumbuka na kaburi lililokuwa wazi. Nikazungukazunguka na sasa nilikumbana nalo. Huenda walikuwa wamejichimbia kaburi hili. R.I.P na mwenzake walikuwa wamejizika huko.
Amakweli wewe ni Roho Iliyo Potea!!! Nilikiri kimoyomoyo baada ya kugundua kuwa sasa RIP amepotea kweli. Nilisikitika kuwa hakuwa amenieleza mambo mengi juu ya alama hizi za maajabu.
Jambo moja la muhimu alilonieleza ni kwamba nilikuwa namilikiwa. Kuna mtu alikuwa ananimiliki. Ili nisimilikiwe ilikuwa lazima alama hiyo ifutwe.
Sasa nilikuwa nimekatwa kipande cha nyama. Damu ya hedhi hainitoki tena na sihisi kichefuchefu cha mimba. Ina maana ndio similikiwi tena? Na mimba nayo imetoka. Nilishangaa.
Lakini sasa mbona siwezi kutoka humu porini? Nilijiuliza sikupata jawabu.
Mawazo yangu yalikatishwa na sura ya mtu mwingine aliyekatisha mbele yangu. Huyu alikuwa ni marehemu mwingine ambaye tulisoma chuo kimoja enzi za uhai wake.
Hivi niko peponi ama jehanamu? Kwa nini sasa nakutana na maiti tu.
Huyu naye hakuonekana kunifahamu. Alikuwa na alama yake sikioni. Nikakumbwa na moyo wa kujaribu. Kama mimi nimekatwa kipande cha nyama na alama imetoweka, nikaamua kujaribu kutumia mbinu ya RIP ambaye sasa ni marehemu.
Nikamnyatia yule binti. Nikakiweka kisu changu tayari nikamkaba. Bila kukumbuka maumivu atakayoyapata nikafyeka sikio lake. Nikasisimuka lakini katika nafsi nikikiri kuwa kile kisu kilikuwa kikali sana. Sikio chini!! Yule binti naye chini, akawa anatoa kilio kikubwa sana. Kitu cha ajabu hakuna msaada alioupata. Mimi nikajiweka mbali niweze kuwa shahidi wa nini kitakachotokea.
Mara upepo mkali ukaanza kuvuma. Miti ikayumba, pori likatulia na sasa alitokeza nyoka mkubwa, ni yule yule wa awali. Nikataka kukimbia, nikakosa ujasiri nikaendelea kujificha, joka lile likatambaa hadi katika ule mwili unaogalagala, kisha likakwapua lile sikio na kisha kuanza kuzurura huku na huko hadi lilipotoweka ndipo nilipomsogelea yule binti. Alikuwa ametulia tuli na damu haikuwa ikivuja sana.
Nikamgusa. Akajigeuza, akanitazama. Mungu wangu!! Tiba inafanya kazi ile. Aliniita jina langu. Akakaa kitako.
Sikuwa nikiamini lakini sasa nikampongeza RIP yule tahira niliyemdharau sasa alikuwa njia.
“Na wewe umejiua?”
“Nimejiua?” nilimuuliza.
“Isabela kwa nini uliniua?” alinihoji. Nikashangaa.
“Mimi nilikuua wewe.”
Yule binti alinieleza kila kitu, akanisimulia alivyouwawa akiwa ndotoni. Akakiri kuniona mimi nikimmaliza huku ninacheka. Akanielezea juu ya sauti alizozisikia. Ni sauti zile zile na mimi nilizisikia katika kifo chake na pia katika mazishi ya yake, hata Jesca alipokufa zilisikika.
Niliamini tena kauli ya RIP kuwa kuna mtu ananimiliki na ananifanya anavyotaka yeye kwa wakati wake. Huyu mtu ni nani? Nilijiuliza huku tuhuma za kwanza nikizitupia kwa Dokta Davis.
******
(OPARESHENI UKOMBOZI)
Jenipher alinieleza mambo mengi huku akinisaidia kupata chakula na maji. Chakula kilikuwa kizuri na maji yalikuwa safi lakini namna ya kuvipata ilikuwa ya namna yake. Wakati huo na yeye hakuweza kuonekana.
Chakula na maji pekee havikuwa vitu tulivyokuwa tukihitaji. Kikubwa tuliuhitaji ukombozi wetu na wanadamu wengine wanaomilikiwa na watu wabaya.
Sasa ilikuwa ni lazima kuuvaa moyo wa ujasiri ili kufanya harakati za ukombozi. Tuliwahitaji wanaume wenye nguvu waweze kuungana nasi.
Basu akawa chaguo la kwanza! Tulimtegea siku akiwa katika kulima shamba kubwa lisilotoa mazao.
Tulifanikiwa kumpata kwa wakati. Huku tukiwa tunajiamini kabisa. Tulimvaa kwa nguvu akaanguka chini huku akiwa haoni lolote. Anaangaza kushoto na kulia. Nikachomoa kisu.
Alama ipo kifuani!! Huu sasa ukawa mtihani. Nichome au nisichome..nikimchoma maana yake ninamuua. Nikabaki kujiuliza.
Hali hiyo ya kujiuliza, ikapoteza sekunde kadhaa. Ni katika sekunde hizo, nilimshuhudia Jenipher akirushwa mbali kisha nikamwona nyoka akimshambulia. Nikajitoa katika mwili wa Basu nikiwa na kisu changu nimesimama wima. Nilimshuhudia Jenny anavyohangaika. Na nyoka yule alikuwa ni mdogo sana. Nikajitoa muhanga.
Bila kusita mbio mbio. Kisu mkononi huku nikipiga kelele nikamfikia yule nyoka nikamfyeka. Akagawanyika vipande viwili.
Jenny akasimama. Hakuwa amejeruhiwa. Tukatoweka mahali hapo. Tukamwacha Basu akiwa katika taharuki asijue nini kimetokea.
Hatukuwa tumezungumza lolote. Hadi pale tulipokutana na mwanaume mwingine. Huyu alikuwa ametoka kukata kuni. Tulimpisha njia kisha tukamfata kwa nyuma tukamvamia, akapiga mweleka. Alipojaribu kurusharusha miguu. Alama ile chafu ikaonekana katika paja lake. Bila kujiuliza Isabela mimi nikafanya kama nachuna mbuzi. Nikaikata nyama ya paja lake. Mwanaume huyu akalia kama mtoto.
Nilipoiondoa nikaitupia mbali. Baada ya muda akatokea yule nyoka akakichukua kile kipande.
Sasa tukazidi kufunguka akili kuwa yule nyoka anawaona watu wenye alama. Na yawezekana ni nyoka huyu yupo katika kuwamiliki wanadamu kwa chapa yake ya hatari.
Swali kuu likabaki. Tunatoka vipi katika pori hilo.
Mwanaume yule hakuzimia, alikuwa na timamu zake. Tukamweleza kwa kifupi naye akajieleza kuwa, tamaa ya utajiri imemtupia katika shimo hili baya.
Yule mwanaume alijitambulisha kwa jina la Samson alikumbuka vyema kuwa kabla ya kufika hapo alikuwa mkazi wa jijini Mwanza na alikuwa mwanafunzi katika chuo cha biashara (CBE) tawi dogo la jijini Mwanza.
Huyu alikuwa Samson kweli maana alikuwa ni mbabe sana. Lile kovu lake la kwenye paja halikumsumbua. Tulitembea kidogo akachuma majani fulani akayasagasaga akayaweka katika lile kovu. Hapa sasa aligumia kwa maumivu. Bila shaka ile dawa ilikuwa kali sana.
Akaniwekea na mimi katika kovu langu. Nikapiga mayowe. Akanikamata imara. Hadi maumivu yalipotulia kidogo. Jenipher hakutaka kovu lake la sikioni liguswe aliweza kuyakadiria maumivu makali ya dawa ile.
Siku mbili zilipita. Kovu lilikuwa linakauka kwa kasi. Nilimshangaa kijana huyu.
Siku hiyo ya pili harakati za kujikomboa zilianza rasmi. Jeshi letu bado lilikuwa dogo. Tulihitaji jeshi kubwa zaidi.
JESHI katika pori tusilolifahamu!!

OPARESHENI UKOMBOZI….ukombozi dhidi ya 666…..harakati n’do kwanza zimeanza……NINI KITAJIRI katika pori la maajabu???

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top