Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA KUMI NA NNE
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SITAISAHAU facebook MTUNZI: Emmy John P. MAWASILIANO: 0654 960040 SEHEMU YA KUMI NA NNE Maria, Maria njoo!! Nilimuita wakati huo tayari niki...

clip_image002SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040
SEHEMU YA KUMI NA NNE
Maria, Maria njoo!! Nilimuita wakati huo tayari nikiwa sebuleni.
Maria kwa hofu akanifuata. Nikamkumbatia. Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana. Lakini yangu yalikuwa juu zaidi. Kila mmoja alikuwa katika kuogopa.
Sikuweza kuzungumza chochote. Nikamvuta Maria tukaelekea chumbani. Nia yangu kumueleza kila kitu kilichonisibu hadi nikatimua mbio. Tulifika chumbani, ajabu Maria alikuwa anatetemeka kuliko mimi muhusika.
Tulitulia kitandani, nikaisogeza laptop nikaanza kumuelekeza Maria, kile nilichokiona. Hasahasa picha ya yule mganga. Lakini sikumweleza lolote juu ya mimi kumfahamu.
“Jamani Bela…wame’HACK’ akaunti yako..mbona haka kamchezo ka kawaida tu!.” Alinieleza.
Ni kweli jambo hilo nilikuwa nalifahamu. Lakini huyu mganga amejuaje kuwa mimi naitwa Isabela hapa facebook? Nilijiuliza.
Ok! Kama ni kweli ameingilia akaunti yangu na kunidhalilisha hivi. Naapa atakiona cha mtemakuni. Nilimuapia Maria. Wakati huo sikumbuki kuwa palikuwa pia na picha ya John.
****
Sikuwa katika utani. Nilikuwa nimekerwa na kitendo cha yule mganga kunifanyia huu upumbavu. Kesho yake pesa ikaongea nikawapa pesa nzuri maaskari. Nikawapa na ushahidi. Ndani ya Defender kwenda kumkamata yule mganga. Lile jaribio la kutaka kunibaka lilikuwa moja kati ya mambo yaliyonitia hasira.
Niliikumbuka vyema njia na tulifika bila usumbufu.
“Mzee alitutoka. Ni wiki sasa imekatika.” Mke wa mganga alitueleza kwa huzuni kuu. Moyo ukawa wa moto ghafla. Mganga amekufa!! Mbona tarehe ya ile picha na kifo cha huyu mganga vinashangaza sasa. Tarehe aliyoweka ile picha tayari alikuwa marehemu.
Ewe! Mwenyezi Mungu nichukue mimi Isabela, dunia imenishinda!!! Nilisali kimoyomoyo. Mauzauza yalikuwa yamenizidi nguvu.
Nilirejea nyumbani nikiwa mwingi wa mawazo. Sikumueleza lolote Maria. Nilimpita akiwa anajisomea. Zaidi ya salamu sikusema neno. Moja kwa moja chumbani nikajinyoosha kitandani nikaanza kulia.
Nikiwa bado sijasinzia vizuri. Simu yangu iliita. Alikuwa ni rafiki yake na John.
Kidogo nisipokee. Lakini alipopiga tena na tena nikaamua kupokea.
“Mambo vipi shemu?”
“Poa!” nilimjibu kwa kujilazimisha.
“Sijakuelewa kabisa shem! Una matatizo gani?” aliniuliza.
“Kwa nini mbona niko poa sema nimechoka tu.”
“Umechoka ndo unaandika mambo gani sasa haya kwenye facebook?” alizungumza kwa hasira kidogo. Nikakaa kitako, usingizi hakuna tena!!!
“Nimeandika nini kwani eeh!! Hebu ngoja.” Nikamkatia simu.
Haraka haraka nikafungua simu yangu sehemu ya mtandao. Jasho lilikuwa linanitiririka. Sijui ni kipi kilikuwa kimeandikwa. Na ni nani ameandika kama ambaye ameiingilia akaunti yangu tayari alikuwa ni marehemu.
“1986-2012..REST IN PEACE ISABELLA” Ilisomeka hivyo katika akaunti yangu.
Karibia kila mtu alikuwa anauliza kulikoni nimeandika hivyo.
Lakini bora ningekuwa nimeandika mimi! Mimi hata sijaandika. Nikaanza kulia nikajigalagaza kitandani, nikavua nguo zangu. Nikavuruga nywele zangu. Nikalia kama mtoto.
“Nimekukosea nini Mungu wangu eeeh!! Nimekosa nini sasa!!” nililaumu sana, uchungu ukanikaba kooni. Ukasafiri hadi moyoni, ukanisurubu kila upande. Suluba nisiyoelewa chanzo chake. Suluba kamilifu.
Naelekea kuchnganyikiwa? Nilijiuliza. Lakini nikajicheka. Tangu lini mwendawazimu anautambua wazimu wake? Huenda mimi ni kichaa tayari.
Munkari ya kusoma ikapotea na mitihani ilikuwa karibu kabisa.
Liwalo na liwe!!
Nilitamani sasa kwenda kwa viongozi wa kiroho waweze kunishauri na kuniombea kama inawezekana lakini tatizo lilikuwa katika kuwaeleza kuanzia mwanzo. Zile ndoto za John anaua na mengine yote. Niliogopa kuaibika.
Nikakaa kimya na siri yangu, mateso pia yakabaki kuwa yangu!!!
Nilipowaza mitihani, wazo la kuwa nina mimba pia likajileta pia katika orodha.
(SHARTI GUMU!!)
Ule ujumbe ulioonekana katika akaunti yangu, ulinishtua sana. Sasa sikuwa na ujanja tena nikafikia hatua ya kukubali kuwa yamenishinda na ninatakiwa kumshirikisha mtu mzigo huu.
Kitu cha kwanza niliiondoa akaunti yangu ya facebook katika matumizi ‘deactivation’. Sikuhitaji tena kuwa katika mtandao huo. Baada ya hatua hiyo nikaandika barua ya kuomba ruhusa ya kutofanya mitihani hiyo iliyokuwa mbele yangu pale chuoni.
Kwa kuwa nilikuwa nafahamika sikupata usumbufu nikapewa ruhusa hiyo upesi. Nikaamua kufunga safari kuelekea nyumbani. Lengo kuu likiwa kumueleza mama kila kitu kilichonitokea na kutishia uhai wangu. Sikuwa na ujanja mwingine.
Usiku nilikuwa nimetingwa katika kujiandaa. Ni Maria pekee ambaye nilimueleza kuwa nitasafiri, na wakati huo alikuwa akinisaidia kufungasha mabegi yangu. Tayari kwa siku inayofuata.
Ilikuwa saa sita kasoro dakika kadhaa. Nilitulia nikamtazama Maria na yeye akanitazama mimi. Kisha kila mmoja akageuka na kutilia maanani kile kinachosikika. Mlango ulikuwa unagongwa.
Hakika ni palepale katika nyumba yangu niliyokuwa naishi.
Nani huyu muda huu? Nilimuuliza Maria kana kwamba yeye alikuwa anamfahamu aliyepo mlangoni. Maria hakuwa na cha kunijibu.
Nikiwa nimemshika mkono Maria tuliufikia malango, tukaulizia ni nani? Hakujibu. Tukauliza tena!! Kimyaa!!
Kila mmoja akamshikia mwenzake kwa nguvu sana!!
Ghafla mlango ukabamizwa kwa nguvu sana.
Mungu wangu!! Watakuwa majambazi! Nilihisi.
Kabla sijajua nini cha kufanya, mlango ulisukumwa bila kutoa kelele ukafunguka. Waaa!!
Ghafla pakawa giza. Nikasukumwa kando na mikono ya baridi sana. Nikajaribu kupiga kelele sauti haikutoka. Nikajaribu tena sikuweza kabisa. Kisha nikasikia mlio mkubwa. Kisha kama gunia la mahindi kitu kikatua chini huku kikipiga kelele. Ilikuwa sauti ya Maria.
Kama vile haitoshi nikashikwa tena na yule mtu mwenye mikono ya baridi. Akaanza kuniburuza. Moja kwa moja hadi chumbani kwangu.
Akaninyanyua akanitupa kitandani.
Nikajaribu tena kupiga kelele sauti haikutoka.
Mara taa ikawashwa!! Chumba kikang’ara.
Ana kwa ana na mtu ninayemfahamu!!
Ni yule niliyemuandikia barua ya kuomba kuacha kazi!!
Dokta Davis mbele yangu!!
Dokta wa maajabu.
Alikuwa amevalia suti nyeupe. Na hakuwa akitabasamu!!
Nikajaribu kuzungumza, sikuweza!! Akacheka, nikamsikia.
“Isabela……” aliponiita, nikajaribu kuitika sauti ikatoka.
Maajabu haya!!
“Milioni thelathini, mama yako mzazi, ama wewe!” alinieleza kwa utaratibu.
Sikumuelewa. Nadhani hata yeye aliitambua hali hiyo.
“Ni hivi..hadi sasa umetumia shilingi hizo…sasa unatakiwa kabla sijaweka saini yangu katika barua yako kuhalalisha wewe kuacha kazi nahitaji ufanye maamuzi. Nakupa wiki moja tu!! Uwe umerejesha pesa hizo, ama mama yako akae mbali nawe maisha yako yote na mwisho ni uchaguzi ujitoe wewe kwa usiku mmoja!!”
“Usiku mmoja?” nilijiuliza. Ikawa tena kama ananisikia.
“Usiku mmoja wewe na mimi na kisha nitakuacha huru na uamuzi wako wa kuamua kuacha kazi. Ole wako umueleze mtu…nitachukua maamuzi ambayo hautaamini”
Sikuamini kama maneno hayo yanatoka kinywani mwa mtu huyu. Na ameweza vipi kufika Tanzania bila kunieleza. Mbaya zaidi amekuja nyumbani kwangu usiku mnene.
Kabla sijamjibu lolote. Alizima taa. Kisha nikasikia mlango unafungwa. Nikaendelea kutulia kama nilivyo huku naogopa.
Nilidhani yupo jirani na eneo lile. Sikuthubutu kusimama. Baada ya dakika kadhaa nikasikia hatua zikijongea kuja katika mlango wa chumba changu.
Anarudi! Niliwaza nikaendelea kutulia. Jasho likilowanisha shuka zangu.
Taa ikawashwa. Kwa ncha za macho nikamtazama aliyepo mbele yangu. Alikuwa ni Maria. Uso wake ukiwa umevimba.
“Bela…nimeanguka mwenzako.” Alianza kunieleza. Nikageuka kumtazama huku nikipatwa na hisia za kumwogopa.
“Mh!! Mbona hivyo Bela. Kimekusibu nini?” aliniuliza.
Sikuwa na cha kumjibu. Nilibaki kushangaa. Maana niliamini na yeye amemuona dokta Davis lakini hakuonekana kujua lolote.
Nilitamani sana kumueleza lakini hofu ya onyo la Dokta ilinitawala. Maria akanisogelea akanikumbatia. Nikahesabu alama kadhaa za vidole katika shavu lake. Huenda kabla ya kuanguka alipigwa kofi.
Siku iliyofuata nilitakiwa kusafiri. Maria aliwahi sana kuniamsha lakini sikuwa na uwezo tena wa kusafiri. Onyo la Davis kuwa iwapo nitamwambia mtu yeyote atafanya anachojua.
Niliunda sababu kadhaa nikafanikiwa kumshawishi Maria kuachana na safari hiyo. Alishangaa lakini hakuwa na jinsi maana msafiri nilikuwa ni mimi.
Siku ya pili hiyo zikasalia siku tano Dokta afanye yake aliyoyaahidi.
Bado sikuwa nimepata jibu sahihi la kumpa. Milioni alizonitajia kwa kweli sikuwa nazo hata nusu yake. Kumuondoa mama yangu katika uso wa dunia ni jambo ambalo sikutaka kulisikia.
Kulala na mimi usiku mzima. Lilikuwa ni sawa na tukio la kubakwa kwa hiari. Udhalilishaji!!
Nikajilaani kumuamini sana Davis. Majuto yakaninyanyasa.
Bila kumuaga Maria, niliamua kutoweka pale nyumbani kwangu na kwenda kupanga katika nyumba ya kulala wageni. Maeneo ya Igoma.
Nilizima simu yangu! Siku zikazidi kukatika na sasa ilikuwa imesalia siku moja ya mimi kutamka jibu langu.
Nikaiwasha simu yangu!! Nikaitafuta namba ya Davis. Nikafungua sehemu ya ujumbe nikamtumia.
USIKU MMOJA MIMI NA WEWE. Nitakueleza wapi nipo uje!!
Ujumbe ukapokelewa! Lakini haukujibiwa!!
****
Siku ya tukio ikafika!! Nilikuwa najaribu kumpigia simu Dokta huyu wa maajabu nimuelekeze wapi nipo lakini simu yake haikuwa inapatikana. Nilijaribu tena na tena bado hali ilikuwa ileile.
Hofu ikanitawala! Huenda Davis ameamua kufanya anachojua yeye. Vipi kama ameamua kumtokomeza mama yangu!! Nilianza kulia baada ya kufikiria hayo.
Nikiwa katika kulia simu ya chumbani ilianza kuita.
Nikaitazama kisha nikaipokea.
“Kuna mgeni wako..”
“Mgeni?”
“Anaitwa Davis.” Sauti ya muhudumu ilinijibu.
Kulisikia jina hilo tu. Nikakurupuka kutoka kitandani bila kujua ni wapi ninakimbilia. Nilikuwa naogopa sana jambo ambalo lilikuwa linakuja mbele yangu. Kufanya mapenzi bila hiari na kiumbe cha ajabu sana.
Haya yote niliyataka mwenyewe!! Sasa nikaanza kuhisi kuwa Davis hakuwa mtu mzuri kwangu!!
Davis ni MCHAWI!!!
Naenda kufanya mapenzi na mchawi!!
Ghafla nikaijiwa na kumbukumbuku za chapa ya shetani 666, niulipokumbuka hili nikakumbuka na mshahara wangu ulikuwa una hizi namba, hata simu ya Osmani nayo ina 666, Davis aliwahi kunitumia nauli nayo ilikuwa na 666 na sasa nipo katika chumba namba 66 namsubiri huyu mfalme wa 666
Hapana! Hapana! Niliipinga nafsi yangu. Na sasa nilikuwa nimeamua kumkimbia mchawi huyu. Kuikimbia chapa ya shetani!!!
Nikawa najiandaa kukimbia
Nilipokishika kitasa ili kuufungua nitoke nikakumbwa na kihoro! Mlango ukafunguka kama vile ulikuwa katika kungojea amri yangu!!
Niliamini kabisa si muhudumu anayeweza kuingia katika chumba cha mteja bila ruhusa. Kwa hiyo kama sio muhudumu basi angekuwa Dokta.
Hakika. Alikuwa ni yeye! Nikatazamana naye ana kwa ana, akapiga hatua mbili akawa ameingia vyema ndani ya chumba. Akaufunga mlango.
Alitaka kuongea jambo lakini mlango ukagongwa tena, akasita kisha akaufungua! Alikuwa muhudumu.
"Barcadi, na Sprite!" aliagiza Davis bila kutoa malipo ya awali. Vinywaji alivyoagiza nilijua fika ni kwa ajili yangu na yeye!
Mlango ukafungwa tena.
Sasa aliufunga na funguo kisha akaziacha pale mlangoni zikining'inia.
Mimi nilikuwa wima mkoba begani nikitetemeka.
Davis akaliendea kochi kubwa hapo chumbani akaketi. Kisha kwa ishara akaniita!
Naitwa na shetani! Nilihamaki. Nikasita kwenda.
"Hautaki?" aliuliza, sikumjibu!. Akaitwaa simu yake kubwa ya kisasa.
"Tabasamu kidogo nikupige picha Bela?" alinishawishi. Sikushawishika.
Alipochoka kunichekesha nisiyecheka akatoweka na kwenda bafuni. Nikabaki chumbani peke yangu! Hapo likanivamia ghafla wazo la kutoroka! Funguo zilikuwa mlangoni! Kwanini nisikimbie? Nilijiuliza. Hapo sasa ndipo nikagundua kwanini sina ubavu wa kukimbia. Huyu bwana alikuwa anahodhi maisha ya mama yangu! Mwalimu Nchimbi.
Nilipotambua hilo nikafadhaika. Nikakiendea kitanda nikajitupa, nikautupa na mkoba wangu!
Ilikuwa lazima nifanye mapenzi na Davis ili kuokoa maisha yake.
Nilifadhaika bila kujua nini la kufanya. Mlango wa maliwatoni ukafunguliwa. Kichwa kilikuwa kizito hata kunyanyuka kushuhudia ni kimbwanga gani kipya atakizua Dokta huyu!
Akajikoholesha kama anayerekebisha koo. Nikaijua nia yake! Nikanyanyua kidogo! Macho wazi!! Yowe la uoga likanitoka kwa nilichokiona.
Hili lilikuwa kubwa kupita yote!
Kilichokuwa mbele yangu ni kiumbe kile kile kinachoitwa Davis.
Lakini sasa hakuwa na nguo. Maungo yake yote yakawa yananidhihaki, japo alikuwa mweusi tii. Lakini ule mwanga pale ndani uliniwezesha kutambua kuwa alikuwa amelowana damu katika viungo vyake vya uzazi, na hiyo damu ilikuwa mbichi na ni kama ilikuwa inaendelea kumtoka lakini ajabu haikuwa inadondoka katika marumaru!
Hapa sasa nilimsahau kwa muda mwalimu Nchimbi, nikauacha mkoba nikakimbilia mlangoni.
Ajabu! Ule funguo haukuwepo tena mahala pake! Dokta akacheka sana huku akinifuata kwa hatua ndogo ndogo!
Nilitegemea huenda nitapoteza fahamu. Lakini hiyo haikutokea niliendelea kushuhudia kiumbe huyu akinifuata.

**UTATA….ISABELA amekubaliana na sharti ambalo kwake lina wepesi kiasi……sharti la kulala na dokta Davis kwa usiku mmoja ili kukubaliwa azma yake ya kusitisha mkataba wake……
Usiku huu unakuwa wa maajabu zaidi…..dokta DAVIS akiwa uchi wa mnyama

…..ISABELA anashuhudia sehemu zake za siri zikiwa zimetapakaa damu, damu mbichi kabisa…..anataka kukimbia…haukuti ufunguo mlangoni…..kiumbe kile cha ajabu kinamsogelea……
Nini kitajiri….UTATAAA!!
ITAENDELEA
NB: Kama unahitaji kuipata riwaya hii mwanzo hadi mwisho…inapatikana kwa shilingi 3000..wasiliana na mtunzi

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top