RIWAYA: SITAISAHAU FACEBOOK SEHEMU YA SITA

clip_image001SITAISAHAU facebook
MTUNZI: Emmy John P.
MAWASILIANO: 0654 960040

SEHEMU YA SITAWiki mbili zilikatika tangu Jesca aache simanzi kubwa katika chuo cha Mtakatifu Agustino. Nilikuwa karibu sana na John nikimfariji kwa kumpoteza mpenzi wake. John kwa kiasi kikubwa sana alifurahia ukaribu wangu kwake. Kiasi kikubwa upweke ukawa unatoweka.
USIKU WA MANANEKila kona ya jijini Mwanza ilikuwa imetulia, upepo ulikuwa unavuma kiasi cha kuyumbisha miti midogomidogo iliyoota pembezoni mwa barabara. Magari machache yalikuwa yakiipa usumbufu barabara ya lami ambayo ilikuwa katika mapumziko baada ya suluba ya mchana.
Gari dogo aina ya Corolla ilipata hitirafu ambayo ilionekana kuwasumbua vichwa abiria waliokuwa ndani yake. Kila mmoja alionekana kumsukumia mwenzake mzigo wa kutafuta suluhu ya ya gari hilo. Wale abiria
watatu wote walikuwa wanafunzi wa chuo cha mtakatifu Augustino.
Baada ya muda wa kujadiliana hatimaye mwanafunzi mmoja aliyetambulika kwa jina la Joseph alivua shati lake akaweka pembeni akaingia katika ufundi. Wenzake wawili walitulia wakimtazama.
Baada ya dakika kadhaa mwanafunzi mmoja alibanwa haja ndogo. Taratibu akajivuta kichakani. Sijui kwanini aliamua kukitafuta kichaka cha mbali wakati usiku ulikuwa mnene na hapakuwa na watu wakipita hovyo. Alikifikia kichaka taratibu akaanza kuifungua zipu yake tayari kwa kukidhi haja yake ya wakati huo.
Ghafla aliiachia suruali yake na kutazama mbele katika namna ya kukodoa huku akiwa na hofu kuu. Alikuwa akitetemeka huku akifanya namna ya kushtua kama anatisha kitu kibaya kinachomkabili. Nilitamani sana kujua ni nini hicho mbele yake lakini nikaendelea kuwa mtazamaji wa filamu hiyo ya ajabu.
Kisha kama aliyesukumwa akaanguka chini. Akawa anajaribu kupambana kwa kujirusha huku na huko. Alikanyagakanyaga lakini hakufua dafu. Alirusha mikono hewani, bado alionekana kukabwa ipasavyo.
Ghafla nikajiona kuwa mtu wa ajabu sana, kwa nini nashuhudia jambo hili na sitoi msaada wowote. Nikataka kupiga kelele. Lakini koo lilikuwa limekauka.
Kwanza ni filamu!! Nilijiambia tena.
Mara yule kijana akatulia tuli. Nami hapo nikashtuka!!!!
Ndoto!! Ndoto mbaya.
Nilikuwa nimeung’ata kwa meno upande wa kitanda. Nilikuwa natokwa jasho na nilikuwa naunguruma kama mbwa mwenye ghadhabu anayejiandaa kubweka.
Nilihisi kama maumivu kwa mbali katika bega langu.
Taharuki!! Kamwe sijawahi kuota ndoto kama hii!! Mbaya sana.
Nilitazama saa ilikuwa saa tisa usiku. Giza nene nikiwa peke yangu kitandani.
Nilisimama nikafanya ishara ya msalaba. Nilikuwa natetemeka. Na nilivyokuwa muoga wa filamu za kutisha, basi nilikuwa sikamatiki kwa hofu.
Nilikuwa nimebanwa na mkojo lakini nilipaogopa sana chooni. Nikaamua kurejea kitandani. Mkojo ukazidi kunibana. Sasa nikajiona kuwa bwege, nina choo ndani halafu naogopa kukitumia.
Ni ujinga kujikojolea kitandani wakati kuna choo ndani ya nyumba!!!
Nikauweka uoga kando nikaenda bafuni. Nikachuchumaa niweze kukojoa, nikahisi maumivu kiunoni.
Mh!! Nimelala vibaya ama!! Nilijiuliza huku nikijilazimisha kuchuchumaa.
Nilipochuchumaa ndipo nikagundua kuwa nanukia marashi yasiyokuwa ndani ya chumba changu. Hilo pia nikalipuuzia.
Nikamaliza haja zangu nikarejea kitandani. Nikajidhihaki kwa hofu ya kijinga niliyoiruhusu initawale.
Usingizi ukanipitia. Sikuota tena!!!!
Asubuhi majira ya saa mbili nikashtuka usingizini. Ilikuwa siku ya jumamosi, nikaamka kuwahi saluni kutengeneza nywele.
Kabla ya kufika saluni nilipita hotelini nikapata stafutahi.
****
Niliwakuta wateja wawili tu hapo saluni, hivyo mahesabu yangu yalikuwa sawa, sikuwa nimechelewa sana.
Nilisubiri kidogo zamu yangu ikafika. Baada ya mimi kuanza kuhudumiwa walimiminika wateja wa kutosha. Kila mmoja na haja yake.
Saluni huwa ni eneo zuri sana kwa wale wabahili wa kununua magazeti ya udaku, kujipatia habari nyingi burebure tena kwa uhakika kwa sababu hata nafasi ya kuuliza maswali huwa inapatikana.
Penye wengi pana mengi. Na sasa tulikuwa wengi pale saluni. Mara kimya kikatawala alipoingia mwanamke mnene. Sikuwa namjua jina lakini haikuwa mara ya kwanza kumwona.
Baada ya kimya hicho ambacho uswahilini kinaitwa ‘jini kapita’ wote tulilipuka na vicheko.
Hata yule mama mnene na yeye alilipuka kwa kicheko kikubwa. Kisha tena akauvaa uso wake wa awali.
“Mnacheka wakati watu tuna msiba” Alikoroma, nusu akimaanisha na nusu ukionekana dhahiri kuwa ni utani.
Wengine wakacheka na wengine wakakaa kumsikiliza.
“Halafu mjue sitanii jamani.” Alikazia kisha akaendelea, “Basu ametutoka.”
“Basu? Basu ndio nani?.” Mwanamke moja aliuliza.
Nami nikapatwa na kihoro cha kuuliza. Nikajizuia lakini sikuweza.
“Basu huyu wa BBA (Bachelor of Business Administration).” Niliuliza.
Mama yule mnene kumbe na yeye alikuwa mwanafunzi. Akaiunga mkono kauli yangu. Kwa kueleza kuwa ni mwanadarasa mwenzake.
Basu alikuwa amekufa!!!
Nini kimemuua jamani, si juzi tu alikuwa anacheza mpira kwenye haya mashindano ya FAWASCO? Niliuliza.
Msomaji mashindano ya FAWASCO ni mashindano ya michezo mbalimbali huwa yanafanyika chuoni SAUT. Na katika mashindano haya watu wengi walitokea kumfahamu Basu kutokana na umahiri wake uwanjani.
Yule mama mnene akashusha pumzi kabla ya kujibu kwa sauti ya kunong’oneza.
“Ameng’atwa shingoni huko Nyegezi Kona. Amekutwa kwenye mawe huko. Kajifia..ushaona mazingaombwe....Basu amekufa kama mazingaombwe!!”
“Niniiii!!!!.” Kila mmoja wetu alishtuka kwa namna yake. Wahudumu walisimamisha walichokuwa wanafanya wote wakamgeukia mama mnene. Hakuna kauli aliyobadilisha alimaanisha alichokisema.
Mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanaenda kasi. Ile mashine kichwani ikageuka mzigo. Nikahisi kizunguzungu.
Alichokizungumza yule mama kilifanana na hali fulani halisi, ilikuwa ni hali gani na kwa nini nilikuwa natetemeka? Nilijiuliza. Sikupata jawabu. Nikafumba macho nikakumbuka saa nane usiku!!!!
NDOTO!!! NDOTO YA KUTISHA!! Ndoto iliyonipelekea kushituka nikiwa na maumivu makali. Na si maumivu tu. Nilikuwa nimekiuma kitanda kwa nguvu sana. Na…na …..na nilikuwa nakoroma kwa hasira. Kama Mbwa!!! Nilikuwa kama mbwa!!!
Hiki nini!! Nilitaharuki kwa hofu. Sikusema kitu chochote, niliulazimisha utulivu!!! Lakini moyoni hapakuwa na amani.
Inamaana nimekiota kifo cha Basu? Nilijiuliza. Bado sikupata jibu.
Nilivuta kumbukumbu ya sura ya Basu, nikamfananisha na yule mhanga wa kwenye ndoto.
Hofu!!! Alikuwa mtu mmoja. Niliyemuota alikuwa ni Basu!!
Nikapiga ukelele wa hofu.
“He Mungu wangu nimemuunguza dada wa watu.” Yule muhudumu alipiga kelele huku akizima mashine.
Hakugundua kuwa nilikuwa dunia nyingine kabisa tofauti na hiyo aliyokuwa anadhania.
Alinimwagia maji akaniosha nywele. Sikujali ubora wa kazi, nilikuwa nimehamakinika. Akili ilimuwaza Basu.
Kama amekufa kifo cha kufanana na kwenye ndoto maana yake nini?
Au nataka kuwa mtakatifu??? Nilijiuliza. Huku nikiamini moja wapo ya dalili za kuwa mtakatifu ni kuyajua yanayokuja kupitia ndoto.
Mh!! Utakatifu gani huu lakini hata kanisani penyewe siendi?? Nilitengua mawazo yangu.
“Dada nakuita jamani!!.” Sauti ya yule muhudumu ilinishtua. Inavyoonekana alikuwa ameniita mara nyingi sana.
Nilikuwa sipo kawaida na niliombea sana wasiitambue hali hii.
Simu yangu ikaita nikaitoa kuitazama alikuwa ni Dokta Davis.
Nikapokea na kuiweka sikioni.
“Samahani nipo saluni.” Nilimsihi.
“Usijali nilikuwa nakutaarifu ukatazame salio katika akaunti yako.”
“Hamna shida.” Nilimjibu na kukata simu.
(KOVU LA AJABU MGONGONI)Nilipotoka pale saluni nilitaka niende kwanza nyumbani kwangu lakini nikaona kwanza nipitie benki kutazama salio.
“Laki sita elfu sitini na sita na mia sita sitini na sita.” Hiki ndio kiasi kilichokuwa kimeongezeka katika akaunti yangu. Sikushtuka sana safari hii, nilikuwa nimeanza kuizoea pesa hii kubwakubwa.
Sikuwa na haja yoyote ya kutoa pesa kwani bado nilikuwa na pesa nyingi ndani. Niliingia katika bajaji iliyokuwa imenileta nikamuamuru anipeleke Kijiweni, huku ndipo nilikuwa naishi.
Tulipoifikia kona ya kijiweni nilitelemka na kuliendea duka la madawa nikachukua dawa za kutuliza maumivu.
Nilipofika chumbani nikanywa na kujipumzisha kidogo kwa minajiri ya kuoga baada ya dakika kadhaa. Nilikuwa bado nawaza kuhusu kifo cha Basu kwa kung’atwa, lilikuwa jambo la kushangaza sana. Na kilikuwa kifo cha kustaajabisha, kivipi afe kama ndoto yangu ya usiku? Nilijiuliza sana. Sikupata jibu. Nikajitia imani kuwa hizo ni ndoto.
Suala la kwamba ninaandaliwa kuwa mtakatifu lilinisaidia kupungaza hofu.
Lakini utakatifu gani sasa huu wa kuupata bila kwenda kanisani??
Kwani watakatifu wote walikuwa wanaenda kanisani!! Nilijiuliza. Kisha nikaukatisha mgogoro huu wa nafsi kwa kumpigia simu John, nilizungumza naye kidogo akaniambia yupo njiani kuelekea Nyegezi kona kutazama maiti ya Basu.
Aliposema jina hilo nikashtuka lakini hakugundua kwa sababu hakuonyesha wasiwasi na wala hakuuliza swali.
“Basu…Basu amekufa?” Nilijifanya sijui lolote. John akanieleza stori ileile kama mama mnene wa kule saluni aliyosema.
Nikaingia katika fumbo, sikumjua mfumbuzi!!!
Nikapitiwa na usingizi!!!
****
Nilikuwa nautazama sasa umati wa watu ambao sikuelewa ni shughuli gani walikuwa wakiifanya. Sikuwatilia maanani sana na wala sikujua
eneo lile ni wapi. Mara nikamuona mtu ambaye ninamfahamu. Nilitamani kumuita lakini niliamini kwa zile hekaheka alizokuwa nazo wala asingeweza kunisikia. Nikapuuzia!!
Sikujua nilikuwa nimejikita katika shughuli gani lakini kuna jambo nilikuwa nafanya.
Mara nikamwona tena yule mtu ambaye nilionekana kumfahamu, sasa alikuwa katika mtafaruku. Wenzake wote walikuwa wakimpigia kelele katika namna ya kupingana. Alikuwa peke yake na hakuna aliyemuunga mkono. Mara wenzake wakaanza kumzonga sasa hayakuwa mabishano tena bali ugomvi. Mtu mmoja anachangiwa na watu zaidi ya kumi. Ugomvi ukawa ugomvi. Kuna jambo walikuwa wanalazimisha. Jambo hilo huyo mmoja hakuunga mkono kabisa.
Baada ya kuzidiwa mara yule mtu akawaponyoka. Akaanza kukimbia. Alikuwa anakimbia huku akiangalia nyuma. Nilikuwa natabasamu nikimtazama maana alionekana kuwa na hofu kuu.
Alipogeuka mara ya kwanza lilikuwa kundi la watu watano wakimfukuza, akazidi kukimbia, alipogeuka tena walikuwa watatu, akajitahidi kujitetea kwa kuendelea kukimbia, wakabaki wawili. Safari hii hakugeuka.
Alipokuja kugeuka sasa alikuwa amekaribia kukamatwa. Lakini cha kutia moyo alikuwa anakabiliwa na mtu mmoja tu. Japo alikuwa amechoka lakini hata huyu aliyekuwa anakabiliana naye alikuwa anahema juu juu. Walikuwa wanatazama kama majogoo yanayofanyiana ubabe.
Mara jogoo lililokuwa linamkimbiza jogoo mwenzake likamrukia yule mkimbizwa. Wakaanguka chini, ugomvi ukazuka.
Wakagalagana hapo chini kwa namna ya kuchekesha. Nami nikawa nacheka.
Mara yule mtu niliyekuwa namfahamu akaangushwa vibaya. Halafu yule aliyemuangusha akachomoa kisu kidogo, upesi akamchana nacho mgongoni. Akatoa ukelele wa uchungu na hofu.
Kuchanwa huko kukawa kumemrejesha upya katika ugomvi. Sasa alikuwa na nguvu kamilifu. Yule aliyekuwa na kisu alipojaribu kumchana tena akawa amechelewa mkono wake ukadakwa, kisha kikafanyika kitendo cha sekunde kadhaa tu cha kuikamata shingo ya mwenye kisu na…na….na…
“Mamaaaaa!!!” Nikakurupuka usingizi!!
Nilikuwa nimelala masaa sita. Niliyapikicha macho yangu huku na huko niweze kuangalia vyema mbele.
Ukungu ulikuwa umetanda. Nikajipikicha zaidi nikaweza kuona, na sasa niliweza kusikia. Mlango ulikuwa unagongwa kwa nguvu. Fahamu zikanirejea vizuri, nikauendea bila hata kuulizia nikafungua.
Alikuwa ni jirani yangu.
“Kakasirika kweli John dah!! Amegonga mlango, kapiga simu yako
hupokei.” Alinieleza huku na yeye akionekana kukasirika.
Nilipiga mwayo mrefu kisha nikamuuliza kuwa alikuja saa ngapi. Akanijibu. Kisha akajieleza shida aliyokuwa nayo nikamsaidia . akaondoka!!!
*****
Sikuweza kuhudhuria msiba uliomuhusu Basu, akili yangu ilikuwa imechoka sana. Baada ya harakati za hapa na pale nilijipikia chakula kisha nilipomaliza nikalala tena.
Mara hii mlango ulipogongwa nilisikia vyema kabisa. Nikasimama na kwenda kumfungulia. Alikuwa John na ilikuwa saa tatu usiku.
John alikuwa amefanya mfano wa hasira usoni, nililitambua hilo na sikuwa na haja ya kumuuliza kwa nini amekasirika.
Baada ya kuzungumza naye dakika kama kumi hivi huku nikijiweka karibu naye. Alilainika na uso wake ukaunda tabasamu.
Tulizungumza mengi na mpenzi wangu huyu wa zamani. Na kama vile tulikuwa tumeambiana kwa pamoja tukageukiana tukakumbatiana kwa nguvu. John alikuwa analia.
Nilijua kuwa anamlilia Jesca, sikutaka kumuuliza najua angelia zaidi. Nilichofanya ni kuzidi kumkumbatia, viatu vikabaki sakafuni, sasa tukawa kitandani. Lugha iliyozungumzwa ilikuwa lugha ya mapenzi.
John alikuwa mtulivu kama aliyesafiri kwenda ulimwengu wa mbali. Nikaitoa shati yake akawa amebakiwa na singlendi. Nikataka kuitoa na ile.
“Ngoja nikaoge kwanza baby…” aliniambia kwa sauti nzito yenye kutamanisha.
Nikatulia nikamtazama naye akanitazama.
“Twende wote pliiz.” Nilimsihi. Hakujibu chochote nikajua kuwa maana yake ni kwamba twende.
Nikaziondoa nguo zangu, nikajivika upande wa kanga.
“He!! Sa na hiyo singlendi waipeleka bafuni kufanyaje tena!!!” Nilimuuliza John baada ya kumuona akiingia na ile singlendi bafuni.
“Si haujataka kunivua sa mi ntafanyaje?.” Aliniuliza kitoto. Nikatabasamu, nikamwendea, akakimbilia upande mwingine wa chumba nikamfata tukawa kama tunagombana. Japo hatukutumia nguvu sana!!!
“Ukiweza kunivua nakubeba mgongoni!!” Alinipa motisha nikazidisha juhudi. Nikaitoa nikawa mshindi.
Mshindi kubebwa mgongoni!! Ikumbukwe hiyo.
Mimi ndiye mshindi, mgongo mali yangu.
John akachuchumaa nikawa nyuma yake.
Ile nataka kupanda mgongoni nikaona kitu cha ajabu.
Kovu!!! Kovu bichi!!! Kovu katika mgongo. Kovu la kuchanwa na kisu!!
“Mamaaaaa!!” nikapiga kelele. John akasimama. Tayari nilikuwa katika kona ya chumba nikiwa natetemeka sana!!!
“Sabe sabe!! Umekuwaje…Umekuwaje mpenzi wangu!!” aliniuliza huku akinisogelea. Nikawa namkimbia, lakini wakati huu haukuwa mchezo tena nilikuwa katika hofu ya ukweli. Nilikuwa namuogopa John.
John alinisihi niache utani!!! Lakini sikuwa natania. Nilikuwa katika kumaanisha.
Hali ilikuwa tete. John alikuwa ananitisha.
Nikiwa katika kumkimbia John. Sasa aligundua kuwa kuna jambo limenisibu. Akanifuata kwa kasi. Akanivagaa. Nikajilazimisha kujitoa mikononi mwake huku nikipiga kelele. Ghafla akaninasa vibao viwili.
Sasa hapo ndio nikachanganyikiwa mwenzenu na kuamini kuwa dunia imefika mwisho. Nililia huku nikimtaja mwalimu Nchimbi.
Lakini cha ajabu na kukera huyo mwalimu Nchimbi hata hakuwa akinisikia.
Iliniuma. John akaniongeza vibao vingine viwili. Sasa yale maumivu akili ikasogeleana.
“John una damu!! Una damu!!”
“Damu??” aliniuliza.
“Mgongoni umekuwaje wewe.”
“Mgongoni pamekuwaje kwani…alilalamika huku akijipapasa”
Maajabu mengine jamani!. Mkono wake haukuwa na damu. Akanigeukia.
Nikatamani kuiaga dunia niende likizo mbinguni. Hakuwa na kovu. Mgongo laini kabisa wa kiume ukatazama nami. Nikaruka mita kadhaa.
Akapoteza uelekeo kuniona naruka vile nikataka kukimbia nje.
Akanidaka kanga yangu. Kanga ikateleza ikauacha mwili.
Shanga nane za rangi tofauti zilizokishika vyema kiuno changu ndio pekee zilizosalia katika mwili wangu. Sasa John alikuwa amebaki na kanga mkononi mimi nikiwa nina shanga kiunoni. Nusu nilikuwa nje na nusu nilikuwa ndani.
Swali likavamia kichwa changu.
Nikimbie na shanga kiunoni nikiwa uchi kwenda nje ama nirudi chumbani kwa John huyu wa maajabu!!! John niliyemuhisi kuwa sasa ni ………….
Nikabaki katika kizungumkuti.

*** ISABELA katika mtihani, ameota ndoto ya ajabu sana mtu anachanwa na kisu mgongoni……cha kushtua na kustaajabisha anakutana na kovu bichi katika mgongo wa John…mara ghafla lile kovu likatoweka…..kwa sasa hii si ndoto ni ukweli mbele yake…….***Je isabela atatoka nje uchi akiwa na shanga pekee ama atamkabili John….ITAENDELEA …..!!!!!!!!!
Previous Post Next Post