RIWAYA:SITAISAHAU facebook
SEHEMU YA KUMI NA NANE.
Hatukuwa tumezungumza lolote. Hadi pale tulipokutana na mwanaume mwingine. Huyu alikuwa ametoka kukata kuni. Tulimpisha njia kisha tukamfata kwa nyuma tukamvamia, akapiga mweleka. Alipojaribu kurusharusha miguu. Alama ile chafu ikaonekana katika paja lake. Bila kujiuliza Isabela mimi nikafanya kama nachuna mbuzi. Nikaikata nyama ya paja lake. Mwanaume huyu akalia kama mtoto.
Nilipoiondoa nikaitupia mbali. Baada ya muda akatokea yule nyoka akakichukua kile kipande.
Sasa tukazidi kufunguka akili kuwa yule nyoka anawaona watu wenye alama. Na yawezekana ni nyoka huyu yupo katika kuwamiliki wanadamu kwa chapa yake ya hatari.
Swali kuu likabaki. Tunatoka vipi katika pori hilo.
Mwanaume yule hakuzimia, alikuwa na timamu zake. Tukamweleza kwa kifupi naye akajieleza kuwa, tamaa ya utajiri imemtupia katika shimo hili baya.
Yule mwanaume alijitambulisha kwa jina la Samson alikumbuka vyema kuwa kabla ya kufika hapo alikuwa mkazi wa jijini Mwanza na alikuwa mwanafunzi katika chuo cha biashara (CBE) tawi dogo la jijini Mwanza.
Huyu alikuwa Samson kweli maana alikuwa ni mbabe sana. Lile kovu lake la kwenye paja halikumsumbua. Tulitembea kidogo akachuma majani fulani akayasagasaga akayaweka katika lile kovu. Hapa sasa aligumia kwa maumivu. Bila shaka ile dawa ilikuwa kali sana.
Akaniwekea na mimi katika kovu langu. Nikapiga mayowe. Akanikamata imara. Hadi maumivu yalipotulia kidogo. Jenipher hakutaka kovu lake la sikioni liguswe aliweza kuyakadiria maumivu makali ya dawa ile.
Siku mbili zilipita. Kovu lilikuwa linakauka kwa kasi. Nilimshangaa kijana huyu.
Siku hiyo ya pili harakati za kujikomboa zilianza rasmi. Jeshi letu bado lilikuwa dogo. Tulihitaji jeshi kubwa zaidi.
Samson alituongoza hadi katika ngome ambayo yeye alikuwa akishi hapo kabla. Walioishi katika ngome hii ni wanaume wababe wanaoweza kufanya kazi ngumu. Tuliindia hapa na kuwakuta wanaume sita waliojaa haswahaswa. Kama ilivyo kawaida hawakuweza kutuona japo kila mmoja alikumbwa na hisia za namna yake mwenyewe.
Mimi kisu mkononi. Samsoni panga kubwa mkononi, Jenipher kazi yake kukaba kwa bidii zote. Sisi wawili tukawa tunakata tu!!
Iwe sikioni hiyo alama. Sikio sio lako tena!!
Iwe kwenye mkono. Samsoni anaushusha mzima mzima.
Kama ni kiganja. Mimi naondoka nacho kwa kutumia kisu changu. Ikishindikana tu, panga kubwa la Samson linatimiza wajibu.
Waliokuwa wamewekewa alama katika vifua vyao hawa walitupa wakati mgumu sana na tulilazimika kuwaacha wanaume wawili. Wanne tukaungana nao.
“Sam kwani we kabila gani?” nilimuuliza wakati tunaondoka.
“Msukuma wa Bariadi!!” alinijibu huku akijaribu kutabasamu.
Amakweli!! Hana huruma mtu huyu kama vile…kama kabila gani vileee…..
Nilipotea katika mawazo nikarejea katika uhalisia. Joka kuu tukapishana nalo. Wenzangu wakakumbwa na uoga. Mimi sikuogopa tena. Nilijua kazi gani linaenda kufanya.
Jeshi lilikuwa kubwa sasa na kila mmoja alikuwa na nia ya kuwa huru hivyo tulipambana kwa bidii sana.
Mapambano yalikolea sana kwani kila siku tuliongeza timu ya ukombozi.
Kilichotutatiza ni kuijua njia ya kutokea. Sasa tukiwa tunajiamini kabisa siku hii hatukutembea kwa kundi kubwa bali kila mmoja alienda njia yake huku akijiamini kabisa kuwa hawezi kuonekana. Nia ikiwa kutafuta njia.
Shughuli hii ilianza asubuhi kabisa. Mimi na Jenipher tulienda njia yetu. Huku jeshi jingine nalo likienda njia tofauti.
Masaa yakapita na jioni ikawadia. Ile jioni ambayo tulikuwa tumekubaliana tukutane.
Tulingoja kwa muda mrefu lile eneo tulilokubaliana tukutane lakini wenzetu hawakutokea.
Tulisubiri sana, hatimaye giza likaanza kuiingia. Nikaingiwa na wasiwasi, huenda wenzetu waliipata njia na sasa wapo huru wametusahau sisi. Nilijilaani kwa kuruhusu hali hii ya kila mmoja aende kivyake.
“Jenny”
“Bela” aliitika.
“Unaweza kuwa unajua lolote kuhusu hawa watu.”
“Mh!! Kwakweli hata mimi nipo katika mashaka.”
“Wanaweza wakawa wamepata njia na kutoroka?” nilimuuliza.
“Kama hawajatoroka basi kwenye kambi ya usiku lazima watakuwepo.”
“Kambi ya usiku ndio nini?”
“Kila usiku wanachama ama wananchi wa mji huu huwa wanaitishwa kitu kama gwaride hivi, tena leo ni gwaride kuu.”
“Linafanyika wapi.”
“Nitakupeleka Bela. Lakini panatisha sana huko. Na sijui kama patakuwa salama.”
“Jenny pawe salama ama pasiwe salama..kwa sasa haina maana ujue bora kufa sasa..maisha gani haya unadhani.”
Jenny alikubaliana na mimi, akaniongoza kwenda katika kambi kuu. Kila mtu alikuwa kimya sana. Nilikuwa namfuata Jenny anapoelekea. Hadi tulipoona mahali panafuka moshi
“Huko wanakula nyama…na damu pia.”
“Kwa mifugo gani sasa?” nilihoji kwa sauti ya chini.
“Wananchi wanaotaka kutoroka huwa wananyonywa damu.” Nilishtuka sana kuisikia kauli hiyo.
“Na leo kuna mwananchi alitumwa damu kutoka Naijeria, ndio leo anaileta sasa.”
“Na wewe umekula nyama ya mtu?” nilimuuliza.
“Hapana hizo wanakula viongozi wakubwa tu. Mwananchi ukila ama kunywa damu wanasema unakuwa kama wao. Kwa hiyo hairuhusiwi hata kidogo”
Alinieleza kwa utulivu mkubwa.
Tukaifikia KAMBI YA USIKU.
Shangwe zilikuwa kubwa na watu takribani hamsini walikuwa wakisheherekea.
“Ndio watu wote hawa ama kuna wengine?”
“Ni hawa tu!! Ujue hii ardhi ndio kwanza ilikuwa imeanzishwa.”
Nilikuwa kimya nikiwatazama watu kwa mbali tulipojificha. Nilimuona John, nikamtambua na Jesca. Baadaye kila mmoja akatulia kuna mtu alitaka kuzungumza neno.
“Leo raisi atakuwa amekuja. Isabela tuyondoke hapa.”
“Raisi ndio nani?” niliuliza kwa jeuri. Kuna kitu kama hasira kilikuwa kimenikaba kooni na sikuhisi uoga hata kidogo.
“Mkuu wa Nchi hii. Huwa haoneshi sura yake lakini anaitwa mtukufu raisi.”
“Na yule anayeonekana ni nani?”
“Yule tulitambulishwa kwake kama waziri wa miundombinu…njia zote anazifahamu yeye.”
Niliposikia hivyo nikatamani sana kumtia mikononi, mtu yule aliyeitwa waziri wakati namfahamu kwa jina la Osmani!! Huyu alikuwa ni Osmani mwanaume aliyenipatia namba ya simu 6666666. Na ni huyu huyu aliyenijia ndotoni akiwa na John wakimkwapua mama yangu mzazi.
Sikuwa na uoga. Nilipiga hatua sasa nikawa nimejichanganya na watu hawa wachache waliokuwa wakimtumikia shetani.
Osmani alikuwa akiongea kwa maringo na kutumia amri sana.
Kila mtu alikuwa anamsikiliza.
“Leo damu ipo nyingi, nyama za kusaza.”
“Manson, Fanson, Rinzon, Wenton, Zeiron.” Alitaja vitu nisivyovijua na kila alipotaja kuna mtu aliitika na kwenda mbele. Walikuwa wanaume watano waliojaa vyema.
Bila shaka walikuwa wanaujua wajibu wao. Niliwaona wakizichukua kamba nene kabisa. Pamoja na visu.
Walitulia kwa dakika kadhaa, mara wakaletwa mbele yao watu ambao walionekana wazi kuwa walikuwa wamechoka sana.
Nilimuona Samson akiwa amevimba sana kutokana na kipigo. Hasira ikanipanda. Nikatulia tuli!!
Wanaume wale walioitwa kwa majina ya ajabu wakatumia kamba zile kutengeneza namna ya vitanzi, kisha wakavitundika mtini.
Mwanaume mmoja akamchukua mvulana kutoka katika lile kundi. Mvulana yule hakuwa na sikio. Nikamkumbuka ni mimi niliyemkata ili kumtoa katika ulimwengu huu wa giza.
Nikiwa sijatafakari nini cha kufanya, nikashuhudia damu ikikingwa kutokea shingoni. Kisha akatupwa katika kitanzi. Alikuwa maiti!!
Samsoni akavutwa akataka kuleta ukorofi. Akachapwa na mjeledi akapiga yowe kubwa huku akitukana matusi mazito mazito kwa kabila la kisukuma.
Alipotukana akanikumbusha wakati aliokuwa ananiambia jina lake. Nikajisikia uchungu.
Liwalo na liwe!! Nikaanza kusogea mbele. Bado Samson alikuwa akiwasumbua. Maajabu nikafika mbele ya hawa wanaume hawakuweza kuniona. Nikajaribu kumsukuma mmoja aliyekuwa na kisu tayari kwa kumchoma Samson. Haya yakawa maajabu makubwa. Isabela mimi namsukuma mwanaume mkubwa kama yule anaanguka kwa kishindo hivyo. Samson mwamba wa kisukuma, msukuma kutoka Bariadi akafanya jambo ambalo hadi leo ni kumbukumbu kwangu. Haraka akaokota visu viwili, akavimba kwa hasira kifua chake kikaweka mfereji mkubwa. Samsoni alikuwa amevimba kama mcheza mieleka.
Nikabaki kushangaa. Akamrukia mwanaume mmoja sijui ndio Frazon, Manson ama vipi. Kisu kimoja. Mwisho wa uhai.
Akakichomoa akamrukia yule ambaye alikuwa chini baada ya mimi kumsukuma. Visu viwili vikazama katika sehemu zake za siri. Damu ikaruka. Nikasisimka sana!! Samson hakujali.
Sasa yule Osman akawa ametaharuki. Hajui nini kinatokea. Na yeye hakuwa ananiona. Nikamwona akimjaribu kumfuata Samsoni huku akiwa na jambia. Samson hakuwa anamuona.
“Saaam!! Saam!! Nilimuita.” Maskini hakunisikia.
Osmani na jambia. Akalichomoa mahali ambapo linahifadhiwa.
Akalielekezea alipo Samson. Alipoanza kukimbia na mimi nikashtuka nikaanza kukimbia. Kabla hajamfikia. Mimi nikamfikia. Nikafanya kumsukuma. Akapepea kama karatasi. Takribani mita arobaini kutoka pale nilipokuwa. Samson alipogeuka, hakunitazama mimi bali alitazama chini. Akakumbana na jambia.
Msukuma huyu mkali kabisa wa mapambano akatupa visu chini akatwaa jambia.
Ilimchukua dakika chache. Manson, Fanson, Rinzon, Wenton, Zeiron. Wote wakawa tayari kwa kuzikwa kama hiyo nchi yao ina huo utaratibu wa kuzika.
Samson alikuwa kidume!! Nilikiri.
Kidume yule ambaye hakuzisikia sifa nilizokuwa nampa. Alizidi kunidhihirishia kuwa kile kifo cha yule mvulana cha kuchomwa kisu shingoni kilimuuma. Aliendelea na zoezi la kuwaondoa wananchi kadhaa kwa fujo zile alama za 666 popote zilipo katika miili yao. Ilimradi tu hakuwaua.
Nia ikiwa kukuza jeshi letu!!
Nami nikamuunga mkono!! Jenny naye huyo akaokota kisu kikubwa kaanza kufanya kazi.
Tulilolifanya hapo lilikuwa kosa kubwa sana. Alama za 666 zilizokuwa zinaanguka katika mfumo wa vipande v ya nyama. Ukaleta balaa.
Joka kubwa kuliko lile la awali likaibuka. Joka hili sasa lilikuwa halijulikani wapi mbele na wapi nyuma.
Lilikuwa na vichwa viwili. Mbele na nyuma.
Halikujulikana linatambaa kwenda kaskazini ama kusini, magharibi wala mashariki.
Yule bingwa wa mapambano Samson akajikuta analiachia jambia lake, Jenny aliyekuwa anaanza kunogewa na shughuli ya kukata nyama za watu naye akatulia tuli.
Nami nikakumbwa na uoga na nikakiona kifo kikibisha hodi.
Isabela nakufa!! Nakufa nikiwa katika u…”
Kabla sijamaliza kuwazua. Ghafla……..Ghafla!!!!!
Ilikuwa ghafla sana!!!!
**ITAENDELEAAA
About Author
JE, UNA HABARI, PICHA, TANGAZO, MAKALA NA USHAURI? USISITE KUWASILIANA NASI SIMU / WHATSAPP NAMBA 0625535420.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.