Kawaida ni kwamba ili soka la sehemu fulani kukua na kustawi zaidi, linabidi kukubali kuchukua baadhi ya vitu vya Soka la eneo lingine ikiwa pamoja na wachezaji ili kuongeza ladha na kulifanya soka la sehemu hiyo kukua zaidi.
Tanzania kama nchi inayopigania kukua kisoka,pia imelazimika kuchukua wachezaji wakigeni ili kuongeza ladha na changamoto kwenye ligi yetu na hatimaye kuistawisha zaidi.
Ukiachana na Haruna Niyonzima, Patric Sunzu, Stephie Mieno, Brian Umonyi na wengineo,yupo mchezaji mwingine wa kigeni kutoka Afrika ya Magharibi Nchi ya Ivory Coast naye ni mshambuliaji wa Azam FC Kipre Tcheche.
Mjue mchezaji huyu kiundani kwa mazungumzo yafuatayo.
MWANDISHI: Mchezaji huyu amesajiliwa na Azam FC takriban misimu miwili iliyopita akitokea Ivory Coast, hapa anaelezea mahali, mwaka na timu ya kwanza aliyoanzia Soka kabla ya kushuka Tanzania.
KIPRE TCHETCHE: Nilianza Soka mwaka 2003 nikiwa shuleni huko kwetu Ivory Coast, mwaka 2006 nilijiunga na timu ya Satellite ikiwa daraja la kwanza, baadae nilijiunga na timu ya ligi kuu inayoitwa Darlua ambapo nilicheza kwa mwaka mmoja, nikapata timu huko Abdijan ambapo nilicheza kwa miaka 3 na kuwa mfungaji bora katika msimu wa mwisho na baadae nikajiunga na Azam.
MWANDISHI: Kipre Tcheche ni ladha mpya kwenye tasnia ya soka la Bongo kutoka Afrika ya Magharibi, kwa muda uliotumikia soka hili, unalielezeaje ukilinganisha na Soka la Ivory Coast ambalo pia limesambaza vipaji vingi barani Ulaya na kwingineko Duniani.
KIPRE TCHETCHE: Soka la hapa ni tofauti na Ivory Coast kidogo, hapa ushindani ni mkubwa, ligi ni ndefu, pia mechi za ugenini ni ngumu mno, nilitakiwa kuwa na uvumilivu wa takriban miezi 6 kuzoea soka la Tanzania, baada ya hapo nikaweza kucheza na sasa nina uzoefu wa miaka miwili.
MWANDISHI: Kitu gani wewe hutamani kukifanikisha mara zote katika Soka la Bongo hasa unapokuwa uwanjani na unakichukulia kama changamoto?
KIPRE TCHETCHE: Ninapofikiria soka na ninapokuwa kwenye uwanja, muda wote nawaza kufunga, ndio maana hutumia juhudi nyingi kutafuta mabao, hata ninapokuwa kwenye mazoezi hupenda kufunga sana pia, huwa nawatania wachezaji wengu kwa kuwaambia kuwa lazima nitafunga na ninafunga kweli hii inanijenga kuwa na uwezo wa kufunga sana kwenye mechi.
MWANDISHI: Ni fahari kubwa kwa mchezaji yeyote anapoitwa kuchezea timu yake ya Taifa, timu ya Taifa ya Ivory Coast ina wachezaji wengi Nyota kutoka ndani na nje ya nchi hiyo,v ipi kwa upande wako una ndoto ya kuichezea timu hiyo?
KIPRE TCHETCHE: Ndio nina ndoto ya kuchezea timu ya Taifa, na nimeshawahi kucheza kipindi cha nyuma lakini kwa sasa ni vigumu ukizingatia mimi ninacheza Tanzania wakati wachezaji wengi wa nyumbani wanacheza Ulaya hasa Ufaransa.
MWANDISHI: Ukiwa mchezaji unayecheza nafasi ya ushambuliaji, kati ya mabao ambayo umewahi kufunga ukiwa na timu tofauti na mechi tofauti, bao gani unalipenda na hauwezi kulisahau muda wote?
KIPRE TCHETCHE: Mimi bao ninalolikumbuka mara zote ninapowaza soka ni nilolifunga dhidi ya Malawi kwenye mashindano ya CECAFA, nilipokea mpira na kufunga nikiwa umbali mrefu, pia nakumbuka sana bao nililofunga dhidi ya Yanga kwenye kombe la mapinduzi nalo nilipokea mpira kutoka kwa Sure boy kisha nikafunga.
MWANDISHI: Jitihada zako unapokuwa uwanjani zimezaa matunda msimu uliopita hatimaye kuibuka mfungaji bora wa ligi kuu, kitendo hicho umekichukuliaje, na je umeshawahi kuwa mfungaji bora sehemu nyingine?
KIPRE TCHETCHE: Yeah nimefurahi sana kupata tuzo hii, ni ndoto ya kila mchezaji kupata kitu mwishoni mwa ligi lakini hii sio mara yangu ya kwanza, nimewahi kuwa mfungaji bora huko Ivory Coast. Ninaishukuru timu yangu, ninawashukuru sana pia wachezaji wenzangu kwani wao ndio waliofanikisha mimi kuwa mfungaji bora.
MWANDISHI: Na vipi kuhusu mahusiano yako na familia yako kwa ujumla ambayo umeicha Ivory Coast kwa muda wa miaka miwili sasa.
KIPRE TCHETCHE: Nina mchumba nyumbani kwetu Ivory Coast, atakuja hapa lakini sio hivi karibuni. Unajua huwa ninatamani sana kuwa karibu na familia yangu, lakini maisha ya soka mara nyingi hayaruhusu hali hiyo, miezi mingi nakuwa mbali nao lakini sina cha kufanya kwa kuwa ndio aina ya maisha niliyochagua.
MWANDISHI: Maneno gani ya Kiswahili ambayo uliyasikia kwa mara ya kwanza kabisa na ukayaelewa na hawezi kuyasahau.
KIPRE TCHETCHE: Maneno ya kwanza ya Kiswahili mimi kuyasikia ni Mambo na Asante. Unajua unapoenda sehemu ngeni, unafundishwa kwa haraka kusalimia na kushukuru, hivyo maneno niliyoyasikia kwa mara ya kwanza maneno mambo na asante........
Kipre Tchetche sio raia wa Ivory Cost pekee anayecheza ligi Kuu Tanzania Bara, yupo na ndugu yake ambaye ni pacha wake anayeitwa Michael Balou ambaye pia anachezea Azam FC. Anamuelezeaje ndugu yake hasa baada ya kuibuka mfungaji bora?
MICHAEL BALOU: Ninachoweza kusema juu ya Kipre ni kwamba ana juhudi ya mazoezi mno, anapenda kufunga hata kwenye mechi ndogo, ndio maana ameweza kufanya kazi hii nzuri lakini kitendo hiki hakinishangazi sana kuwa ameshawahi kuwa mfungaji bora mara kadhaa na msimu wa mwisho Tchetche kucheza Ivory Coast alikuwa mchezaji bora.
MWANDISHI: Michael ukiwa pacha wa Kipre, unajisikiaje unapokuwa uwanjani na kaka yako katika michezo mbalimbali.
MICHAEL BALOU: ninapokuwa uwanjani na kaka yangu ninafurahi sana, kama nilivyosema anapenda kufunga, hivyo mara nyingi ninapokuwa nae huniita na kuniomba pasi ili afunge - kitendo hicho hunifanya kujihisi mwenye furaha na amani.
Imeandaliwa na James TupaTupa
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.