Unknown Unknown Author
Title: RIWAYA: ROHO MKONONI 3
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
MTUNZI: George Iron Mosenya SMS: 0655 727325 SEHEMU YA TATU Hatimaye Betty akatoweka kama anayerejea baada ya masaa kadhaa lakini ikakati...

MTUNZI: George Iron Mosenya

SMS: 0655 727325

SEHEMU YA TATU

Hatimaye Betty akatoweka kama anayerejea baada ya masaa kadhaa lakini ikakatika miaka bila wawili hawa kuonana, hadi Joyce akakiri kuwa wasingeweza kuonana tena, hasahasa baada ya mama yake Betty naye kutoweka kijijini kuelekea mjini Bukoba kuwasabahi ndugu zake kisha akaipanda meli ya Mv Bukoba aende Mwanza kumsalimia Joyce.

Ile ajali mbaya isiyosahaulika nchini Tanzania, ajali ya meli ya MV Bukoba: na yeye ilimkumba akiwa ndani.

Mwili wake haukuweza kupatikana, labda uliliwa na samaki ma vinginevyo…..

Kizazi cha Betty kikatoweka rasmi Ukala. Katika namna ya kufadhaisha na kuumiza mioyo.

Hii ilikuwa mnamo mwaka elfu tisa mia tisini na tano (1995)

Kifo cha mama Betty kilipokelewa kwa simanzi kuu, lakini kwa kuwa hakikuwa kifo cha kwanza kuwahi kutokea. Nacho kilisahaulika kama vingine kisha maisha yakaendelea.

Joyce akabaki mpweke kwa miezi kadhaa kisha akaizoea hali, akapata marafiki wapya. Alipobalehe na kuingia darasa la sita tayari alikuwa amemsahau Betty. Akabakia katika simulizi tu hasahasa wanafunzi walipokuwa wakikumbushana umahiri wake katika michezo ya riadha.

“Angekuwepo Betty, tungeshinda….” N’do kauli zilizosikika. Kisha kupotea kama upepo maana huyo Betty hakuwapo tena.

Ilikuwa siku ya mtihani wa kumaliza muhula wa kwanza na kwenda likizo ya mwezi wa sita. Likizo ndefu ya mwezi mzima.

Joyce alikuwa ametoka katika mtihani akiwa na furaha sana. Licha ya usichana wake kuanzia utoto na sasa akiwa amebalehe hakuwahi kutoka katika kisiwa cha Ukerewe na kusafiri hadi mkoa ama wilaya nyingine. Sasa likizo hii alikuwa ana safari ya kwenda mkoani Mwanza. Mama yake mdogo aliahidi kumchukua kwa ajili ya kwenda kumsaidia kulea mtoto wake ambaye alikuwa na miezi minne tangu azaliwe. Joyce hakujali kuhusu ugumu wa kulea mtoto, alichotazama ni kupanda meli na kuufikia mkoa wa Mwanza, mkoa ambao alikuwa akiusoma tu katika masomo ya Jiografia na Historia.

Safari hii ilikuwa iwe siku inayofuata asubuhi sana, kwani mama yake mdogo alitarajiwa kujiunga nao nyumbani siku hiyo ya kumaliza mtihani kisha kufunga safari siku inayofuata.

Tofauti na siku nyingine za kufunga shule ambapo Joyce huungana na wanafunzi wengine kufanya lolote lile ambalo litaitangaza furaha yao ya kumaliza ngwe moja na kuhamia nyingine, siku hii alikuwa tofauti sana, hakuwa na hamu kabisa na vikundi vikundi, na hata makamu mkuu wa shule alivyotangaza rasmi kuwa shule inafungwa Joyce alitimua mbio kuelekea nyumbani ili aweze kujiandaa na safari siku inayofuata.

Alihisi akitembea atachelewa kufika, basi akawa anaimba huku akiruka rukia huku na kule. Hatimaye akaikaribia nyumba.

Tabasamu likachanua usoni alipoona begi jipya nje ya nyumba yao ndogo.

“Mwee!! Mam’dogo kafika huyo.” Joyce alijisemea, kisha kabla ya kupiga hatua zaidi akaikung’uta sketi aliyokuwa amevaa na kisha kuichomekea vyema blauzi yake. Halafu akasita kujirusha rusha akawa anatembea kwa ustaarabu.

Akafika mlangoni akajikoholesha, maana kuna wakati mama na baba yake huwa na faragha hivyo anahofia kuwaingilia.

Kimya!! Hakuna aliyesema neno lolote.

Akaanza kujiimbisha nyimbo zisizokuwa na mantiki yoyote ili kutambulisha marejeo yako kutoka shuleni, waliomo ndani waweze kumsikia na kumlaki kama itafaa. Nyimbo hazikumshtua yeyote.

“Au wameenda kisimani….” Alijiuliza tena. Lakini akajikuta kama kuna sauti inamsihi kuwa kisimani hawawezi kwenda na kuacha begin je.

Joyce akajikongoja akaufungua mlango huku akisindikizwa na neno ‘hodi’ neno lisilojibiwa na mtu yeyote hadi pale jicho la Joyce liliposhuhudia dimbwi la damu katika sebule yao isiyokuwa na marumaru wala sakafu.

Aliyelizunguka dimbwi lile alikuwa ni mwanamke wa makamo. Alikuwa ameuma meno yake kwa maumivu makali sana, mikono yake ililikumbatia tumbo lake na uso wake ulifanywa wa kutisha na yale macho ambayo yalikuwa yamekodolewa. Joyce alidondosha bila kutambua kalamu zake pamoja na rula chini.

Hivyo hivyo bila kujua nini anafanya akajikuta anapiga yowe moja kubwa sana huku mikono yake ikiwa imekipakata kichwa chake.

Kisha historia ikabadilika……

*****

. . Kifanya NJOMBE, 1998.

Mwanafunzi mwembamba, si kwa kuzaliwa bali lolote lile linalohusiana na hitilafu kiafya alikuwa akitetemeka. Meno yakigongana kinywani, wanafunzi wenzake hawakupoteza muda wao kumtazama, kila mmoja alikuwa na mambo yake anayofahamu mwenyewe. Nguo zake mpya zilizolizidi umbo lake zilimfanya asikitishe zaidi kumtazama, kichwa chake kisichokuwa na nywele nd’o walau kingeweza kuushawishi umati wa wanafunzi kumtazama kwa jicho la kuibia kutoka mbali. Maana wasichana walikuwa katika harakati za kushindana mitindo ya nywele lakini mwenzao hata hakuonekana kuhangaika na mambo hayo. Alishangaza.

Msichana mmoja aliyetembea kijivuni alijikwatua huku macho yake yakipepesa huku na kule. Na kila alipoangaza huku na kule wanafunzi walizidi kujikita katika majukumu yao nje ya darasa.

Macho yale yanayopepesa kwa shari na midundiko ya kijivuni hatimaye kituo kikawa mita hamsini kutoka mahali alipokuwa ameketi msichana mwembamba akisota na baridi.

“Yaani wewe wenzako wanadeki madarasa, wengine wanafyeka nyasi wewe ambaye hii shule ni ya baba’ko unaota jua sivyo bosi!!” ilisikika sauti ile kali kwa uzuri kabisa.

Macho ya wanafunzi yakahamia tena katika kuwatazama wawili hawa, bila shaka lilionekana kama jambo la kushangaza sana kwa sauti hii kukoroma kisha yeyote yule anayeambiwa asiruke upesi na kujitetea ama la kukimbilia mahali anapoelekezwa. Lakini leo ilikuwa tofauti. Sauti ililazimika kurudia mara ya pili.

“We mtoto una kiburi eeh!! Yaani mimi naongea……..” akaikata kauli yake ile kwa muda kisha akapiga hatua kubwa kubwa akamfikia yule msichana mwembaba, “…halafu wewe mjinga umekaa umeridhika” akaimalizia kauli yake kwa kofi zito lililotoa mlio mkubwa sana na kuwaduwaza wachache kwani wengi kati yao walikuwa wakiitambua vyema shughuli ya dada yule.

“Mi mge…ge…ni dada!!” hatimaye yule msichana mwembaba ambaye hakujishughulisha kupambana na dada yule alijitetea kwa sauti ya kulalamika huku kwa mbali akiugulia maumivu.

“Mgeni?..mgeni hapa kwa mama yako nimekuuliza, shule alijenga baba yako hii pumbavu wewe…..ujinga ujinga mwingine uwe unamfanyia mama’ko nyumbani sio hapa…..hili ni jeshi. Bastard!!!” alizidi kupayuka yule dada, sasa alikuwa anaiweka sawa fimbo yake ambayo ilikuwa imehifadhiwa kiunoni.

Hapa sasa wengi walimuonea huruma msichana mwembamba kwani kilichokuwa kinaenda kufanywa na dada mwenye mikogo kingemuharibia siku kabisa na huenda kumtia makovu kadhaa ya muda mrefu.

Msichana mwembamba aliunyanyua uso wake vyema na kumtazama yule dada mkubwa kiumbo na mwenye madhari yote ya ujivuni wa maksudi, na uso wake ulitangaza mamlaka.

Macho yalinata katika uso wake, hiyo sura aliwahi kuiona mahali lakini hakumbuki ni wapi. Alijaribu kumkazia macho huenda na yule mtazamwaji atamkumbuka lakini haikuwa hivyo. Akashtukia ghafla fimbo ikipenya katika shingo yake, mauymivu yakatambaa kuanzia shingoni kisha kuutawala mwili mzima, hakumbuki kama alipiga yowe kubwa kwani alikuwa ameendelea kumkodolea macho msichana yule ambaye midomo yake ilikuwa inachezacheza kama anayesema kitu.

Hatimaye akamkumbuka……

“We mshenzi ninarudia tena, ujinga ujinga kafanye kwa mama yako nyumbani sawa!!!” neno kutoka kwa dada mjivuni likamwingia msichana mwembamba masikioni vyema. Na hapo akili yake ikiwa imemkumbuka vyema yule dada, pigo lililofuatia msichana mwembamba akafanya jitihada za kupangua.

Kama alipanga vile akafanikiwa kuikamata ile fimbo. Na hakuiachia, hapa macho ya wanafunzi yakazidi kuweka umakini, walikuwa kimya bila kushabikia lolote maana halikuwa tukio la kwanza shuleni hapo. Wengi walisikitika maana kuikamata fimbo ya dada yule akiwa anakuchapa ni kujihalalishia kung’atwa meno na kupigwa mateke.

Mama!! Anamtukana mama yangu….mama yangu hakuzaa mtoto mjinga kama anavyodai, mama yangu aliwahi kusema kuwa nina akili sana…..mama hakuwahi kunipiga namna hii…hakuwahi hakuwahi……ANAMTUKANA MAMA!!!!! Msichana alifunguka akili na wakati huo yule dada mweupe alikuwa anajiweka sawa kwa shambulizi jipya.

Ni hapa alipokutana na upinzani wa kwanza katika maisha yake ya uonevu, msichana mwembamba ambaye baridi lilikuwa limeukimbia mwili kwa kashkashi zile alimrukia na kumtia kucha za usoni kisha hakutuliza mikono akaanza kumkwangua.

Puuu! Dada mweupe akaanguka chini.

“Wewe mjinga unamtukana mama yangu…” alisema haya huku sasa akipiga bila kuangalia wapi anapiga, “hujui wapi alipo mama yangu unamtukana tu….umenichokoza pumbavu wewe!!” aliendelea kumdhibiti.

Kwa kuwatazama ilishangaza sana ni sawasawa na ule ugomvi wa ‘Zena na Betina’ katika majarida ya Sani enzi hizo.

Hapa sasa wanafunzi wakasogea kuangalia tukio hilo la kuuanza mwaka. Dada mjivuni alijaribu kufurukuta lakini hakufua dafu, sasa wanafunzi walipata nafasi ya kutangaza chuki zao, kelele za kuzomea zikachukua hatamu. Waalimu ofisini wakashtuka na kukimbilia eneo la tukio wajue nini kinawasibu wanafunzi.

Lahaula!! Dada mkuu shule ya msingi Kifanya alikuwa amewekwa katika wakati mgumu na msichana mgeni shuleni pale, upesi waalimu wakaingilia, wakajaribu kumwondoa yule binti lakini alikuwa ameung’ang’ania uso wa dada mkuu, hata waliposaidiana ndipo walifanikisha. Dada mkuu alikuwa hatamaniki, waungwana wakawahi kumstiri, matiti yake makubwa yalikuwa nje..msichana mwembamba alikuwa amemrarua haswaa.

Wakati wakijishughulisha na matiti mara sketi nayo ikaanguka, kumbe zipu ilishavurugwa na mikono ya dada mwembamba.

Wanafunzi wa kiume wakashangilia kwa nguvu zote. Sio kwa kukifurahia kile kitendo bali kwa kufurahia ni nani kimemtokea.

Msichana mwembamba akiwa bado na hasira kali alibebwa mzegamzega na kufikishwa ofisini. Ofisi ya mkuu wa shule. Akafungiwa humo.

Ni huku macho yake yakakutana na picha ya yule dada aliyetoka kumjeruhi vibaya pale nje.

Kumbe ile sura aliyodhani aliwahi kuiona mahali, mahali penyewe ni katika ofisi ya mkuu wa shule juma moja lililopita alipokuja kuandikishwa kama mwanafunzi mgeni.

SIKU HIYO hapakuwa na jingine la kutetemesha kijiji zaidi ya jina la Keto. Keto alitajwa kila mahali kwa kitu alichomfanyia dada mkuu wa shule hiyo.

Hata ulipojili wakati wa kuipokea shule ya msingi Namvura kutoka Makambako iliyokuja kwa ajili ya michezo, bado stori ilikuwa ileile, wageni walijikita zaidi katika kusimuliwa simulizi ile kwani hata wao walimfahamu vyema Jackline Mageta yule dada mkuu na ubabe wake.

Jackline alikuwa amefunzwa adabu na msichana ambaye kila mmoja alitamani kumjua kwa ukaribu zaidi. Kwa wakati huu walimtambua kwa jina moja tu la Keto.

“Bado wewe shoga…..na wewe watakudunda siku moja mwee!” msicha mmoja kutokea shule ya Namvura ya Makambako alimtania dada mkuu wao ambaye alikuwa mpole sana tofauti na Jack Mageta.

“Wee mi sigusi mtoto wa mtu, kwanza nataka nimwone huyo Keto sijui ili awe rafiki yangu anifundishe mbinu.” Naye alijibu kimasihara, mambo mengine yakaendelea.

Majira ya jioni mzee mmoja akiwa anaikokota baiskeli yake alikuwa akimlaumu msicha mwembamba huku wakiongozana kuelekea nyumbani.

“Sawa amekutukania mama yako, lakini ulipompiga hayo matusi yamemrudia eeh!!” mzee alilalamika kwa sauti iliyoonyesha upendo. Msichana hakujibu zaidi ya kuendelea kulia kwa kwikwi.

Msichana mwembamba alikuwa amefukuzwa shule rasmi bila mjadala wowote.

Aliondoka akiwa ameukomesha ubabe wa Jack Mageta.

****

MAKAMBAKO

Wanafunzi wakiwa kimya darasani, kilikuwa kipindi cha somo la Baiolojia na mwalimu alikuwa mkali sana. Hodi ikasikika kutokea mlangoni.

“Nani wewe unayekuja darasani muda unaotaka….” Ilihoji kwa fujo sauti ile.

“Mi mgeni…”

“Mgeni? Mgeni nd’o hajui kama kuna kuwahi. Piga magoti hapo nje.” Alikoroma, wanafunzi kadhaa wakaguna. Mwalimu Simba akawageukia.

Ndani ya dakika saba darasa zima kasoro msichana mmoja tu aliyepona, wengine wote walikuwa wameoga fimbo za mgongoni.

“Na wewe nenda ukaniletee uthibitisho wa ugeni wako, mtafute dada mkuu akupe maelezo upesii.” Wanafunzi wakacheka, safari hii hakujali yule mwalimu kwani alijua kwanini wanacheka.

Yule msichana aliyekuwa amepiga magoti nje akasimama upesi na kuanza kurandaranda, tayari aliiona hatari ya mwalimu yule.

Ilikuwa kama bahati, akakutana na mwanafuzi aliyeagizwa chaki ofisini. Akamsimamisha na kuulizia darasa analosoma dada mkuu. Akaelekezwa!!

Akastaajabu kuwa ni darasa lile lile alilokuwa ameomba ruhusa ya kuingia mwanzo. Hata alipokutana na mwanafuzi mwingine na kuelekezwa darasa lile lile alirejea na msimamo wa liwalo na liwe. Akaugonga tena mlango.

“Dada mkuu yupo wapi?” ilihoji sauti ile.

“Nimeambiwa anasoma humu mwalimu….” Darasa likacheka tena.

“Dada mkuu!!” sauti ile ikaita. Yule msichana aliyenusurika kuchapwa fimbo za mgongoni akasimama, akatembea kwa maringo kama ilivyo kawaida yake. Blauzi yake safi na sketi iliyonyooshwa na soksi zinazowaka. Nywele ndefu zilizopakwa mafuta vizuri. Hakika alipendeza kumtazama.

Akaruka miguu ya wanafunzi wanyonge walioketi chini na kwenye matofali. Akamuaga mwalimu kisha akatoka nje kwenda kuonana na huyo aliyedai ni mwanafunzi mgeni.

“Wewe…ndi…..” hakuweza kuendelea na kauli yake, macho yake yakanata katika uso wa yule mwanafunzi mgeni, mwembamba na asiyekuwa nadhifu. Wakazidi kutazamana kwa mshangao wa aina yake. Hawakuwa wakifananishana tena, japo dada mkuu alikuwa anasita kubashiri kama ni kweli ama la! Lakini msichana mwembamba tayari moyoni alikuwa amekiri kuwa huyu ndiye.

“Joy….Joyce……” aliita kwa kusitasita.

“Betty!!!!!” msichana mwembamba hatimaye alitokwa na neno hilo.

Wakakaribiana, Joyce akamezwa na mikono ya Betty ambaye alikuwa na mwili mkubwa kiasi. Lile joto la miaka kadhaa nyuma wakiwa wanafunzi wa shule ya msingi visiwa vya Ukala wilaya ya Ukerewe. Joto likatambaa katika miili yao. Lilikuwa joto la upendo, tena ule upendo wa dhati isiyofichika.

Kilichofuata baada ya joto la upendo ni kilio ambacho kwa kila mmoja kilianza kama machozi pekee kisha kwikwi na hatimaye wakaharibu utulivu wa darasa. Wakaugulia kwa sauti za juu na hakutakiwa mtu kuwanyamazisha maana hakuna aliyeijua sababu.

Yule Joyce aliyempigania marehemu mama yake Betty kwa kujitolea damu ili aweze kupona sasa alikuwa mbele ya Betty. Rafiki wa dhati ambaye alionekana kuwa katika muonekano ambao kidogo ulitia matumaini. Lakini yule Joyce, masikini kutoka Ukala alizidi kukondeana na kuonekana mdogo sana.

Darasa halikuendelea, wanafunzi wakaanza kuchungulia madirishani, waalimu wakatoka nje.

Wakabaki kuwatazama jinsi walivyolia huku wakiwa wamekumbatiana. Dada mkuu Betty, alimwongoza Joyce hadi chini ya mti. Hatimaye wakasimuliana yote yaliyotokea, Betty hakuwa na jipya sana maana kifo cha mama yake kwa ajali ya meli kilikuwa kinafahamika. Lakini upande wa Joy ilikuwa zaidi ya simulizi nzito sana hadi kufika hapo alipo kwa dakika ile.

”Joy inaniuma sana sikuweza kumuona mama kwa mara ya mwisho…. Ziwa Viktoria liliamua kunipa uchungu wa milele…lilimmeza mama yangu, na halikutaka kumtapika tena.” Aliongea huku akibubujikwa na machozi.

Ni heri yeye alijua ni jinsi gani mama yake alipoteza uhai. Ama anajitambua kwa nini ni yatima…….

Laiti angejua kuhusu upande wa Joyce!!!!.....

Simulizi ya Joyce Kisanga ilianzia siku ambayo alikuwa amemaliza mitihani na anatarajia kusafiri kwenda Mwanza siku inayofuata.

Akafumba macho na kuanza kusimulia kama kwamba vile anavyosimulia vipo katika giza lipatikanalo macho yakiwa yamefumbwa. Ilikuwa simulizi inayotisha sana na kw yeyote mwenye moyo wa nyama angeguswa.

***HATIMAYE JOYCE na BETTY wamekutana tena katika mkoa mwingine pia katika wajihi mwingine……Je urafiki huu utaendelea kuvuma????

**JOYCE ana simulizi gani hiyo iliyomfanya afike Makambako?? Katika shule ya msingi hiyo….

***NINI HATMA YA ELIMU ZAO…..

ITAENDELEA JUMAMOSI..

***BOFYA LIKE NA SEMA CHOCHOTE JUU YA SIMULIZI HII

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top