KOCHA Mkuu wa klabu bingwa ya soka Tanzania na Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC, Mholanzi Ernie Brandts amerejea nchini wiki hii kutoka kwao Uholanzi, alipokuwa kwa mapumziko mafupi baada ya kumaliza msimu.
Baada ya kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, nilipata fursa ya kufanya naye mahojiano na miongoni mwa aliyozungumza kuelekea msimu ujao katka suala la maandalizi yake, ni kuhusu Uwanja mzuri wa mazoezi.Aliwataka viongozi wa Yanga SC wajitahidi kumpatia Uwanja mzuri wa mazoezi na baada ya hapo watafurahia timu.
Yanga kwa sasa wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa kukodi wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam ambao si mzuri, hivyo ndivyo unavyoweza kusema na wanalazimika kufanyia hapo, kwa sababu Mholanzi huyo ameona hapo ni nafuu kulinganisha na sehemu nyingine ambazo wamekuwa wakienda.
Katika mipango ya muda mrefu, tunafahamu Yanga wanataka kujenga Uwanja wa kisasa ulipo Uwanja wao wa sasa ambao umeharibika kwa kukosa matunzo, Kaunda maeneo ya Jangwani, makao makuu ya klabu yao.
Natambua kuna watu Yanga hawapendi kuambiwa ukweli Yanga- na ukithubutu kufanya hivyo wanakuchukia mpaka basi- kwa Bin Zubeiry mimi watanuna na kuvimba mpaka wapasuke, lakini ukweli kama dawa naamini ndiyo tiba yao na nitaendelea kuwapa.
Yanga SC ni klabu kubwa na haiyumkininiki eti Dar es Salaam nzima imekosa sehemu ya kuwekeza Uwanja wa mazoezi tu, bali nachokiona hapa, watu waliopewa dhamana ya klabu bado hawajatekeleza majukumu yao ipasavyo.
Pengine kutokana na kutotaka tu kufanya hivyo, au wigo wa uelewa wao katika soka kwamba, baada ya ubingwa wa Bara na kumfunga Simba SC basi wamemaliza- kumbe wanasahau wana jukumu la kuitengenezea misingi imara klabu.
Mabadiliko katika Yanga SC hayatamaanishwa na aina ya viongozi tu, kutoka hohe hahe hadi wenye uwezo wa kifedha, bali pia na kwa hatua za kimsingi za kimaendeleo ambazo klabu inafikia siku hadi siku.
Narudi nyuma kidogo mwaka 2007 wakati Yanga SC ipo chini ya Mwenyekiti Wakili Imani Omar Madega na Makamu wake, Rashid Ngozoma Matunda (sasa merehemu) na leo ikiwa inaongozwa na Milionea Yussuf Mheboob Manji Mwenyekiti na Makamu wake, Clement Sanga, hakika sioni tofauti.
Magari yote ya timu yametoka kwa wadhamini wa timu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na timu bado inahaha kuazima viwanja vya kufanyia mazoezi. Jengo la makao makuu lipo vile vile kama alivyoliacha Madega.
Sijui kuhusu akaunti ya klabu ina nini kwa sasa, maana haijawahi kuwekwa wazi na uongozi huu, lakini wakati mwezi ujao Manji na timu yake ‘Jeshi la Miamvuli’ aliyoingia nayo mdarakani watatimiza mwaka mmoja, bado kwa kweli hadhi ya klabu haijabadilika.
Hadhi ya klabu si tu kusajili wachezaji wa fedha nyingi au kupeleka timu kambini Ulaya wakati hauna hata Uwanja wa mazoezi, huu ni ufahari wa kuweka fenicha za gharama katika nyumba ya kupanga, wakati mwenyewe hauna hata kiwanja cha kusema siku moja utakuwa na nyumba yako japo ya ‘ mbavu za mbwa’.
Yanga imekwishafanya ziara Brazil enzi za Tarbu Mangara (sasa marehemu) miaka ya 1970 nini Uturuki na ilikuwa inasajili wachezaji wazuri tangu miaka ya 1940 na kushinda mataji pamoja na kufika mbali katika michuano ya Afrika. Hakuna kigeni katika hayo.
Wanachama na wapenzi wengi wa Yanga hawajui tu, kuna watu wanapenda kutumia udhaifu wa klabu yao kujipatia umaarufu na kutengeneza majina kesho wakatimize malengo yao mengine kwa mgongo wa klabu.
Sitaki kuamini viongozi wa sasa wa Yanga ni wa aina hiyo, lakini pia na wao wana wajibu wa kuwaonyesha watu kwamba wao si watu wa aina hiyo kwa kufanya mambo yenye manufaa na mustakabali mzuri kwa klabu.
Pale Kaunda wanataka kuporomosha Uwanja wa kisasa na mchakato umeanza, tuombe Mungu yatimie, lakini kwa sasa katika hili tatizo la msingi la klabu kukosa Uwanja mzuri wa mazoezi hadi kocha analalamika, wanafanyeje? Hilo ndilo swali la msingi.
Nafahamu kuna maeneo nje kidogo tu ya mji ni tulivu, ardhi nzuri, Yanga SC wanaweza kununua kwa gharama isiyozidi Sh. Milioni 100, wakakarabatri na kuotesha nyasi kisha kupata Uwanja mzuri wa mazoezi. Yapo.
Tena wakijenga vizuri, wakaweka uzio na kuweka sehemu za watu kutulia watazame maeozi, fedha walizotumia zinaweza kurudi kwa muda mfupi tu kutokana na viingilio. Watu wanaifuata Yanga hadi Mwanza watashindwa kuifuata Mwasonga, Kisarawe ama Mlandizi au Bunju kuiangalia ikifanya mazoezi katika uwanja wake mzuri?
Pamoja na ujenzi wa Uwanja mpya wa kisasa wa Kaunda, lakini Yanga wakipata Uwanja mwingine wa mazoezi watakuwa wamefanya uwekezaji mzuri kwa manufaa ya klabu na historia itawakumbuka viongozi wa sasa daima.
Kuwekeza Sh. Milioni 300 kwa wakati mmoja kwa ajili ya kupata Uwanja wako mwenyewe ni tofauti sana na kila siku kutumia Milioni japo moja kwa Uwanja wa kukodi.
Viongozi wa Yanga SC wajue kwamba, kwa vyovyote wafanyavyo kama watakuwa hawana japo Uwanja mzuri tu wa mazoezi, angalau usio na uzio, bali pitch nzuri tu, watakuwa wanaonyesha jinsi ambavyo hawaisaidii klabu kwa mustakabali wake.
Na umefika wakati sasa tuwe na aina ya viongozi ambao watabadilisha hisia za mashabiki kwa kuwaonyesha mlengo mpya wa klabu, ili siku moja wajivunie kupenda kitu chenye mafanikio na siyo kilichodumaa.
Leo unakutana na shabiki limbukeni, anatamba eti viongozi wa Yanga wana magari mazuri na matajiri, ndiyo wanayo na tunajua ni matajiri kwa sababu wengi wao ni wafanyabiashara wakubwa, lakini wanainufaishaje klabu?
Yanga ina uwezo wa kujiendesha yenyewe iwapo uongozi utaamua kuiendesha kibiashara na si kuwa klabu ambayo siku moja kiongozi mmoja akiamka na kusema yeye Yanga basi, klabu inaporomoka mara moja.
Katika mechi yao dhidi ya Simba Mei 18, Uwanja ulisheheni na kwa haraka robo nzima ya watu waliokuwapo Uwanja wa Taifa walikuwa wamevaa jezi za Yanga walizonunua zikiwa na nembo ya klabu, je nani ananufaika na mauzo ya hizo jezi?
Bado kuna maeneo mengine kadhaa Yanga inaweza kuchuma fedha kupitia nembo yake, ambayo viongozi waliotangulia pamoja na ‘ufukara’ wao walifanya jambo la maana kuisajili, lakini je yanatumikaje?
Na ni hadi lini tutaendelea kuimba nyimbo zile zile, lakini Yanga wenyewe hawabadiliki?
Hivi wana Yanga wanajua kwamba mfumo ambao klabu yao inaendeshwa kwa sasa siyo salama? Leo wana Yanga wanatembea kifua mbele Manji yupo pale, akiondoka watampata Manji mwingine lini?
Wamesahau enzi zile za mabakuli kutembezwa jukwaani ili timu ichangiwe fedha za japo wachezaji kupata posho? Wapo matajiri waliomtangulia Manji Yanga, lakini kwa sababu hawakufanya kitu kwa mustakabali wa klabu, bali kutoa fedha kusajili na kufanya mambo mengine ya kifahari Yanga SC ilirudia tena kwenye hali ngumu kabla ya kuokolewa na Manji.
Sasa mwezi ujao, Manji na timu yake wanatimiza mwaka mmoja, lakini hadi leo klabu haina japo Uwanja wa mazoezi tu, hizi si dalili nzuri. Tuombeane uzima inshaallah, tutakutana tena Jumatano Mungu akipenda, hapa hapa
CREDIT TO BINZUBER