Unknown Unknown Author
Title: CECAFA CHINI YA MUSONYE SAFARI KUELEKEA KUZIMU, NA TENGA YUPO PALE PALE
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
KLABU za Tanzania hazitakwenda kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame inayofanyika kuanzia w...

KLABU za Tanzania hazitakwenda kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame inayofanyika kuanzia wiki ijayo mjini Kigali, Rwanda.
Hiyo inafuatia kukanganywa na taarifa za Serikali, awali ikizizuia kwenda kwa sababu kuna machafuko, na baadaye ikiziruhusu kwenda baada ya kuhakikishiwa usalama wa klabu hizo na Serikali ya Sudan.
Iliziruhusu jana, wakati mashindano yanaanza Jumanne na hazijafanya maandalizi yoyote ya safari. Kana kwamba hiyo haitoshi, baada ya zuio la awali, CECAFA (Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati) likateua timu mbadala kuziba nafasi ya timu tatu za Tanzania.
Timu za Tanzania zilizotarajiwa kushiriki michuano hiyo ni Simba SC, Yanga za Dar es Salaam na Super Falcons ya Zanzibar.
Inafahamika vyema, ustawi wa timu za taifa za nchi unatokana na klabu imara zinazoshiriki mashindano na kuwapa uzoefu na changamoto wachezaji wake.
Kwa nchi zetu za ukanda wa CECAFA, ambazo klabu zake hazipati fursa ya kushiriki na kufika hatua za mbali katika michuano ya Afrika kama Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa, michuano hii ya Kagame bado ni muhimu sana kujipima baina yetu.
Ni fursa ya wachezaji kutambuana baina yao- kufahamu hali halisi ya soka ya nchi nyingine katika ngazi ya klabu kwa ukanda wetu na pia kudumisha ushirikiano baina yetu.
Sidhani kama CECAFA wanalitambua hilo. Nasema hivyo kwa sababu, michuano hii ya Kagame imekuwa ikiendeshwa kwa ubabaishaji wa hali ya juu na haipo katika utaratibu mzuri kama ule uliokuwapo awali.
Hadi mashindano yanakaribia kufanyika, watu hawajui yatafanyika wapi. Nchi moja inaweza kupewa uenyeji mfululizo. Taratibu haswa za mashindano hazieleweki.
Na tatizo halipo hapa tu kwenye Kagame, bali ni michuano yote ya CECAFA kuanzia ya vijana hadi ya timu za taifa za wakubwa, Challenge mambo ni shaghalabagala.
Miaka ya nyuma hii michuano ya Kagame ilikuwa ina tija sana, kwa sababu kwanza ilikuwa inafanyika mwanzoni mwa mwaka, timu zinapata fursa ya kujiandaa kwa ajili ya michuano mikubwa ya Afrika- pili ilikuwa ndani ya utaratibu maalum, ulioitengenezea hadhi ya kiushindani.
Lakini leo inaonekana wazi michuano hii imepoteza heshima yake ile iliyokuwa nayo enzi zile akina Abdallah Kibadeni, Sunday Manara wanacheza kabla ya akina Zamoyoni Mogella, Said Mwamba ‘Kizota’, Mwameja Mohamed na Manyika Peter.  
Namheshimu sana Leodegar Tenga, rais wa CECAFA na nilikuwa shabiki wake wakati anacheza ‘mkoba’ pale Pan Africans na Taifa Stars. Nilifurahia kuingia kwake madarakani TFF na CECAFA pia.
Lakini nashindwa kujizuia kumkunjia ndita kutokana na jinsi ambavyo mambo yanakwenda shaghalabagala CECAFA na TFF chini yake, yeye akiwa kiongozi wa juu wa vyombo vyote hivyo.
Tatizo moja ambalo nimegundua kuhusu Tenga baada ya kumsoma kwa takriban miaka 10, ni kwamba anawaamini watu kupita kiasi na hata wanapoharibu, kwanza huwatetea, tena kwa nguvu zake zote, hata kama ndani kwa ndani wanasuguana.
Hii ndiyo ipo pale TFF na ndivyo ilivyo hata kwa CECAFA pia, Tenga amemuamini kupita kiasi Katibu wake Nicholas Musonye na ndiye anayeharibu kabisa soka ya ukanda huu.
Musonye ni mtu wa ajabu sana anafanya madudu, ni jeuri na asiyejali. Mwaka jana pale Kampala, Uganda nilistaajabu sana walipompa mchezaji wa Uganda ufungaji Bora wa Challenge wakati alizidiwa kwa mabao na wachezaji wa Tanzania.  
Sasa rejea kwenye hii michuano ya Kagame mwaka huu, haikustahili kufanyika Sudan, ambako kila siku tunasikia watu wanauawa kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, lakini kwa sababu zake mwenyewe Musonye ameamua kuipeleka huko.
CECAFA haina mipango, dira wala mikakati ya kuendesha mambo yake na hilo ndilo tatizo kubwa, mwisho wake kinageuka kuwa chombo mzigo tu ambacho nafuu kisingekuwapo.
Mungu amejaalia katika ukanda wetu hivi sasa kuna makampuni mengi yanayojiendesha kisasa, yanayojua umuhimu wa kujitangaza kupitia mchezo unaopendwa na wengi, soka. Lakini ajabu CECAFA imeshindwa kujifunga kwa ndoa za kudumu na makampuni, kwa sababu tu haijui hata inapolalia na haijui itaamkia wapi. Mambo ni bora liende.
Tunataka kusikia CECAFA inaingia Mkataba wa Miaka mitano na makampuni kwa ajili ya michuano fulani- na wakati tunaingia kwenye michuano ya mwaka huu, tuwe tayari tunajua michuano ya mwakani itafanyika wapi.
Musonye amekalia fitina za kupanga safu za uongozi tu pale CECAFA ili kutafuta watu wa kumlinda aendelee kuwa Katibu wa CECAFA, wakati hakuna cha maana anachokifanya zaidi ya kuigeuza CECAFA kama chombo cha Wakenya pekee.
Mwaka jana niliona jarida la CECAFA limeandaliwa na timu ya Waandishi wa Kenya, ni utumbo mtupu. Wameandika kwa usahihi kuhusu Kenya tu, lakini nchi nyingine wameboronga ile mbaya. Hili lingeweza kuepukika kama CECAFA ingeshirikisha Waandishi wa nchi zote za ukanda huu, lakini kwa ubinafsi wa Musonye wamefanya madudu kwa bajeti kubwa.
Boniface Wambura ni Ofisa Habari wa TFF amekuwa akiandika habari za soka tangu miaka ya 1990, angeweza kuandika vizuri na kwa usahihi kuhusu Tanzania, lakini Mkenya mmoja kaandika mafyongo tu.
Yaani kwa ujumla CECAFA chini ya Musonye ni safari kuelekea kuzimu na iwapo Tenga hatabadilika na kujitoa moja kwa moja kusimamia soka ya Ukanda huu, mambo yataharibika zaidi.   Wikiendi njema.

MAKALA KWA HISANI YA BINZUBER

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top