Title: SEHEMU YA TAARIFA YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU GESI BUNGENI.
Author: Unknown
Rating 5 of 5
Des:
3.4 BOMBA LA GESI TOKA MTWARA HADI DAR ES SALAAM Mheshimiwa Spika, Pamoja na ushauri wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wakati wa kuwasili...
3.4 BOMBA LA GESI TOKA MTWARA HADI DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Spika, Pamoja na ushauri wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wakati wa kuwasilishwa kwa bajeti ya wizara 2012/2013 kuitaka Serikali kuwasilisha Bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika ili Bunge liweze kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63; kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya Taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa lakini bado serikali haikutilia maanani ushauri huu. Matokeo yake siyo tu kusababisha mkanganyiko kwa wakazi wa Lindi na Mtwara bali pia kuacha maswali mengi kwa watanzania juu ya nini hasa nia ya serikali kwa kuficha mikataba inayohusu rasilimali hizi za Taifa kwa wananchi wake na hata kwa chombo cha kuwakilisha wananchi kama Bunge.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA inaitaka Serikali isiendelee na ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar Es Salaam hadi kwanza; Mosi, iweke wazi kwa Bunge mikataba yote inayohusu uendelezaji wa gesi asilia ikiwemo ya ujenzi wa Bomba hilo. Pili, ikutane na wananchi kuwashirikisha na kuhakikisha manufaa kwa taifa na kwao.
Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na CHADEMA imeshangazwa na hatua ya Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo tangu kuibuka kwa mgogoro huo amejikita zaidi katika kutoa kauli kupitia vyombo vya habari badala ya kwenda kukutana na wananchi hatua kwa hatua na kuwezesha ufumbuzi kupatikana. Aidha, manufaa kwa wananchi wa Lindi na Mtwara ambayo taarifa yake imechapwa kwenye vyombo vya habari yaletwe kama taarifa rasmi bungeni ikiwa na ulinganisho baina ya shughuli za kijamii zilizofanywa na makampuni tajwa pamoja na miradi iliyotekelezwa na Serikali kufuatia mapato katika sekta hii tangu mwaka 2004 na thamani halisi ya mapato ambayo makampuni tajwa na Serikali wamepata.
Mheshimiwa Spika, pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo, Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Serikali kueleza ni miradi ipi iliyotengewa fedha inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na imetengewa kiasi gani cha fedha katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 ili kuharakisha msukumo wa maendeleo kwa mikoa hiyo ya Kusini ambayo imesahaulika kwa siku nyingi na hivyo siyo tu kuharakisha maendeleo kwa mikoa ya Kusini bali pia kuhakikisha usalama wa mradi huo mkubwa kwa manufaa mapana ya jamii ya kitanzania.
Mheshimiwa Spika, kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia pamoja na bomba la kusafirisha gesi hiyo hadi Dar es salaam na usambazaji wa umeme katika vijiji 52 vinavyopitiwa na bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Lindi haikidhi wala kujibu kilio cha wananchi wa Mtwara na Lindi cha kutaka ugunduzi wa gesi asilia katika mikoa hiyo uweze kunufaisha mikoa hiyo kimaendeleo kutokana na kuwa nyuma kimaendeleo miaka 52 baada ya uhuru wa Taifa hili.
Mheshimiwa Spika, wakati waziri akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ya Wizara ya Nishati na Madini tarehe 27-07-2012 aliliambia bunge hili kuwa, kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya Tanzania na China kwa ajili ya kusafirisha Gesi asili na ujenzi wa Bomba la kusafirishia gesi toka Mnazi BAY hadi Dar es saalam na kusainiwa kwa mikataba mingine mitano (5) na mkataba wa uzalishaji na ugawanyaji wa mapato ya mafuta na Gesi asili kuwa ni miongoni mwa jitihada ambazo serikali imechukua katika jitihada za kukabiliana na tatizo sugu la umeme hapa nchini, hata hivyo kama ulivyo utaratibu wa serikali mikataba hii inaendelea kuwa siri.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali na Wizara ya Nishati na Madini kuainisha miradi hiyo na kuitengea fedha ili wananchi wa mikoa ya kusini waweze kunufaika na rasilimali hiyo kwani kwa muda mrefu sana wamekuwa wavumilivu wakisubiria utekelezwaji wa ahadi za kuwapelekea maendeleo kwa miaka mingi bila kuyaona wala kuyapata.
Kambi rasmi ya Upinzani , inaitaka serikali isitishe ujenzi wa Bomba hilo kwanza iende ikajadiliane na wananchi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani na wakubaliane jinsi ya kuendelea na mradi huo ndipo ujenzi wa bomba hilo uweze kuendelea , kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeamua kumaliza tatizo la msingi kwani serikali ikiendelea bila kujali madai ya wananchi hawa na kuamua kutumia mabavu kujenga hakuna atakayekuwa mshindi kati ya serikali na wananchi hawa. Ni rai yetu kuwa serikali itaweza kuiona busara hii ili gesi iweze kuwanufaisha watanzania wote yaani wa Mtwara na wale wa maeneo mengine.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.