Kikosi cha Young Africans kilichoanza leo dhidi ya Armini Bielefeld
Timu ya Young Africans Sports Club imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani katika mchezo wa kirafiki uliofanyika leo jioni katika uwanja wa Adora Football pemebni kidogo ya mji wa Antalya. Armini Bielefeld ilianza soka kwa kasi kwa lengo la kujipatia bao la mapema lakini umakini wa walinzi wa Yanga na mlinda mlango Ally Mustafa 'Barthez' ilikuwa kikwazo kwao kwani mashambulizi yao yaliishia mikononi mwake.
Ikiwa ni mchezo wake wa kwanza wa kujipima nguvu Young African iliweza kuonyesha soka safi katika kipindi cha kwanza hali iliyowashangaza wajerumani hao na kipindi cha pili kuamua kufanya mabadiliko ya kikosi kizima.
Viungo wa Yanga Frank Domayo, Haruna Niyonzima na Kabange Twite waliweza kutawala mchezo kwa dakika 45 zote za kipindi cha kwanza huku baadhi ya wajerumani waliokuwa wakishuhudia mchezo huo kushangazwa na kiwango cha timu ya Yanga
Hadi mapumziko timu zote zilikwenda mapumziko , Young Africans 0 - Arminia Bielefeld.
Kipindi cha pili Arminia Bielefeld iliamua kubadilisha kikosi chake chote cha wachezaji kwa lengo la kuingiza nguvu mpya ili waweze kuikabili kasi ya wachezaji wa Yanga ambao walionekana kuwa imara na bora zaidi.
Dakika ya 55 Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Said Bahanuzi na David Luhende na nafasi zao kuchukuliwa na Jerson Tegete na Saimon Msuva.
Jerson Tegete aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 60 ya mchezo, akiunganisha pasi safi aliypewa na Saimon Msuva aliyewatoka walinzi wa Arminia Bielefeld na kumpa pasi Tegete ambaye aliukwamisha mpira wavuni na kuhesabu bao la kwanza.
Kuona hivyo wajerumani walikuja juu kusaka bao la kusawazisha, lakini bado ukuta wa Yanga uliendelea kuonekana kuwa makini lakini makosa ya mshika kibendera yaliipelekea Armini Bielefeld kupata bao la kusawazsiha dakika ya 81 kupitia kwa Eric Agyemang amabaye alikua ameotea.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika Young Africans 1 - 1 Armini Bielefeld.
Kocha Mkuu wa Young Africans Ernest Brandts amesema amefurahishwa na kiwango walichokionyesha wachezaji wake na anaamini kadri siku zinavyokwenda wanazidi kuimarika na kuwa bora, hivyo katika michezo mingine wataendelea kuonyesha mabadiliko makubwa.
Young Africans: Ally Mustafa 'Barthez, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Kabange Twite, Haruna Niyonzima/Nizar Khalfan, Frank Domayo/Nurdin Bakari, Said Bahanuzi/Jerson Tegete, Didier Kavumbagu, David Luhende/Saimon Msuva