AFYA za wakazi na wafanyabiashara wanaotegemea soko la wapiwapi wilayani Masasi mkoani Mtwara zimo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu kutokana na kuwepo kwa mlundikano mkubwa wa taka ngumu katika eneo la soko hilo zilizo dumu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Bahadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na mtandao huu jana kwenye eneo hilo la soko hilo walisema kuwa kutokana na hali hiyo ya kuwepo kwa mlundikano wa takataka ngumu ambazo zimezagaa kandokando ya soko hilo kunawafanya wafanyabiashara na walaji kuwa katika hali ya hatari ya kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu jambo linalohatarisha afya zao hasa kipindi hiki cha masika ambapo takataka hizo hunyeshewa mvua na kusababisha kutoa harufu mbaya.
Walisema kuwa ili kuokoa hali ya kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa, wafanyabiashara hao wameiomba halmashauri ya mji Masasi kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha takataka hizo zinaondolewa ili kuyaweka mazingira ya soko hilo kuwa katika hali ya usafi tofauti na yalivyo hivi sasa na kwamba hali hiyo pia inaweza kuwa athiri hata wateja wanaokwenda kununua bidhaa katika soko hilo, hatua ya utupaji wa takataka katika eneo hilo umewashangaza wafanyabiashara hao na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwa kuwa eneo hilo sio maalumu kwa utupaji wa takataka.
Wakizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzao katika soko hilo, Siajabu Namadi, Hamisi Saidi walisema kuwa kwa sasa eneo hilo limekuwa likitumika kwa utupaji takataka na baadhi ya vibarua wa halmashauri ya mji pindi wanapozikusanya kutoka katika maeneo mbalimbali wilayani humo ikiwemo kutoka stendi kuu ya mabasi.
Walisema kuwa kuwepo kwa mlundikano huo wa takataka ambazo zimezagaa kando ya soko hilo kuna hatarisha afya kwa wafanyabiashara wa soko hilo na kwenda hali hiyo ikasababisha kuibuka kwa magonjwa mbalimbali ya mlipuko iwapo halmashauri hiyo isipo chukuwa hatua za makusudi kuziondoa takataka hizo.
Saidi alisema kwamba halmashauri hiyo inapaswa kuangalia namna ya kutafuta eneo lingine ambalo litakuwa maalumu kwa ajili ya utupaji wa takataka badala ya kuendelea kuzitupa katika eneo la soko hilo kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchafua mazingira na kwamba hali hiyo inahatarisha afya kwa wafanyabiashara wanoendesha shughuli zao katika eneo hilo na hata kwa wakazi waishio katika eneo hilo.
“Tunaiomba halmashauri ya mji ifanye kila jitihada ili kuziondoa takataka hizi kwani hii ni hali ya hatari na kwamba ni uchafuzi wa mazingira hivyo lazima kuangalia uwezekano wa kutafuta eneo husika ambalo litakuwa maalumu kwa ajili ya utupaji wa takataka hizi…kwa nini wanatupa takataka kwenye eneo hili ebu mwandishi angalia hali ya mazingira ilivyo kwakweli ni mbaya,”alisema Saidi
Kwa upande wake katibu wa soko hilo Bakari Ismail alisema kuwa suala hilo la mlundikano wa takataka katika eneo la soko hilo amelifuatilia kwa mara kadhaa kwa uongozi wa halmashauri ya mji ili kushinikiza halmashauri hiyo kuziondoa takataka hizo na kuacha kuendelea kutupa katika hilo.
Alisema licha ya kufuatilia suala hilo kwa uongozi wa halmashauri ya mji amekuwa akipewa majibu kwamba tayari kuna mzabuni ambaye amekabidhiwa kufanya kazi hiyo ya ukusanyaji wa takataka katika maeneo mbalimbali ya mji na kwamba mzabuni huyo ameahidi kuanza kufanya kazi wiki hii.
“Nimefuatilia mara nyingi juu ya suala la mlundikano wa takataka katika eneo hili la soko ili kuhakikisha takataka hizi zinaondolewa kwa sababu kuna uwezekano wa kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa ya mlipuko ambao waathirika wakubwa hapa ni wafanyabiashara waliyopo katika soko hili majibu tunayopewa ni kwamba tayari kazi hiyo ameshapewa mzabuni ili kuziondoa taka hizo,”alisema Ismail
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Masasi, Mohamedi Nanyanje alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la mlundikano wa takataka na kudai kuwa tatizo hilo limesababishwa na kuwepo kwa changamoto ya uchache wa magari ya kuzolea takataka na hata lililo kuwepo kwa sasa lina matatizo ya matairi kwa muda mrefu jambo lililosababisha zoezi la ukusanyaji wa taka kusimama kwa zaidi ya wiki mbili na nusu hali iliyopelekea kuwepo kwa mlundikano huo wa takataka.
Alisema kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo la mlundikano wa takataka katika maeneo mbalimbali ya mji halmashauri hiyo iliamua kuipa tenda kampuni ya SHUU Enterprise ya wilayani humo kwa ajili ya kuanza kuzoa takataka ambazo zimelundikana katika maeneo ya mji ili kuuweka mji huo katika hali ya usafi.
“Tayari tumeshampa mzabuni ili aanze kukusanya takataka zote zilizolundikana maeneo mbalimbali hasa kuanza soko kuu lilipo maeneo ya mkuti hadi zile zilizopo katika soko la wapiwapi la soko sela na kwamba tayari ameshaanza kufanya kazi hiyo kwa kuanza na zile za soko la mkuti na baadaye atakwenda katika soko hilo la wapiwapi,”alisema Nanyanje
UCHAFU MASASI
Title: UCHAFU MASASI
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
AFYA za wakazi na wafanyabiashara wanaotegemea soko la wapiwapi wilayani Masasi mkoani Mtwara zimo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko ...