Unknown Unknown Author
Title: POLISI YAZIMA MAANDAMANO YA KUMNG’OA RC MTWARA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
POLISI wilaya ya Mtwara imeyazima maandamano ya wakazi wa mkoa huo ya kumuondoa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia kut...
kanalijosephsimbakalia[1]POLISI wilaya ya Mtwara imeyazima maandamano ya wakazi wa mkoa huo ya kumuondoa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia kutokana na kauli zake za kuwaita wapuuzi na wahaini wananchi hao walipoandamana kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Mtwara jana, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa vyama vya siasa vya upinzani mkoani hapa, Uledi Abdallah alisema polisi imekataa kutoa kibali cha kuruhusu maandamano hayo.
Alisema kwa mujibu wa barua ya Januari, 15 mwaka huu kwa umoja huo, polisi imetoa sababu tatu za kuzuia maandmano hayo ikiwa pamoja na hali tete ya usalama baada ya vurugu alizofanyiwa mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia na kufungwa kwa barabara katika kijiji cha Msimbati wakizuia kuingia kijijini hapo kwa kiongozi yeyote wa ngazi ya juu wa serikali.
Uledi alisema sababu ya tatu ni taarifa za kitelijensia kuonesha kuwa wananchi wameingiwa na hofu juu ya usalama wao hivyo askari wengi wametawanywa maeneo mbalimbali ya wilaya kuimarisha ulinzi na kwamba siku iliyokapangwa kwa ajili ya maandamano hayo polisi haitakuwa na askari kutosha kusimamia ulinzi.
“Sisi kama umoja tumekubaliana na taarifa ya polisi na tunatamka wazi kuwa maandamano yetu tuliyopanga kufanya Januari, 21, mwaka huu kuanzia Mikindani hadi Viwanja vya Mashujaa kwa ajili ya kumng’oa mkuu wa mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia tumeghairisha, hadi siku nyingine tutakapoyapanga” alisema Abdallah
“Lakini pia polisi imeturuhusu kuendesha mikutano ya adhara mitatu kuanzia Januari, 15, 17 na 20, katika maeneo ya Kokobichi, Mikindani na Sabasaba….tunalishukuru jeshi la polisi wilayani kwetu kwa kuonesha imani nasi” aliongeza

Akizungumzia tukio la Januari 13 mwaka huu ambapo mwnyekiti wa NCCR Mageuzi, Mbatia alinusurika kipido, Uledi alisema jambo hilo lilitendwa na vijana wachache ambao alidai walitumwa na watu maalum kwa ajili ya kuwaondoa wanamtwara kwenye ajenda ya gesi.
“Tumefanya utafiti na kubaini waliohusika ni vijana wachache ambao wametumwa na vyama ambavyo havipo kwenye umoja huu…lengo lao ni kutuondoa wana-Mtwara kwenye ajenda yetu…ionekane tumeanza kufanya vurugu” alibainisha Abdallah na kuongeza
“Tunamuomba radhi Mbatia kwa tukio hilo, ni changamoto kwetu kwa sababu waliofanya hivyo walikuwa na ajenda yao ya siri…asiogope kututembelea na kuhutubia wananchi…wananchi wengi wamefurahia hotuba yake na hawajaona sababu ya vurugu zile”
Mwenyekiti wa Chadema Mtwara mjini, Mustafa Nchia ambaye ni mjumbe katika umoja huo alisema amefadhaishwa sana na tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kuwa tayari kuwasikiliza viongozi hata kama hawakubaliani na watakayoongea.
“Sikiliza kwanza, kama unaona hukubaliani utafanya uwamzi kichwani mwako…tusionekane sisi ajenda yetu haikuwa gesi kunufaisha wana Mtwara bali vurugu” alisema Nchia
Naye mwenyekiti wa CHAUMA, Fatuma Selemani alisema madai ya wana-Mtwara yatabaki paepale hadi serikali itakapojishusha na kukubali matakwa ya wengi ya kujengwa kwa mitambo ya kufua umeme na kuhakikisha gesi inayosafirishwa ni ile iliyosindikwa kutoka mkoani humo.
“Sisi wanawake tukianza kudai talaka tunahakikisha unaachwa…gesi hii sio kwa ajili yetu, ni ya watoto, wajukuu na vitukuu…sio kazi rahisi kupigania maslahi ya wengi, hata Nyerere (Hayati Mwalimu Nyerere) alipigania uhuru kwa ajili yetu, leo tunafurahia uhuru lakini wapo walioumia na sisi tunapigania gesi ili watoto wafurahie matunda” alisema Selemani
Umoja huo unaundwa na vyama Tisa vya siasa ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi, SAU, TLP, APPT Maendeleo, ADC, VDP, CHAUMA na DP,













About Author

Advertisement

 
Top