Unknown Unknown Author
Title: JK: Uvumilivu sasa basi
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SERIKALI imesema haitavumilia kwa namna yeyote ile vurugu za kidini, kikanda na ukabila ambazo baadhi yake zilitaka kulitia doa taifa mwaka ...
SERIKALI imesema haitavumilia kwa namna yeyote ile vurugu za kidini, kikanda na ukabila ambazo baadhi yake zilitaka kulitia doa taifa mwaka jana.
Pia imesisitiza kwamba haitawavumilia wanasiasa wanaotumia rasilimali za taifa kujitafutia umaarufu kwa gharama za kuligawa taifa.
Akizungumza na mabalozi kwa nyakati tofauti Ikulu, Dar es Salaam; kwanza katika sherehe ya kuukaribisha Mwaka Mpya iliyofanyika juzi na alipokuwa akiagana na Balozi wa Uingereza nchini, Dianne Corner jana, Rais Jakaya Kikwete alisema vurugu zilizotaka kujitokeza mwaka jana zinatosha.
“Serikali haitavumilia vurugu wala ukabila kwa namna yoyote ile…. Mwaka 2012 vurugu zenye sura ya kidini zilianza kujitokeza ila sasa nasema kwamba hatutazivumilia kwa namna yeyote ile, inatosha,” alisema Rais Kikwete.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kiongozi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Juma Mpango alisema jumuiya ya mabalozi imefurahishwa na namna ambavyo Serikali imekuwa ikishughulikia vurugu za kidini ambazo zilitaka kujitokeza bila kusababisha madhara kwa wananchi.
“Tumeridhishwa na namna ambavyo Serikali imekuwa inashughulikia mambo yake vizuri. Tunaomba mwendelee kushughulikia amani ya nchi hii maana ndiyo mhimili wa nchi za Maziwa Makuu,” alisema Balozi Mpango.
Kuhusu gesiRais Kikwete alizungumzia suala la rasilimali za taifa na kusisitiza kuwa pia hatavumilia kuona wanasiasa wakitumia suala la gesi kujitafutia umaarufu.
Wakati Rais Kikwete akitoa kauli hiyo jana, habari kutoka Mtwara zilidai kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amewekewa magogo barabarani kumzuia asiende kwenye kijiji kinachozalisha gesi hiyo, huku Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Regina Chonjo akizomewa.
Hata hivyo, polisi walikiri wananchi kuweka magogo barabarani kwa lengo la kumzuia waziri huyo, lakini ikaeleza kuwa gari lililozuiwa siyo la Simbachawene.
Rais Kikwete alikemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia suala la rasilimali za taifa, ikiwamo gesi asilia kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kuwapotosha wananchi.
“Ni jambo la hatari na lisilo na tija kwa wanasiasa kujaribu kuigawa nchi vipandevipande kwa sababu ya kujitafutia umaarufu kwa kutumia rasilimali za taifa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Unawezaje kuwa na nchi moja na taifa moja wakati kila mmoja anadai rasilimali kutoka kwenye eneo moja ibakie na kunufaisha watu wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na yenye umoja wakati kuna nchi ya gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa kule Kilimanjaro, kuna nchi ya chai na ndizi kule Bukoba,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kwa sababu kama gesi asilia inatakiwa kubakia na kunufaisha watu wa Mtwara tu, basi wenye haki zaidi ya kudai jambo hili siyo watu wa Mtwara, bali ni watu wa Msimbati ambako ndiko ilipogunduliwa gesi ambako ni maili 60 kutoka Mtwara, kilomita 200 kutoka Newala.”
“Nchi yetu inao baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa umaarufu na ambao wanatumia jambo hili jema kwa manufaa yao binafsi, bila kujali umoja na jadi ya taifa letu la rasilimali zetu kutumika kuiendeleza nchi nzima.”
DC azomewa
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea na viongozi wawili wa CCM Mkoa wa Lindi; Mwenyekiti Albert Mnali na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, Fadhili Liwaka, juzi walijikuta katika wakati mgumu, baada ya umati wa wananchi waliohudhuria mkutano wake kuanza kumzomea alipowataka waache kuunga mkono mgogoro wa gesi.

“Serikali haina nia mbaya na wakazi wa Lindi na Mtwara, kinachofanyika ni kuipeleka hii gesi sokoni ili iweze kutumika kwa faida ya Watanzania wote kwani soko la gesi lipo huko inakopelekwa na ni sehemu ya mgawanyo wa rasilimali zetu za Taifa,” alisema DC Chonjo.
Zomeazomea ilianza baada ya kuwataka wananchi wa Nachingwea kutokujiingiza kwenye maandamano yanayoandaliwa hivi karibuni katika Miji ya Mtwara na Lindi kuishinikiza Serikali kuacha mpango wa kuhamisha gesi kwenda Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Chonjo alisema wakazi wa Nachingwea hawana sababu ya kushiriki migomo hiyo kwani tangu awali, wamekuwa wakitumia rasilimali zilizo nje ya wilaya na mkoa wao, akitaja baadhi kuwa ni umeme na Barabara ya Kibiti hadi Lindi ambayo ujenzi wake umetegemea rasilimali zilizotoka nchi mzima
Alizomewa baada ya kuruhusu maswali na mkazi aliyejitambulisha kuwa ni Geofrey Membe wa Kata ya Nachingwea kumweleza kuwa wanapaswa kutambua kuwa gesi hiyo ni muhimu kubaki Mtwara ili mitambo ya kuzalishia umeme wa gesi ijengwe Mtwara.
“Mikoa ya Mtwara na Lindi inachangia kwa kiasi kikubwa pato la taifa kupitia zao la korosho,” alisema. Kauli hiyo ilipokewa kwa shangwe na wananchi waliohudhuria.
Baada ya mkuu huyo wa wilaya kumaliza mkutano huo na kuondoka, kundi la vijana lilianza kuwafuata viongozi wa CCM wakiimba ‘gesi haitoki… gesi haitoki’.

SimbachaweneIlidaiwa kwamba msafara wa Simbachawene uliwekewa magogo barabarani juzi saa nane mchana na kumfanya waziri huyo na msafara wake kugeuzia katika Kijiji cha Ziwani na kurejea mjini Mtwara.
Habari hizo ambazo zimekanushwa na Simbachawene zilidai kuwa aliwasili Mtwara kwa ndege asubuhi na kupokewa na viongozi wa mkoa kabla ya kuanza safari ya kwenda Msimbati kimyakimya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Msimbati, Salum Athumani Tostao alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa polisi walikwenda kijijini hapo na kufyatua mabomu ya machozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki alithibitisha wananchi kufunga barabara lakini alikanusha madai kwamba Naibu Waziri Simbachawene alikuwapo ziarani mkoani hapa.
“Waandishi wa habari waliokwenda katika ziara za kazi zao za kawaida ndiyo waliozuiliwa na wananchi hao… Naibu Waziri (Simbachawene), hajawahi kufika Mtwara kwa siku ya jana… Wananchi walidhani hilo gari ni la waziri lakini ukweli si yeye,” alisema Kamanda Nzuki.

Akizungumzia madai hayo Simbachawene alisema: “Hapana si kweli, ningekuja hapo mjini nisingejificha… Tatizo la wananchi wetu hawajapata elimu sasa nitaendaje huko kimyakimya ili iweje? Jana nilikuwa ofisini na vikao kutwa nzima… Nenda ‘airport’ (uwanja wa ndege) kaulize… Hata mimi nimeona kwenye jamii forum mtu yeyote anaweza kuweka chochote.”
Habari hii imeandikwa na Christopher Lilai, Nachingwea na Abdallah Bakari, Mtwara na Mkinga Mkinga Dar.






















About Author

Advertisement

 
Top