Unknown Unknown Author
Title: HIKI KIKIFANYIKA KILWA, NDICHO WAKUSINI WANACHOLILIA
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
Mchoro unoonesha hospitali itakayojengwa wilayani Kilwa kutokana na upatikanaji wa gesi. BILA shaka kwa baraka za Mungu wasomaji wa safu h...
Mchoro unoonesha hospitali itakayojengwa wilayani Kilwa kutokana na upatikanaji wa gesi.
BILA shaka kwa baraka za Mungu wasomaji wa safu hii hamjambo, kama hivyo ndivyo, basi hatuna budi kumshukuru kwa kutufanya tuwe na afya njema siku hii ya leo, hakika yeye ni mwema na tumhimidi milele.
Leo ningependa kuzungumzia tatizo la muda mrefu linalojadiliwa na kila mpenda maendeleo kuhusiana na upatikanaji wa gesi asili kusini mwa nchi yetu.
Kuna usemi wa wahenga usemao  ‘mgeni njoo, mwenyeji apone’ ambao una tafsiri nyingi  lakini mojawapo ni ile ya kuona kwamba mara nyingi mgeni afikapo, mwenyeji hujikuta akipata zawadi au manufaa ya ujio wake.
Ndugu zangu, utaratibu huu unaweza kushabihiana na itakavyokuwa katika Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi ambako imegundulika gesi.
Tumejulishwa kuwa Kampuni ya Statoil kutoka Norway ikishirikiana na Exxon Mobil imegundua gesi katika Visiwa vya Zafaran na Lavan vilivyopo Kitalu 2, Ukanda wa Pwani ya Tanzania, hususan Pwani ya Kilwa.
Mradi huo utafanywa na wageni ambao wana utaalamu wa miaka mingi katika biashara ya gesi duniani na ni dhahiri kwamba wakazi wa Kilwa, Lindi na Mtwara kwa jumla hawana budi kupata faida za moja kwa moja na zingine zisizo za moja kwa moja kutokana na mradi huo.
Miongoni mwa faida zisizo za moja kwa moja ni gesi hiyo kutumika kutengeneza umeme utakaopatikana kwa uhakika na kuuzwa kwa wananchi wote Tanzania bila ubaguzi.
Lakini  ujio wa mradi huo kwa upande mwingine una faida kwa wana Kilwa kutokana na kutoa ajira ambayo itazingatia uwezo.
Faida nyingine kwa wakazi wa Kilwa nimeisikia ikisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa, Adoh Mapunda ambaye amesema walijiuliza baada ya kufika kwa wageni hao.


Akasema madiwani, watendaji na mkuu wa wilaya yao walikaa na kutafakari kwa kina juu ya faida ya kudumu itakayoonekana wilayani mwao kutokana na ujio wa mradi huo wa gesi.
“Sisi tulikataa kauli za kusaidiwa madawati kwenye shule zetu, ama kupewa dawa kwenye hospitali na zahanati zetu. Hii ni kwa sababu tuna uwezo nazo, badala yake tukabuni mradi mkubwa wa kimataifa ambao utakuwa na faida ya kudumu kwa Kilwa na taifa kwa ujumla,” anasema.
Anafafanua kwamba mradi huo ni ujenzi wa hospitali ya kimataifa itakayolingana na ile ya Apollo ya nchini India ambayo viongozi mbalimbali duniani hukimbilia kwenda kutibiwa.
Anasema hospitali ya aina hiyo itajengwa na mwekezaji na itaendeshwa na taasisi nyingine ya kimataifa huku halmashauri ikiwa na hisa za kupata gawio la kila mwaka kutokana na faida itakayopatikana.
Anasema walizungumza na wawekezaji, yaani Statoil, kwamba wawajengee hospitali ya aina hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kutoa tiba kwa viongozi, wakiwamo marais wa Afrika na wakuu wa kampuni mbalimbali za Afrika na wafanyabiashara wa nchi mbalimbali na wananchi wa kawaida.
Mapunda anafafanua kuwa mpango huo unatekelezwa kupitia utaratibu uliopo kwenye mikataba kwa wawekezaji kuhusu uwajibikaji na ushiriki katika masuala ya kijamii, yaani, Social Co-operation Responsibility (SCR).
Anasema tayari Statoil imetenga Shilingi bilioni 18  za kuanza ujenzi wa hospitali hiyo mjini Kilwa wakati wowote kuanzia mwaka huu, ipo tayari na imechorwa kama lilivyokuwa jengo la kifalme, yaani Kasri lililojengwa eneo la Kilwa Kisiwani enzi za sultan wa Kiarabu aliyekuwa akimiliki kisiwa hicho.
Ndugu zangu, viongozi wa Kilwa wanastahili pongezi nyingi sana, tunataka viongozi kama hawa.
Amesema wanatarajia kwamba taasisi ya kimataifa ya Aga Khan Foundation ndiyo itakayoendesha hospitali hiyo kwa kiwango cha kimataifa . “Tulikaa na kuzungumza pande zote tatu, yaani Kilwa, Statoil na Aga Khan Foundation na kukubaliana kuanzisha hospitali hiyo, hivyo tuna imani itaendeshwa kama ile ya Apollo,’’ anasisitiza Mapunda.
Anasema hospitali hiyo itaajiri madaktari mabingwa kutoka ndani na nje ya nchi, itakuwa na wafanyakazi wataalamu, pamoja na wahudumu ambao wengi watatoka Halmashauri ya Kilwa.
Niseme bila kumung’unya maneno kuwa viongozi wa Kilwa wamefanya kile ambacho kila penye maliasili inatakiwa wananchi wafaidike nayo maana Mungu aliwawekea kwa makusudi maalumu.
Naamini kabisa kuwa kama kule Mtwara viongozi wangekuwa na mikataba kama hiyo na wananchi wakatangaziwa, kusingekuwa na maandamano ya kudai neema kama waliyoyafanya.
Waliandamana baada ya kuona hawaambiwi chochote cha kuwanufaisha, wakahisi kuwa yaliyowapata watu wa Buhemba kwenye madini, yangewakumba hata wao! Kwani maeneo mengi ya madini yamebaki ‘mahandaki’ yasiyo na faida kwao.
Viongozi wa halmashauri zote ambazo zina maliasili waige mfano wa viongozi wa Kilwa ambao hakika walichokifikiria ni cha maendeleo kwa wananchi wa Kilwa na taifa.
Ni wajibu wa viongozi sasa kukataa kabisa mikataba mibovu ambayo inawanufaisha wageni na wenyeji wachache wenye roho ya ubinafsi.
Viongozi wa aina hiyo tusiwape nafasi na naamini haya ya Kilwa yatafanywa Mtwara na kwingineko kwenye rasilimali za taifa na kiongozi atakayekiuka, basi tumuone ni msaliti wa Watanzania.

source: global publisher

About Author

Advertisement

 
Top