Na Said Hauni, Lindi.
Januari 17: WAKAZI wa mji mdogo wa Nachingwea,wilayani humo,mkoani Lindi,wamewazomea viongozi watatu wa wilaya hiyo, akiwemo mmoja wa Serikali na wawili wa kisiasa kwa madai ya kutoridhishwa na ushawishi wao wa kuwataka wasiwaunge mkono wannanchi wa mkoa wa Mtwara, wanaopinga mpango wa Serikali wa kuisafirisha kwa njia ya bomba gesi kwenda kuzalishwa umeme Jijini Dar es salaam.
Viongozi waliokumbwa na zomeazomea hiyo,ni mkuu wa wilaya hiyo,Reginal Chonjo,mwenyekiti wa Chama cha mapinduzi (CCM) Albert Mnali na mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa ya Chama hicho,Fadhili Liwaka.
Tukio hilo limetokea mwanzoni mwa wiki hii,kwenye mkutano wa hadhara uliohitishwa na viongozi hao uliofanyika viwanja vya kituo cha mabasi cha mji mdogo wa Nachingwea.
Wakiwa wanahutubia umati mkubwa wa watu katika eneo hilo,kwa nyakati tafauti viongozi hao,waliwataka wananchi wa wilaya hiyo,kutowaunga mkono mgogoro mgogoro wa gesi unaoendelea mkoani humo,kwa madai kwamba hauna maslahi kwa wakazi hao.
Zomeazomea hiyo,ilikuja muda mfupi,baada ya mkuu wa wilaya hiyo kusimama na kuanza kuhutubia huku akiwataka kutojiingiza kwenye maandamano yanayoandaliwa hivi karibuni katika miji ya Mtwara na Lindi,kuishinikiza Serikali kutoihamisha gesi iliyogundulika mkoani Mtwara na kuipeleka Dar es salaam,ikiwa ni jitihada za wakazi hao kuishinikiza Serikali kutoihamisha kwa ajili ya kuzalishwa umeme nje ya mkoa wao.
Katika mkutano huo Chonjo alisema wakazi wa wilaya ya Nachingwea hawana sababu ya kushiriki migogoro hiyo, kwa madai kwamba tangu awali wananchi hao wamekuwa wanatumia raslimali zilizo nje ya wilaya na mkoa wao wa Mtwara.
Mkuu huyo wa wilaya ya Nachingwea, alizitaja baadhi ya raslimali ambazo wana Mtwara wanazitumia kutoka nje ya maeneo yao kuwa ni pamoja na umeme na barabara ya Kibiti hadi Lindi, ambao ujenzi wake umetokana na raslimali alizodai ni za nchi nzima.
Kufuatia kauli hiyo kuliwafanya wananchi hao bila ya kujali itikadi zao za kisiasa,wakaanza kumzomea hata pale aliporuhusu kuulizwa maswali kutoka kwa wakazi hao.
“Ndugu zangu wana Nachingwea,Serikali haina nia mbaya na wakazi wa Lindi na Mtwara kwa kuipeleka gesi hiyo Dar es salaam,kinachofanyika ni kuipeleka hii gesi sokoni, ili iweze kutumika kwa faida ya watanzania wote, kwani soko la Gesi lipo huko inakopelekwa na ni sehsmu ya mgawanyo wa raslimali zetu za Taifa”Alisema Chonjo.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi,kutoburuzwa na wanasiasa ambao wanatumia udhaifu na ufahamu mdogo waliokuwa nao,kutaka kuleta mgawanyiko miongoni mwa Watanzania,kutokana na raslimali zisitumike katika eneo lingine,badala yake iwe inatumika pale inapopatikana tu.
“Kama kila rasilimali inapopatikana itumike ndani ya eneo husika,basi hata uwezekano wa barabara ya Kibiti hadi Lindi isingeweza kujengwa kwani kwa kutumia raslimali za mikoa ya Lindi na Mtwara isingetoshereza”Alisema Chonjo.
Aidha mkuu huyo wa wilaya katika mkutano huo,amewataka wananchi kutilia mkazo suala zima la elimu kwa watoto wao,kwani licha ya Serikali kujenga Shule za msingi na Sekondari za kutosha kwa kila kata na vijiji, bado mwitikio wa wanachi umekuwa ni mdogo hali inayosabaisha kukithiri kwa utoro.
Baada ya maelezo hayo ya mkuu wa wilaya,mkazi wa kata ya nachingwea,Jofrey Membe,amewataka viongozi wa Serikali,akiwemo mkuu wa wilaya hiyo,na mwenyekiti,Albert Mnari,kutiwapotosha umma kutokana na kauli zao wanazozieneza mbele ya Jamii, kwamba wana Mtwara wanazuia gesi isiwanufaishe watanzania.
Membe aliuambia uongozi huo kwamba,hakuna mwana Mtwara wala kusini kwa ujumla anayetaka gesi hiyo iendelee kubaki mkoani humo,bali kinachotakiwa ni viwanda au kinu kitakachohusika na uzalishaji wa umeme vijengwe mkoani humo,badala yake usafirishwe umeme uliokuwa tayari umeshatengezwa, badala ya kusafirisha mali ghafi kwenda Jijini Dar es salaam.
“Ndugu zetu viongozi wa Serikali na Chama tawala,msiupotoshe umma,hakuna mwana-Mtwara hata kusini kwa ujumla anayesema gesi isiwanufaishe watanzania,,,,,,,,,,,kinachotakiwa kinu au viwanda vya kusindika umeme vijengwe Mtwara,kama ilivyokuwa katika maeneo mengine ya nchi yetu”Alisema Membe.
Membe alitaja baadhi ya maeneo ambayo vipo viwanda vilivyojengwa nje ya mkoa wa Dar es salaam, ni pamoja na Morogoro,Moshi na Kagera,kunakolimwa miwa na zao la kahawa, na viwanda vya kuzalishia bidhaa hizo zimejengwa ndani ya maeneo husika.
“Hakuna sababu kwa Serikali kuingia mzigo mkubwa wa gharama ya kuisafirisha gesi kwa bomba,wakati Mtwara kuna maeneo ya kutosha kujengwa kwa viwanda, na ukasafirishwa umeme takribani nchi yote ya Tanzania na kama kusafirishwa basi usafirishwe umeme na sio gesi”
“Kama ni wingi wa viwanda kuwa Dar es salaam, sio kigezo cha kusafirisha gesi, kwani viwanda vinahitaji umeme, kwani kabla ya gesi ya Songosongo Kilwa nah ii ya Mtwara viwanda hivyo vilikuwa vikitumia umeme wa maji kutoka mkoa wa Morogoro,lakini maji yale hayakusafirishwa kwa bomba mbona,iweje gesi”Alihoji Membe.
Naye, Godfrey Chuma kasema kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha umeme ndani ya mkoa huo,hauna lengo la kuwagawa watanzania, kwani hata Mbeya kinajengwa kiwanda cha gesi inayodaiwa kugunduliwa huko.
“Kama kuwagawa watanzania basi ni nyinyi viongozi wa Serikali na Chama tawala mnaoshabikia mambo haya,kwa kila kitu kupeleka sehemu moja ya dare s salaam”Alisema Chuma.
Chuma alisema hata hiyo barabara ya Kibiti-Lindi haikujengwa kwa rasilimali za kutoka nje ya mikoa hiyo pekee, kwani hata wao kuna sehemu kubwa ya michango yao, wakiwemo na wafadhili kutoka nje ya Taifa letu.
Baada ya mkuu huyo wa wilaya kumaliza mkutano huo na kuondoka eneo hilo,kundi la watu wakiwemo vijana liliwafuata viongozi HAO wa Chama cha mapinduzi (CCM) huku wakiwaimbia kwa kusema hawapo tayari gesi itoke Mtwara, hali iliyosababisha askari Polisi waliokuwepo kwenye mkutano kutawanya wananchi hao, walikuwa wanaendelea kuwafuata kwa nyuma huku wakiendelea kuwazomea pia.