Unknown Unknown Author
Title: UCHOVU ULITUNYIMA USHINDI JANA, ASEMA KOCHA AZAM
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
KOCHA wa makipa wa Azam, Iddi Abubakar Mwinchumu amesema kwamba, jana walilazimishwa sare ya 1-1 na Dragons ya hapa katika mchezo wa Kundi B...
KOCHA wa makipa wa Azam, Iddi Abubakar Mwinchumu amesema kwamba, jana walilazimishwa sare ya 1-1 na Dragons ya hapa katika mchezo wa Kundi B kuwania Kombe la Hisani kwenye Martyrs mjini hapa kutokana na uchovu wa safari na pia timu kucheza bila makocha wake.
Akizungumza baada ya mechi ya jana mjini hapa, Iddi alisema kwamba timu ilifika usiku sana wa juzi na jana ikaingia uwanjani, hivyo wachezaji walikuwa wana uchovu, lakini anaamini mechi ijayo kesho watashinda.
Aidha, Iddi alisema pia timu kucheza bila makocha wake, ambao wamebaki Kenya nako kwa namna moja au nyingine kulichangia matokeo hayo. “Ilikuwa ghafla tu, nikaambiwa Iddi utaongoza timu katika mechi hii, nashukuru tumepata sare na tumecheza mpira mzuri sana kila mtu ameona, ila kama makocha wangekuwapo tungecheza vizuri zaidi na tungeshinda,”alisma Iddi ambaye ni kocha wa makipa Azam na kipa wa zamani wa timu hiyo.

Azam ilicheza mechi hiyo bila makocha wake wote wawili, Waingereza Stewart Hall na Msaidizi wake, Kali Ongala ambao wamebaki Nairobi, Kenya pamoja na Daktari Mjerumani Paulo Gomez na wachezaji Kipre Balou na Kipre Tcheche kutokana na kukosa viza za kuingia DRC.
Katika mechi ya jana, hadi mapumziko, wenyeji walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na mshambuliaji wao hatari, Nkate Jason dakika ya 24.
Nkate alifunga bao hilo baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Azam, ambao walichanganyana na kipa wao, Mwadini Ally. Pamoja na kufungwa, Azam walicheza vizuri katika dakika 45 za kwanza na zaidi walikosa mipango tu ya kumalizia.
Hata hivyo, mashambulizi ya pembeni ya wapinzani wao yalilitia misukosuko ya kutosha lango la Azam katika ungwe hiyo.
Kipindi cha pili Azam walirudi na kikosi kile kile, lakini walibadilika kiuchezaji na iliwachukua dakika nne tu kukomboa bao, kupitia kwa Nahodha mpya, Jabir Aziz aliyeunganisha pasi ya Abdi Kassim ‘Babbi’.
Baada ya bao hilo, Azam waliendelea kushambulia lango la wapinzani wao, lakini safu ya ulinzi ya Dragons ilisimama imara kudhibiti mashmbulizi hayo.
Katika dakika ya 76, kipa Mwadini alipangua kwa uhodari mkubwa mkwaju wa penalti wa Mukinzi Mawesi, baaada ya mchezaji huyo huyo kuangushwa kwenye eneo la hatari na Ibrahim Mwaipopo.
Baada ya hapo Azam walihamia langoni mwa Dragons, ambao safu yao imara ya ulinzi iliwanusuru adhabu hii leo.
Azam ambao ni washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Ligi Kuu, wamepangwa katika Kundi B pamoja na Dragons na Shark FC, ambayo watacheza nayo Desemba 17.
Ikifuzu kwenye kundi lake, Azam itaingia Nusu Fainali moja kwa moja, ambazo zitachezwa Desemba 25 na Desemba 26 itakuwa Fainali na mechi ya kusaka mshindi wa tatu. 
Kundi B, lina timu za DC Motema Pembe, Diables Noirs, FC MK na Real De Kinshasa. 
Kikosi cha Azam jana kilikuwa; Mwadini Ally, Himidi Mao, Waziri Salum, Luckson Kakolaki, David Mwantika, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Abdi Kassim, Gaudence Mwaikimba, Abdallah Seif/Humphrey Mieno na Uhuru Suleiman/Zahor Pazi.













About Author

Advertisement

 
Top