Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa (mbele) akiongozana na Mkewe Mama Anna Mkapa (kulia) pamoja na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini na mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mkapa Foundation, Mheshimiwa Hawa Ghasia (kushoto) wakiwasili kwenye hafla ya kukabidhi Nyumba 30 za watumishi wa afya katika wilaya za Mtwara Vijijini, Newala na Masasi, mkoani Mtwara.
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, amekabidhi rasmi nyumba 30 za watumishi wa afya katika wilaya za Mtwara Vijijini, Newala na Masasi, mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa kukabidhi nyumba hizo katika hafla iliyofanyika tarehe 19 Desemba 2012 katika kijiji cha Imekuwa, Mtwara Vijijini Mheshimiwa Mkapa alizisisitizia Halmashauri za wilaya tatu zilizokabidhiwa nyumba hizo zizitunze ili ziweze kutumika kwa muda mrefu na pia akasisitizia Halmashauri zitenge bajeti ya kutosha kwa ajili matengenezo madogo madogo.
Rais Mstaafu pia akatoa rai kwa Halmashauri hizo za wilaya kuzipatia dawa, vifaa na watumishi wa afya wa kutosha zahanati ambazo nyumba hizo zimejengwa na akatambua mazingira magumu ya kazi katika maeneo ya vijijini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mkapa Foundation, Dr. Ellen Mkondya-Senkoro akaeleza gharama za ujenzi wa nyumba zote 50 zilizojengwa katika mkoa wa Mtwara zimegharimu takribani Shilingi bilioni 3.2 pesa za Kitanzania.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye alikuwepo kwenye makabidhiano hayo, alitambua mchango wa Taasisi ya Mkapa Foundation katika kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ya kuleta maendeleo katika sekta ya afya.
Nyumba hizi ni sehemu ya nyumba 50 ambazo Taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation kupitia mradi wa uimarishaji wa mfumo wa sekta ya afya (Health Systems Strenghtening) unaofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria- Mzunguko wa 9.
Nyumba nyingine 20 zilizobaki ziko katika hatua za mwisho wa ujenzi kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa halmashauri za wilaya Tandahimba na Nanyumbu.
Wengine waliokuwepo kwenye hafla hiyo walikuwa ni pamoja na Waziri katika ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ambaye ni Mbunge wa Mtwara Vijijini na mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mkapa Foundation, Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mkapa Foundation, Meja Mstaafu Herman Lupogo.
Ujenzi wa nyumba hizi umesimamiwa na Kampuni ya Arqes Africa na mkandarasi aliyejenga nyumba ni kampuni ya Namis Construction.Jiwe la Msingi lililowekwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh. Benjamin Mkapa lililopo katika moja ya nyumba hizo.