BAADA ya kumaliza msimu uliopita ikiwa na majeruhi wengi, Manchester United imeamua kuwekeza nguvu na akili zake katika kuondoa tatizo hilo.
Tayari, klabu hiyo imewekeza pauni 25milioni kujenga kituo cha kisasa cha tiba kwenye uwanja wake wa mazoezi Carrington.
Uamuzi huo unalenga kuipunguzia klabu hiyo gharama ambazo inadai kuwa iliingia baada ya kumaliza msimu uliopita ikiwa na majeruhi wengi mno.
Kocha wao, Sir Alex Ferguson amekuwa akikabiliana na tatizo la majeruhi wengi msimu huu ambao ni pamoja na Nemanja Vidic, Ashley Young na Phil Jones , wote hawajarudi uwanjani.
Kituo hicho kipya na cha kisasa kinaifanya United kuwa ya kwanza duniani kuwa na kituo bora ambacho kitaweza kutambua majeraha kwa wanasoka pamoja na kufanya uchunguzi kama wa magonjwa ya moyo ambayo yanasumbua wanasoka kama Fabrice Muamba wa Bolton msimu uliopita.
Ukarabati wa kituo hicho ambao umegharimu karibu pauni 13m umekamilika na Man United imetangaza mpango wa miaka mitano wa kuingia mkataba na Kampuni ya Toshiba Medical Systems ya Japan ambayo itatoa vifaa tiba ya pauni 12m.
"Nilidhani wanacheza, kumbe wanajenga kwa haraka," alitania Ferguson na kuongeza:"Lakini,Toshiba wameingia na wako tayari kuweka vifaa vya kisasa, hii ni hatua muhimu katika sayansi ya michezo na tiba kwa wachezaji wetu.
"Huu ni ushirikiano ambao utatuweka juu, mbali ya klabu nyinginezo duniani. Siamini kuwa Toshiba wanakuja hapa na vifaa vya kisasa vya tiba, bali kutusaidia. Tayari tunajivunia wataalam wazuri, ambao sina shaka watajifunia kufanya kazi kwa pamoja na Toshiba.
"Tatizo wakati mwingine ni kwa mashabiki ambao ni kama hawaoni uwekezaji huo. Lakini, tutaona faida yake, kila mmoja atafurahi. Haya ni maendeleo makubwa.
"Tumesajili wachezaji wengi mahiri msimu huu, lakini hawawezi kuwa wenye faida kama hawatakuwa fiti kucheza na kutoa matokeo mazuri."
Kituo hiki kitaiwezesha United kufanya uchunguzi wa afya ya wachezaji wake wapya na kutambua uwezo wao, aina za kudumu za majeruhi yao na hata mbinu za kuwatibu.
Tags
Man UTD FC