Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa Saintiefe anatarajiwa kuwasili nchini saa 7:25 na atakwenda moja kwa moja katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.
Sendeu alisema kuwa kocha huyo atafanya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa klabu yao na endapo watafikia makubaliano, atasaini mkataba wa mwaka mmoja na kuanza kazi kesho jioni.
Juni 2011, Saintfiet aliteuliwa kuiongoza Ethiopia na siku kumi baadaye akafanya maajabu kwa kuiwezesha timu hiyo kupata sare isiyotarajiwa ya ugenini ya mabao 2-2 dhidi ya Nigeria inayoundwa na nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya, wakiwemo Obi Mikel wa Chelsea na Joseph Yobo.
Matokeo hayo yaliikosesha Nigeria nafasi ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2012 zilizofanyika Gabon na Equatorial Guinea na kuzua gumzo kubwa kwani katika mechi yao ya awali ambayo Saintfiet alikuwa bado hajatwaa madaraka, Nigeria waliishindilia Ethiopia 4-1 na siku nne kabla ya mechi yao, Nigeria waliiadhiri timu ya taifa ya Argentina kwa kuifunga mabao 4-1.
Hata hivyo, Saintfiet aliiacha Ethiopia miezi mitatu baadaye kutokana na kile alichodai kuwa ni kutotimizwa kwa baadhi ya mambo aliyokuwa amekubaliana na mwajiri wake, chama cha soka cha Ethiopia.
Machi 28, Nigeria walitangaza kumteua Saintfiet kuwa mkurugenzi wao wa ufundi, lakini chama cha soka cha Nigeria kikasitisha azma hiyo baada ya Waziri wa Michezo wa Nigeria, Bolaji Abdullahi kuwataka waachane naye.
Saintfiet aliwahi pia kuifundisha timu ya taifa ya Namibia kuanzia 2008 hadi 2010 ambapo aliiacha timu hiyo na kufuata ‘ofa’ nono ya Zimbabwe ambako hata hivyo, hakudumu sana baada ya serikali kumnyima kibali cha kufanyia kazi.
Wakati Yanga ikimuwania Saintfiet, rekodi yao ya kukaa na makocha hivi karibuni mekuwa si ya kuridhisha sana. Wanajangwani walishaachana na Dusan Kondic, Sam Timbe na Kostadin Papic kutokana na sababu kadhaa, zikiwemo zinazodaiwa kuwa ni kutotimizwa kwa baadhi ya makubaliano wanayoingia.
MINZIRO
Katika hatua nyingine, kocha wa sasa wa Yanga, Fred Minziro alisema jana kuwa maamuzi ya kupeleka yosso Zanzibar si kwamba wameikimbia Simba kwenye michuano ya Kombe la Urafiki inayoendelea Visiwani Zanzibar.
Yanga inadaiwa kupeleka Yanga B kwenye mashindano hayo ili kukwepa kukutana na mahasimu wao Simba ambao wanarekodi ya kuwafunga magoli 5-0 na hivyo wanahofia kuendeleza uteja.
Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mazoezi ya asubuhi kwenye uwanja wa Kijitonyama, Minziro, alisema sababu ya kupeleka timu B katika michuano ya Urafiki si kuwahofia mahasimu wao Simba ila ni kutokana na wachezaji wake wa kikosi cha kwanza kufanya mazoezi ya pamoja kwa muda mfupi.
“Hatujawahi kuihofia Simba, tumepeleka timu B ili nao kuwapa nafasi ya kupata uzoefu,” alisema Minziro ambaye alikuwa akiisimamia timu hiyo ikipata kipigo cha aibu cha 5-0 kutoka kwa Simba huku aliyekuwa kocha mkuu, Kostadin Papic, akiwa jukwaani baada ya kukacha kuendelea kuifundisha Yanga kutokana na mkataba wake kumalizika.
“Tumekuwa na muda mfupi sana wa mazoezi ya pamoja. Tumecheza mechi moja ya kujipima dhidi ya Express (ya Uganda ambayo wana Jangwani walishinda 2-1) na tunahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi ya pamoja, halafu kuna michuano ya Kagame inakuja Julai 14. Huwezi kwenda namna hiyo. Tunahitaji mazoezi. Tunahitaji kutetea kombe,” alisema nyota huyo wa zamani wa klabu hiyo.
Katika mazoezi hayo yaliyomalizika saa sita mchana, nyota wote wa Yanga, akiwemo kiungo wa timu ya taifa ya Rwanda, Haruna Niyonzima, Mganda Hamisi Kiiza, beki aliyejiunga kutoka Simba, Kelvin Yondani, Nizar Khalfani na kipa Yaw Berko wote walikuwepo.
Tags
Young African FC