Simba inashuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na URA ya Uganda kwenye mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Kagame lililoanza jana bila mshambuliaji wake nyota wa kimataifaifa, Mganda Emmanuel Okwi ambaye inadaiwa yupo katika harakati za kutafuta timu ya kumsajili Ulaya.
Lakini hata bila mshambuliaji huyo kipenzi namba moja cha mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi aliyetoa mchango mkubwa katika kuipa ubingwa wa Bara msimu uliopita, kocha Milovan Cirkovic amesema hatarajii kama kutakuwa na pengo.
Milovan alisema katika mchezo wa leo atawaanzisha wachezaji wake nyota waliosajiliwa kutoka nje ya nchi.
Mchango wa Okwi ni mkubwa kiasi kwamba mshambuliaji huyo ama alifunga au kutengeneza nafasi katika magoli yote yaliyoipa Simba ushindi wa 5-0 dhidi ya mahasimu Yanga waliofungua pazia la michuano hiyo jana dhidi ya Atletico ya Burundi.
Akizungumza na Nipashe Jumapili Milovan alisema wachezaji aliowateua kwa mashindano hayo wana uwezo mkubwa wa kuipa mafanikio timu hiyo.
“Kila mchezaji Simba ana nafasi yake na umuhimu wake katika kikosi, kesho (leo) tunapambana na URA lakini sina hofu kwa sababu wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mashindano haya,” alisema.
“Tumepata michezo ya kutosha kujiandaa kwa ajili ya mashindano haya na naamini kesho tutafanya vizuri na kuwafurahisha mashabiki na wanachama wa klabu hii.”
Alisema kuwa pamoja na kuwa hajaiona URA ikicheza, lakini hilo halimpi presha na kikosi chake kitacheza soka kulingana na mchezo wa wapinzani wao.
Kwa upande wake, Nahodha wa Simba ambaye pia ni kipa namba moja wa klabu hiyo, Juma Kaseja, amesema kuwa yeye na wachezaji wenzake wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mashindano hayo na kuahidi ushindi kwenye mchezo wa leo dhidi ya URA.
“Sisi kama wachezaji tupo tayari kwa mashindano haya. Kocha wetu amefanya kazi yake kabla ya mashindano na sasa ni zamu yetu sisi kama wachezaji kufanya kazi yetu uwanjani,” alisema.
Kaseja alisema katika mashindano ya mwaka huu lengo ni kuvuka hatua waliyoishia kwenye mashindano ya mwaka jana ambapo walifika fainali na kufungwa na Yanga goli 1-0.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano hayo iliyotolewa na baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kesho ni siku ya mapumziko ambapo michezo itaendelea tena Jumanne.
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.