SIMBA ITAPAMBANA ILI IFUTE UTEJA MACHI 8

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema maandalizi kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba utakaopigwa Jumamosi, Machi 8 yanaendelea vizuri.

Kamwe alithibitisha kuwa kikosi cha Yanga kilirejea mazoezini jana baada ya mapumziko ya mwishoni mwa wiki, na kuwa na muda mzuri wa kujiandaa kwa ajili ya mchezo huo, ambao kwa sasa umekuwa gumzo kila kona.

 
"Niwaambie mashabiki na wanachama wa Yanga, tayari tumeanza maandalizi kuelekea mchezo huu. Wachezaji wetu wameingia kambini na wanakamilisha maandalizi ya siku hii ya Machi 8 ambapo tutakutana na Simba," alisema Kamwe.

Kamwe alikiri kuwa Yanga ina rekodi nzuri dhidi ya Simba, wakiwa wamepata ushindi mara nne mfululizo, lakini pia aliongeza kuwa rekodi hiyo inafanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi, kwani Simba watakuja wakitaka kufuta uteja.

"Tuna rekodi nzuri dhidi ya Simba, tumeshinda mara nne mfululizo, lakini tunatambua kuwa hiyo rekodi nzuri imeongeza ugumu wa mchezo, kwani wenzetu watakuja wakitaka kupambana kufuta uteja. Sisi tunajiandaa na hilo, na tuko tayari kupambana nao," alisema Kamwe.

Aidha, Kamwe alisisitiza kuwa malengo ya Yanga ni kushinda mchezo huo ili kuendelea kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi, huku akiamini kuwa bado watakuwa na kazi kubwa ya kupambana katika mechi saba zitakazosalia ili kutetea ubingwa wao kwa msimu wa nne mfululizo.

Post a Comment

Hii ni Blog kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Nchi yetu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...

Previous Post Next Post