
Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Malkia wa Bongo Fleva, Faustina Charles Mfinanga, maarufu kama Nandy, pamoja na msanii mahiri wa RnB kutoka Tanzania, Juma Jux, wamepata fursa ya kupokea tuzo zao za Trace usiku wa kuamkia leo, Machi 2, 2025. Hafla hiyo ya kipekee ilifanyika katika hoteli ya kifahari ya Johari Rotana, iliyopo Dar es Salaam.
Tuzo hizi zilicheleweshwa kutokana na vikwazo vya kimazingira, ambapo baadhi ya washindi walishindwa kuzipokea katika hafla ya awali iliyofanyika visiwani Zanzibar hivi karibuni. Lakini, usiku wa leo, mafanikio hayo yalipata jukwaa la heshima.
Nandy alitunukiwa tuzo ya Msanii Bora wa Kike, akiendelea kung'ara na umashuhuri wake katika muziki wa Bongo Fleva, huku Juma Jux akishinda tuzo ya Msanii Bora wa Kiume nchini Tanzania. Ushindi wao ni uthibitisho wa juhudi, ubunifu, na ufanisi wao mkubwa katika sekta ya muziki ya Tanzania na ulimwengu mzima.