Jamii imeaswa kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na Magonjwa ya mlipuko
ikiwemo Marburg.
Hayo yamebainishwa na Afisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo
Mkoani Kagera Bi.Domina Jeremiah wakati akitoa elimu ya Afya katika Kanisa la
Waadventista Wasabato Ng'ambo.
Amesema miongoni mwa tahadhari muhimu za kuchukua
katika kujikinga ni pamoja na kuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara
kwa maji tiririka na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.
"Tunasema Kinga ni bora kuliko Tiba hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari,
tunawe mikono kwa maji tiririka na sabuni, tusisalimiane kwa kushikana
mikono, pia toa taarifa kwa uongozi wa Kijiji, mtaa, Kituo cha Huduma za Afya
kilichokaribu nawe au piga 199 bure" amesema.
Aidha, ametaja baadhi ya dalili za ugonjwa wa Marburg ni kutoka damu mwilini,
Homa, kuhara au kuharisha damu na unaweza kuenezwa kwa kugusa majimaji ya
mgonjwa ikiwemo jasho, damu, nguo, matandiko ya mtu mwenye maambukizi na
kuchangia vitu vyenye ncha kali, maambukizi kutoka kwa wanyamapori ikiwemo
sokwe, tumbili.
Mchungaji Samwel Mbilanga ni Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato
Ng'ambo Wilayani Biharamulo ameishukuru Serikali kwa kuweka jitihada kubwa za
Utoaji wa Elimu ya Afya huku akisema Kanisa hilo limejizatiti katika masuala ya
Afya.
"Tunashukuru Serikali kwa kuweka Kipaumbele cha elimu ya Afya ambapo na
sisi kama Kanisa moja ya jambo kubwa tunalozingatia ni masomo ya Afya kanisani
na tumehakikisha kuwa na ndoo za maji tiririka kila lango la Kanisa na chooni,
na suala la ulaji huwa tunazingatia sana Afya" amesisitiza.
Aidha, Mchungaji Mbilanga amesema katika kipindi suala la maombi kwa kushikana
wamesitisha ili kuzua maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.
Katika utoaji wa elimu ya Afya kanisani hapo,baadhi ya wadau walioshiriki ni
pamoja na Uwakilishi kutoka UNICEF, Africa CDC na TADIO.