Serikali
ya Tanzania imesaini mikataba miwili ya msaada yenye thamani ya dola za
Marekani milioni 20.3 sawa na shilingi bilioni 50.13 kwa ajili ya
kunusuru kaya masikini awamu ya pili (PSSN II).
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba alisema msaada huo
umetolewa na Serikali ya Uswisi dola za Marekani milioni 18 na Euro
milioni 2.2 sawa na dola za Marekani milioni 2.3 zimetolewa na Serikali
ya Ireland.
"Kiasi
cha misaada kilichosainiwa leo ni mwendelezo wa misaada mingine
iliyopokelewa kutoka kwa serikali hizi mbili ambapo misaada ya kipindi
cha nyuma kwa mpango huu wa kunusuru kaya maskini awamu ya pili ilikuwa
faranga za Uswisi milioni 15.72 sawa na dola za Marekani milioni 17.1
kutoka serikali ya Uswiss na Euro milioni 2 sawa na dola za Marekani
milioni 2.1 kutoka serikali ya Ireland. ," alisema Dkt. Mwamba.
Alisema misaada hiyo imewezesha serikali kufanya kazi yao kuwa rahisi katika kuleta maendeleo kwa watanzania wote.
Aidha,
PSSN II inaendana na Dira ya Tanzania ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo
inatoa mwelekeo wa juhudi za kuleta maendeleo ya nchi kiuchumi na
kijamii hadi kufikia mwaka 2025.
"Dira
hii kwa sasa inatekelezwa kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa
wa kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26 ," alisema Dkt. Mwamba.
Alisema
kwamba pia misaada hii pia inaendana na lengo la kwanza la Malengo ya
Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ambalo linalenga kuondoa umaskini
wa aina zote ifikapo mwaka 2030, na ajenda ya Afrika ya mwaka 2063
ambayo inalenga kuwezesha mpango wa Afrika kufikia ukuaji jumuishi na
endelevu wa uchumi na maendeleo ifikapo mwaka 2063.
Alisema
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umewezesha wanafunzi kutoka Kaya
maskini kupata elimu ya sekondari na elimu ya Juu. Mwaka 2022 wanafunzi
2,950 kutoka kaya maskini walipata mkopo wa asilimia 100 kutoka bodi ya
mikopo ya Elimu ya juu chini ya msaada wa PSSN II.
Aidha
alisema ukuaji wa uchumi wa Tanzania umeanza kuimarika ambapo katika
robo ya kwanza ya mwaka 2023 ukuaji ulikuwa ni asilimia 5.6.
Alisema
kwa mwaka 2019 kabla ya UVIKO – 19, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakuwa
kwa asilimia 7 lakini ukuaji huo ulishuka na kuwa asilimia 4.8 mwaka
2020 kutokana na madhara ya UVIKO – 19 na mwaka 2021 ukuaji ulipanda
hadi asilimia 4.9 kabla ya kushuka kuwa asilimia 4.7 mwaka 2022 kutokana
na madhara ya vita vya Ukraine na Urusi.
"Natumaini
misaada yenu kupitia PSSN II itawezesha kaya nyingi maskini kuondokana
na umaskini na kuchangia ukuaji wa pato la taifa," alisema Dkt. Mwamba.
Dkt.
Mwamba alisema bajeti yote ya PSSN II ni dola za Marekani milioni
883.32 ambapo watafikia malengo yaliyokusudiwa ifikapo mwishoni mwa PSSN
II mwwezi Septemba 2025 kwa kuwezesha kaya maskini kupata huduma za
kijamii na kiuchumi.
Dkt.
Mwamba alisema Serikali za Uswisi na Ireland siyo tu wanachangia kwa
mpango wa kunusuru kaya maskini lakini pia wanachangia sekta nyingine
zikihusisha Afya, Elimu, Haki za Binadamu, Utawala bora na Demokrasia.
Dkt.
Mwamba aliwahakikishia utayari wa Serikali chini ya Mheshimiwa Dkt.
Samia Suluhu Hassan kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi hizo kwa
maendeleo ya watu wetu na kuahidi kuwa msaada uliotolewa utatumika kwa
malengo yaliyokusudiwa.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, alisema PSSN
II itaboresha upatikanaji wa fursa za mapato na huduma za kijamii na
kiuchumi kwa kaya zenye uhitaji sambamba na kuimarisha na kulinda
rasilimali watu ya watoto wao.
Alisema
TASAF hadi sasa imefikia walengwa milioni Moja na laki tatu huku wakiwa
wametoa ruzuku ya shilingi bilioni 7.78, pia wametoa ajira 760,000 na
vikundi 50,000 vimewezeshwa kiuchumi.
"PSSN
II itafikia malengo yake kupitia utekelezaji wa hatua zilizojumuishwa,
kuongeza mapato ya kaya kupitia kujenga na kufanya kaya kujiamini,
kuimarisha udhibiti na kuwezesha kuwepo kwa ajira zenye tija zaidi,"
alisema Mziray .
Naye
Balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Mhe. Didier Chassot, alisema msaada
walioutoa ni mwendelezo wa ushirikiano baina ya Tanzania na Uswisi,
tangu mwaka 2020 serikali ya Uswisi imekuwa itoa misaada kwenye PSSN .
Balozi
wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Mary O'neil, alisema ushirikiano wa
Tanzania na Ireland ni wa zaidi ya miaka 40, kwa kipindi hicho chote
wamekuwa wakisaidia katika kuwawezesha wanawake, sera, amani na kaya
masikini.
Tags
HABARI ZA KITAIFA