Unknown Unknown Author
Title: SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 07
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 07 MTUNZI: NYEMO CHILONGANI ILIPOISHIA......!!! “Hakikisheni mnawakamata. Nawaongezea polisi huko!” “Saw...
SIMULIZI:: SITALIA TENA
SEHEMU YA 07
MTUNZI: NYEMO CHILONGANI

SIMULIZI:: SITALIA TENA SEHEMU YA 07
ILIPOISHIA......!!!
“Hakikisheni mnawakamata. Nawaongezea polisi huko!”
“Sawa mkuu! Tupe dakika thelathini, watakuwa mikononi mwetu wote wawili,” alisikika mwanaume kutoka upande wa pili. Simu ikakatwa. Kamanda akashusha pumzi nzito.


ENDELEA NAYO SASA....
Kareem alikuwa akizungumza na simu, alitaka kujua kama kile alichokipanga na Hassan kilifanyika kama kilivyotakiwa au la. Akawapigia simu na kutaka kusikiliza, hakutaka kusubiri mpaka usiku kwani aliwaambia kuwa ilikuwa ni lazima wakutane, wampe Saida wake na yeye kuondoka naye.

Akawapigia simu. Moyo wake ulikuwa na presha kubwa, alikuwa akimuomba Mungu ili Hassan na Hussein wawe na Saida wake. Simu ilianza kuita, ikaita na kuita, baada ya sekunde kadhaa, ikapokelewa na sauti ya Hassan kusikika.

“Tumefanikiwa mkuu!” alisema Hassan.
“Mnaye hapo?”
“Ndiyo!”
“Siamini! Hebu nizungumze naye,” alimwambia Hassan.

Hapohapo Hassan akampa simu Saida na kuanza kuzungumza naye. Kitu cha kwanza kabisa, msichana huyo akaanza kumshukuru Kareem kwa kile alichokifanya kwani vinginevyo angeweza kupigwa mawe na kuuawa.

Hilo halikuwa tatizo kwa Kareem, kama baba mtarajiwa alikuwa na wajibu wa kuilinda familia yake, hakuwa tayari kuiona ikipotea machoni mwake.

“Nitakuwa kila sehemu kwa ajili yenu, ni lazima nikupeleke Tanzania,” alisema Kareem huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
“Tutaondokaje? Najua kuanza leo jioni nitatafutwa tu,” alisema Saida.
“Hilo niachie mimi! Wala usijali!”

Alipomaliza kuzungumza na Saida, akaomba kuzungumza na Hassan na kumwambia sehemu ambayo walitakiwa kuonana ili amchukue mpenzi wake na kuondoka naye. Wakapanga kwamba sehemu iliyokuwa nzuri kuonana ilikuwa katika Jengo la Kiwanda cha Nguo cha Lammah Khuwair ambacho kwa kipindi hicho kilifungwa kutokana na matengenezo kadhaa yaliyokuwa yakifanyika.

“Huko kutakuwa kuzuri, ila si kuna ulinzi mkubwa?” aliuliza Hassan.
“Hilo usijali! Hatuingii ndani, nitafika hapo kwa ajili ya kumchukua mtu wangu,” alisema Kareem.
“Baada ya hapo?”
“Nitaondoka naye na kwenda ufukweni. Nitawasiliana na Yusuf Al Sadiq kwa ajili ya kutumia boti yake,” alijibu.
“Kwenda wapi?”
“Dubai!”
“Mmh!”
“Haina jinsi! Ni lazima nimpeleke msichana huyo huko kwani bila hivyo, watamuuua!” alisema Kareem.
“Haina shida. Tunakuja!”

Wakati wakizungumza hayo, tayari Hassan na wenzake walikwishafika katika eneo lililojulikana kama Al Amerath ambapo hapo kulikuwa na kampuni kadhaa kutoka humohumo Oman ambazo zilikuwa zikifanya uchimbaji wa mafuta.

Kutoka hapo mpaka Al Khuwair ilikuwa ni umbali wa kilometa kumi na mbili na barabara ambayo ilikuwa ikielekea huko ilipita katika jangwa kubwa la Bedouin.

Kulikuwa na joto kali, muda wote vioo vya gari vilikuwa wazi. Walijaza mafuta ya kutosha ya kuweza kuwatoa katika jangwa hilo mpaka huko walipokuwa wakielekea. Waliifuata barabara kubwa ya lami ambayo ilizungukwa na mchanga wa jangwa hilo, hawakutaka kurudi nyuma, hiyo ilikuwa safari ndefu kumpeleka na kuyaokoa maisha ya Saida.

Walikwenda kwa saa moja, wakawa wamebakiza kilometa kadhaa kabla ya kuingia Khuwair, wakaamua kuingia katika jangwa hilo, mchangani kabisa, waliamua kuachana na lami kwa sababu walihisi huko mbele kungekuwa na maaskari waliokuwa wakimtafuta Saida na wao waliohusika kumtorosha.

“Mbona tunapita huku?” aliuliza Hassan.
“Huku ni salama zaidi kuliko kule. Tunakaribia Khuwair, tunaweza kukuta maaskari njiani, huku ni salama Hassan,” alisema Hussein huku akiendelea kupiga gia.

Njiani, walikutana na watu mbalimbali, hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu naye kwani kwa nchi za Uarabuni lilikuwa jambo la kawaida sana kwa magari kuendeshwa jangwani.

Hawakutaka kusimama sehemu yoyote ile, hata waliposimamishwa na watu wengine waliohitaji lifti, waliwapita kwa kasi kubwa.

Walikwenda mpaka walipofika sehemu iliyokuwa na mahema makubwa meupe, nje ya mahema hayo kulifungwa ngamia watano. Hawakutaka kuendelea na safari kwa sababu gari lilihitaji maji baada ya yale yaliyokuwa yamewekwa kwenye rejeta.

“Maji yamekwisha, ni lazima tuongeze maji,” alisema Hussein.

Hakutana kubaki garini, harakaharaka akateremka na kuanza kuelekea kule kwenye mahema. Akasogea kule walipokuwa ngamia wale, akasimama mbele yao, akaanza kuzungumza maneno fulani, ngamia wote wakakaa chini na kutulia.

Wanaume wawili na mwanamke mmoja waliokuwa ndani ya hema moja wakatoka ndani. Mikononi walikuwa na majambia, walipomuona Husein, wakamuuliza kilichokuwa kimemleta.

“Nahitaji maji!” aliwaambia huku akiwaangalia mmoja baada ya mwingine.
“Hapana! Hatuna maji!” alisema mwanaume mmoja.
“Jamani! Naomba mtusaidie!”
“Tumesema hatuna maji! Na hata kama tunayo, si ya kutoa, humu ni jangwani, tukiwapa nyie, tutakunywa nini?” aliuliza mwanaume mmoja, alionekana kuwa kisirani hata kwa kumwangalia usoni.

“Mzee! Kesho tunaingia kwenye mfungo! Yaani upo radhi kuona mfungo wako wote ukiharibika kisa tu umetunyima maji! Vitabu vimeandika kwamba kabla ya kufunga ni lazima uwe msafi, ujiandae kwa ajili ya mfungo. Yaani maji tu yanataka kuharibu mfungo wako mzima,” alisema Hussein, japokuwa alikuwa mhuni lakini alijua mengi kuhusu dini.

Mzee akabaki kimya huku akikiinamisha kichwa chini kwa aibu, alipokiinua, akamwambia mwanamke yule akawape maji.

Mwanamke yule akachukua kidumu chake na kuingia ndani. Wanaume wale walibaki wakimwangalia Hussein. Alionekana kama mtu mwenye hofu nyingi, macho yao hayakutulia kwa Hussein tu bali waliangalia mpaka ndani ya gari lile, walimuona Hassan akiwa na wanawake wawili, hawakuelewa walikuwa wakina nani.

“Wale ni wakina nani?” aliuliza mwanaume mmoja.
“Wake zetu!”

Wakati hata hajaulizwa swali la pili, mwanamke yule akarudi huku akiwa na maji kwenye kidumu kile, Hussein akakichukua, akafungua boneti la gari na kuanza kuanza kujaza maji katika rejeta, alipomaliza, hakutaka kukaa, akafunga, akawashukuru na kuondoka zake.

Safari ikaendelea, baada ya saa moja, wakafika katika barabara kubwa ya Maanun Al Rajjit ambapo mbele kabisa ndipo kulipokuwa na kiwanda kile walichokubaliana na Kareem kwenda kuonana.

“Ingia barabarani, pale kule mbele utakata kushoto,” alisema Hassan na Hussein kufanya hivyo.

Walitumia dakika ishirini ndipo Hussein akakata kona na kuchukua barabara nyingine ya vumbi. Hapo walipoingia, kulikuwa na majumba mengi mabovu ambayo yalikuwa yakitumiwa na bilionea mmoja aliyeitwa Yasmir Al Fattar ambaye aliuawa miaka ya 1960 kwa kosa la kuwalawiti watoto wa kiume zaidi ya ishirini na hivyo nyumba zake zote kulaaniwa na kutelekezwa na hakutakiwa mtu yeyote kuingia humo, na kama mtu yeyote angeingia basi angelaaniwa yeye na kizazi chake, hivyo watu hawakutaka hata kuzisogelea nyumba hizo ambazo zilibaki magofu.

Wakasonga mbele na baada ya dakika tano ndipo wakaanza kuingia katika mtaa huo wa Khuwair ambapo ndipo kulipokuwa na kiwanda hicho walichokubaliana. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na hofu na gari lao, kila lilipopita, watu hawakuwa na habari nao, hawakujua kwamba ndani ya gari hilo kulikuwa na mtu aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba.

Wakati wakiwa wamebakiza kama umbali wa mita mia moja tena huku kwa mbali wakimuona Kareem akiwa anawasubiri nje ya kiwanda hicho, ghafla wakaanza kusikia king’ora cha gari la polisi nyuma yao na kutakiwa kusimama.

“Mungu wangu! Polisi!” alisema Hassan huku akiangalia nyuma.
“Ooppss..Tufanye nini? Nisimamishe gari’ aliuliza Hussein.
“Hapana! Kata kona!”
“Kuelekea wapi?”
“Kurudi nyuma tulipotoka.”
“Tulipotoka?”
“Ndiyo! Hatutakiwi kumsogelea Kareem, vinginevyo tutamharibia,” alisema Hassan. Alichokifanya Hussein ni kukata kona na kuanza kurudi nyuma, wakawa wakiangaliana na gari la polisi ambalo liliwataka kusimama.

Wakawapita, polisi wale hawakutaka kukubali, wakahisi kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta alikuwa ndani ya gari hilo, walichokifanya, nao wakaligeuza gari na kuanza kuwafuata watu hao.

“Twende wapi? Mafuta yameanza kuisha?”
“Unasemaje?”
“Mafuta yameanza kuisha!” alisema Hussein, mlio wa kuashiria kwamba mafuta yameanza kuisha ukaanza kusikika.
“Tumekwisha! Tufanye nini? Turuke garini?” aliuliza Hussein, gari hilo lingeanza kupunguza mwendo na kusimama muda wowote ule.

Hassan akainamisha kichwa kwa sekunde kadhaa. Alipokiinua, alikuwa na wazo jingine kabisa ambalo lilimshtua na kumshangaza kila mmoja. Hata kama lilionekana kuwa la hatari, hawakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima kulitekeleza haraka iwezekanavyo.

Je, ni wazo gani alilolipata Hassan kiasi cha kila mtu kumshangaa?

Je, Saida ataweza kufikishwa Dubai salama?
Usikose Saa moja Jioni

About Author

Advertisement

Post a Comment Blogger

Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii

Note: Only a member of this blog may post a comment.

 
Top