Na. Ahmed Mmow, Lindi.
Watu kumi wamefariki dunia na wengine 44 wamejeruhiwa kutokana na ajali ya Basi la kampuni ya Barcelona iliyo tokea jana katika kijiji cha Miteja wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii kutoka wilayani Kilwa, mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai, amesema ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Miteja, baada ya gari ya abiria ya kampuni ya Barcelona iliyokuwa inatoka jijini Dar-es-Salaam kwenda Tandahimba mkoa wa Mtwara, kupinduka baada ya kupasuka gurudumu la mbele.
Ngubiagai ambae pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo amesema ajali hiyo imesababisha vifo vya watu 10 na wengine 44 kujeruhiwa.
"Ajali imetokea leo(Jana) saa nne asubuhi, changamoto iliyopo hapa nikwamba chumba cha kuhifadhia maiti hakina majokofu ya kutosha kuhifadhia maiti kumi, tunaangalia uwezekano wa kusafirisha miili hiyo hosipitali ya mkoa," alisema Ngubiagai.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri kuangalia usalama na uhai wa abiria badala ya faida pekee.
Akibainisha kuwa pamoja na mwendo wa kasi, lakini pia ajali hiyo imechangiwa na uchakavu wa magurudumu.
"Tairi(magurudumu) za gari ile ni vipara kabisa, hata kondakta analalamika nakusema mara kadhaa walimshauri mmiliki anunue tairi mpya lakini hakuwasikiliza," alisema Ngubiagai.
Pia mkuu huyo wawilaya amelaumu umakini wa askari wa usalama barabarani kwa kuruhusu gari hiyo iendelee na safari kutoka Dar-es-Salaam hadi eneo iliyopata ajali wakati waliona magurudumu yake yalikuwa hayafai.
Kwa upande wake, kamanda wa polisi wa mkoa wa Lindi, kamishna msaidizi mwandamizi wa polisi, Renatha Mzinga. Amethibitisha kutokea ajali hiyo, nakuzitaja namba za usajili za gari hiyo aina ya Yu Tong, kuwa ni T110CCU. Ambae nae alisema "Licha ya kutembea kwa mwendo mkali,lakini lakini ilizidisha abiria, kwasababu uwezo wake ni kubeba watu 48. Hatahivyo ilibainika kwamba ilipakia watu 54.
Kamanda Mzinga alisema kati ya majeruhi hao, watano wana hali mbaya.
"Majeruhi wa nne wanatibiwa katika hospitali ya Tingi,ambapo arobaini wanatibiwa katika hospitali ya wilaya ya Kilwa" alisema kamanda Mzinga.
Huku akibainisha kwamba dereva wa gari hiyo bado hajapatikana na hata jina lake halijapatika. Ambapo kondakta wake ambae pia jina lake hajatambulika, anaendelea kupata matibabu katika hosipitali ya wilaya.
Juhudi za kumpata mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Kilwa, Dkt Vitalis Katalyeba hazikufanikiwa. Baada ya simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa.
****************
Post a Comment Blogger Facebook
Toa Maoni Yako Kuhusu habari Hii
Note: Only a member of this blog may post a comment.