Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akikata utepe huku viongozi wengine wakiushikilia kuashiria uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akipata picha ya kumbukumbu viongozi wengine baada ya uzinduzi rasmi wa Daraja la Kigamboni katika wilaya mpya ya Kigamboni jijini Dar es salaam leo Aprili 19, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli amekataa daraja la Kigamboni lisiitwe ‘Daraja la Magufuli’ na badala yake ameshauri lipewe jina la muasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Akiongea wakati wa kuzindua daraja hilo leo, Rais Magufuli amesema kuwa awali aliletewa mapendekezo na waziri mwenye dhamana akimtaka aridhie daraja hilo lipewe jina lake, lakini kwakuwa wazo la ujenzi huo lilianza tangu wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere, alikataa na kushauri jina la Nyerere litumike .
“Nilikataa lisiitwe kwa jina langu kwa sababu wazo la ujenzi wa daraja hili lilianza mwaka 1979 wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere.
“Wazo hilo halikufanikiwa kutokana na ukosefu wa pesa wakati huo. Mwalimu Nyerere ni kiongozi aliyejenga misingi imara katika taifa letu.
“Alikuwa ni kiongozi asiyebagua mtu kwa misingi ya dini, chama au kabila. Alifanikiwa kutuunganisha watanzania wote bila kujali itikadi zetu.
“Leo hii, daraja hili limekamilika, ni daraja ambalo halitambagua mtu kwa sababu wa CCM watapita hapa, wa Chadema watapita hapa na bahati nzuri mstahiki Meya wa jiji hili ambaye ni Chadema naye yuko hapa na amepita katika daraja hili.
“Ndugu zangu sistahili sifa zozote, najua nimefanikisha ujenzi huu nikiwa waziri wa ujenzi, lakini wakati huo nilikuwa natimiza wajibu wangu kama mtumishi wa umma, hivyo nashauri hili daraja liitwe daraja la Nyerere ili tuweze kumuenzi mwasisi wa taifa hili” alisema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanalitunza daraja hilo katika kujenga uchumi wa taifa.
TAZAMA VIDEO YA HUTOBA YAKE: