KAMPUNI YA TOTAL AFRIKA YAMHAKIKISHIA RAIS MAGUFULI KUANZA UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA KUTOKA UGANDA HADI TANGA HIVI KARIBUNI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU

Simu : +255-22-2114512, 2116898
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi : 255-22-2113425
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM,
TANZANIA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw. Javier Rielo amemuhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kuwa kampuni hiyo itaanza ujenzi wa mradi wa bomba la kusafirisha Mafuta kutoka nchini Uganda hadi bandari ya Tanga hapa Tanzania haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.

Bw. Javier Rielo ametoa ahadi hiyo leo tarehe 14 Machi, 2016 alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es salaam.

Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na utarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.

Katika Mazungumzo hayo Bw. Javier amemueleza Rais Magufuli kuwa Kampuni yake inatarajia kutumia dola za kimarekani karibu bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa.

Pamoja na kuukaribisha uwekezaji huo mkubwa kwa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameitaka kampuni hiyo kuharakisha mchakato wa kuanza kwa mradi, na ameshauri muda wa miaka mitatu uliopangwa kuukamilisha mradi huo upunguzwe, ili manufaa yake yaanze kupatikana mapema.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo, amesema Wizara yake ipo tayari kuhakikisha mradi huo unafanikiwa, na itatoa ushirikiano wa kutosha kuharakisha utekelezaji wake.

Prof. Mhongo amebainisha kuwa licha ya kwamba hali ya kijiografia, hali ya hewa na bandari ya Tanga vinatoa mazingira bora ya kufanikiwa kwa mradi huo, Tanzania pia inatarajia kunufaika na bomba hilo, kwa kuwa kuna tafiti mbili za mafuta zinazoendelea katika ziwa Tanganyika na katikati mwa Tanzania, ambazo zikikamilika kwa mafanikio inatarajiwa bomba hilo litasaidia kusafirisha mafuta yake.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
14 Machi, 2016
Ikulu
RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AKIAGANA NA MAKAMU WA RAIS WA KAMPUNI YA TOTAL AFRIKA BWANA JAVIER RIELO WAKATI ALIPOTEMBELEA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

*****************************
TAZAMA VIDEO :: RAIS MAGUFULI AKUTANA NA MAKAMU WA RAIS WA TOTAL AFRICA MASHARIKI
Previous Post Next Post