Mgomo wa Madereva uliodumu kwa takriban siku moja na ushee, hatimaye umepata muafaka baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Paul Makonda (pichani) kufanikiwa kuusuluhisha kwa kusaini makubaliano na Uongozi wa Chama cha Madereva.
Makubaliano hayo yaliitaka Serikali kuboresha Mikataba kwa Madereva, malipo kwa madereva hao, pamoja na tatizo la ukaguzi wa magari ili kuondoa usumbufu kwa madereva hao, na kuiomba Serikali kufanya ukaguzi huo kwa siku moja tu.
Akizungumza na Madereva hao, Mhe, Makonda amewataka Madereva hao kuachana na mgomo huo na kuwaahidi Madereva hao kuyafanyia kazi madai yao katika muda ambao wamekubaliana usiozidi saa 4 asubuhi kesho.
Aidha, Mhe Makonda amesema katika madai hayo imeundwa Tume ambayo itashughulikia madai hayo pamoja na kuwahakikishia Madereva hao kuwepo na mwakilishi katika Tume hiyo iliyoundwa, ambayo itajadili masuala ya Mkataba, malipo, matibabu pamoja na suala la kusoma kwa Madereva hao.
Pia Makonda amelitaka Jeshi la Polisi kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni kuwaachia Madereva ambao tayari walikua wamekamatwa kutokana na kuonekana kufanya fujo katika mgomo huo katika Soko la Urafiki jijini Dar es Salaam.
Kwa Upande wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Madereva, Bw. Rashidi Salehe amemuomba Mkuu wa Wilaya kutatua madai ya Madereva hao ili kuondoa mgomo ambao unakwamisha usafirishaji wa abiria.
HALI ILIVYO KUWA KABLA YA UTATUZI HUO MAPEMA ASUBUHI YA LEO...
Baadhi ya Madereva na Makondakta wa Mabasi wanaondelea na Mgomo, wakiwa wamekaa juu ya Kontena zilizopo kwenye Kituo kikuu cha Mabasi, Ubungo jijini Dar es salaam kusubiria mustakabali wao, huku ulinzi Mkali wa Jeshi la Polisi ukiwa umetawala eneo hilo.
Ghafla likazuka tukio la kurushwa mawe kutoka kwa watu wasiojulikana waliokuwa nje ya Stendi hiyo na kupeleke watu wote waliokuwa kwenye eneo hilo kukusanyika sehemu moja ili kujinusuru.
Hali ilikuwa tete pale mawe yalipokuwa yakirushwa, na kupelekea baadhi ya viongozi pamoja na wanahabari waliokuwepo kwenye eneo hilo kukusanyika sehemu moja. hivyo polisi walilazimika kutumia mbinu zao na kufanikiwa kulituliza tukio hilo.