Baadhi ya Mdiwani wa jiji la Arusha wakiongozwa na Meya wa jiji hilo Gaudence Lyimo kulia ,wakiwa wamebeba jeneza la Belina Kabuje ambaye alikuwa diwani wa viti maalumu jijini Arusha kuelekea katika katika kanisa la Parokia Mtakatifu ngarenaro jijini hapa jana.
Baadhi ya vijana wa jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM(Uvccm) wilayani Arusha wakibeba mwili wa marehemu Belina Kabuje ambaye alikuwa diwani wa viti maalumu jijini Arusha kuelekea katika eneo la mazishi eneo la Oljoro nje kidogo ya jiji la Arusha jana
Anayetajwa kuwania jimbo la Arusha mjini Mustafa Panju mwenye asili ya Kiasia Mtanzania akiwa katika ibada hiyo jana katika kanisa hilo
Na. Mwandishi Wetu, ArushaMazishi ya diwani wa viti maalumu jijini Arusha, marehemu Belina Kabuje ambaye alifariki hivi karibuni katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi jana yalitawaliwa na huzuni na hisia mbalimbali mara baada ya familia ya marehemu kuzuiwa isipokee fedha za rambirambi.
Fedha hizo zilizuiwa na meya wa halmashauri ya jiji la Arusha, Gaudence Lyimo wakati akitoa salamu za rambirambi ndani ya kanisa Katoliki Parokia ya Roho Mtakatifu Ngarenaro wakati mwili wa marehemu ulipofikishwa kwa ajili ya ibada.
Akizungumza wakati akitoa salamu hizo bila kutaja kiasi chake meya huyo alisema kuwa fedha zote zilizokusanywa kama rambirambi ya marehemu hazitakabidhiwa mbele ya familia yake hadi pale utaratibu wa kufungua akiba utakapokamilika.
Alisema kuwa lengo la kuweka utaratibu huo ni kuepusha matumizi mabaya ya fedha hizo kutumika hovyo huku akisisitiza ya kwamba marehemu enzi za uhai wake alikuwa mtu mwenye hofu na mashaka.
"Marehemu enzi za uhai wake alikuwa na hofu sana kuna mambo mengine yalikuwa ni siri kwa familia lakini alilazimika kutushirkisha sisi madiwani"alisema Lyimo
Hatahivyo, katika hali isiyo ya kawaida baadhi ya waombolezaji waliohudhuria kanisa hapo walijikuta wakipiga makofi kushangilia hotuba ya meya huyo pale alipotamka ya kwamba mali za marehemu huyo kamwe hazitaguswa na mtu yoyote kwa kuwa kuna wosia umeachwa na marehemu.
Naye, mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) mkoani Arusha, Flora Zelothe aligusa hisia za watu kanisani hapo mara baada ya kutamka kwamba marehemu aliacha wajukuu watatu ambao alikuwa akiwahudumia na kudai kimsingi wanapaswa kutambuliwa na familia.
Hatahivyo, paroko wa kanisa hilo, Anchi Mpota akiendesha ibada ya kumuombea marehemu huyo aliwataka watu kuondoa tofauti zao za kidini, kikabila na kisiasa kwa madai kwamba zitawagawa.
"Kwa hali ilivyo sasa amani tuliyonayo tusiichezee tuondoe tofauti zetu za kidini, kisiasa na kikabila kama tukiziendekeza basi zitatugawa" alisema paroko huyo