Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoa hotuba ya uzinduzi rasmi wa Klabu Zalendo iliyoko katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu tarehe 10.5.2015. Aliyekaa kushoto kwa Mama Salma ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi Bwana Yahaya Nawanda na kulia ni Mwenyekiti wa Klabu Zalendo Mwalimu Mwajuma Malugu.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akijumuika na wanachama wa Klabu Zalendo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kucheza wimbo wa ‘NANI KAMA MAMA’ muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi klabu hiyo inayoundwa na walimu, wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari pamoja wa wananchi mbalimbali katika Manispaa hiyo.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea kwa kuyapungia mkono maandamano ya wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari katika Manispaa ya Lindi ambao ni wanachama wa Klabu Zalendo wakiongozwa na chipukizi kwenye Uwanja wa Ilulu wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi wa klabu hiyo tarehe 10.5.2015
Vijana wa chipukizi kutoka Klabu Zalendo katika Manispaa ya Lindi wakionyesha michezo ya halaiki wakati wa sherehe za uzinduzi rasmi wa klabu yao uliofanywa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye uwanja wa Ilulu tarehe 10.5.2015.
(PICHA ZOTE NA JOHN LUKUWI).
Na: Ahmad Mmow, Lindi.
Wananchi Mkoani Lindi na nchini kwa ujumla wameaswa kuwa wazalendo na kuwapuuza wanaobeza muungano. Wito huo umetolewa Jana na mjumbe wa halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi, ambye pia ni mke wa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, Salma Kikwete wakati wa uzinduzi wa klabu ya wazalendo, Uliofanyika katika uwanja wa Ilulu, manispaa ya Lindi.
Salma alisema muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unaendelea kudumu na kuwa imara ni matokeo ya uzalendo na juhudi kubwa zilifanywa na waasisi wa taifa hili. Hivyo kuubeza muungano huo ni kuwasaliti wa waasisi hao, jambo ambalo siyo jema.
Kwani nchi nyingi zinausifu muungano huu. "Epukeni maneno ya baadhi ya wanasiasa wanaoubeza muungano huu, mkiwasikiliza mtaharibikiwa," alisisitiza Salma.
Alisema uzalendo ndio njia pekee itayowafanya wananchi wajione kuwa niwamoja na kuepuka ubaguzi unaoweza kuondoa upendo. Alitahadharisha kuwa iwapo wananchi wakikosa upendo, kunauwezekano mkubwa wa amani kutoweka.
Alibainisha na kufafanua kuwa uzalendo ni pamoja kuyakataa matendo ambayo yatakwamisha na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi. Alisema wananchi hawanabudi kuwazuia na kuwapuuza wale wote wanaotenda vitendo vinavyoharibu na kukwamisha maslahi ya umma.
Aidha mjumbe huyo wa halmashauri kuu ya taifa ya CCM aliwaasa wananchi, viongozi na watendaji wa serikali na vyama vya siasa, kutanguliza maslahi ya taifa na kuepuka ubinafsi ambao unasababisha kutanguliza maslahi yao badala ya maslahi ya umma.